span style="color: #000080;">
Miss Singida 2014 Dorice Mollel akizungumza muda mfupi kabla ya kukabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 1.2 milioni kwenye wodi ya watoto njiti ya hospitali ya mkoa mjini Singida. Miss Singida huyo ambaye mwaka jana alikuwa pia mshindi wa kwanza Miss kanda ya kati na kushika nafasi ya tatu katika shindano la kumsaka Miss Tanzania, amesema ametoa msaada huo kwa sababu na yeye alizaliwa mapacha njiti.
Na Nathaniel Limu, Singida
JUMLA ya watoto 284 hadi 300, huzaliwa kila mwaka katika hospitali ya mkoa iliyopo mjini Singida wakiwa hawajatimiza umri wa kawaida wa kuzaliwa (njiti).
Kati ya watoto hao,inakadiriwa 60 hadi 83 hufariki kutokana na sababu mbalimbali kila mwaka ikiwemo ya tatizo la kupumua.
Hayo yamesemwa na kaimu mganga mfawidhi hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida,Dk.Daniel Tarimo,wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada wa vifaa tiba vitakavyotumika kwenye wodi ya watoto njiti katika hospitali ya mkoa mjini hapa.
Kuhusu watoto hao njiti wanaofariki dunia,Dk.Tarimo alisema vifo vingi vinachangiwa na baadhi ya akina mama wajawazito kujifungulia nyumbani mahali hakuna wataalamu wa huduma ya afya.
“Watoto wa aina hii kwa kawaida wanakuwa na matatizo ya kupumua.Sasa mama akijifungulia nyumbani,wakiwa njiani kukimbiza watoto/mtoto wa aina hiyo hospitalini,mtoto/watoto husika hupata tatizo la kupumua linalopelekea vifo vyao”,alifafanua zaidi Dk.Tarimo.
Miss Singida 2014 Dorice Mollel akimkabidhi Kaimu Mganga Mfawidhi Hospital ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dk.Daniel Tarimo, msaada wa vifaa mbali mbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 1.2 milioni kwa wodi ya watoto njiti.
Kaimu mganga huyo,alitumia fursa hiyo kuwakumbusha akina mama wajawazito kujenga utamaduni wa kuanza mapema kuhudhuria kliniki ili endapo watagundulika wana tatizo,waweze kuhudumiwa mapema kabla tatizo husika halijaleta madhara makubwa.
Aidha, Kaimu Mganga Huyo Mfawidhi,amemshukuru Miss Singida 2014 Dorice Mollel kwa kutoa msaada huo wa vifaa tiba kwa ajili ya wodi ya watoto njiti.Amewataka wadau wengine kuiga kitendo hicho.
Kwa upande wake Miss Singida 2014, Dorice Mollel alisema amechukua hatua hiyo ya kusaidia watoto njiti kwa madai kuwa na yeye alizaliwa akiwa njiti pacha na kwa vyo vyote kuna watu walijitolea kuwasaidia katika kipindi hicho.
Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dk.Daniel Tarimo, akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya tiba vilivyotolewa msaada na Miss Singida 2014 Dorice Mollel kwenye wodi ya watoto njiti hospitali ya mkoa wa Singida.
Aidha,alisema hatua hiyo ni kuiunga mkono serikali katika kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini.Ametaka wadau wengine kusaidia kundi hilo la watoto ili kuwapunguzia matatizo mbalimbali yanayowakabili wakati wa ukuwaji waoa.
Kwa mujibu wa Miss Singida 2014, Mollel baadhi ya vifaa hivyo ni suction mashine-manual na electronic na mizani vyote vina thamani ya zaidi ya shilingi 1.2 milioni.Mollel pia ni Miss kanda ya kati na alikuwa mshindi wa tatu katika shindano la kusaka Miss Tanzania la mwaka jana.
Miss Singida 2014 Doris Moleli,akimwangalia mtoto mchanga aliyelazwa kwenye wodi ya uzazi kawaida iliyopo kwenye hospitali ya mkoa mjini Singida.
Miss Singida 2014, Dorice Mollel akiangalia watoto njiti pacha waliolazwa katika hospitali ya mkoa mjini hapa.(Picha na Nathaniel Limu).