BREAKING NEWS

Thursday, January 29, 2015

SEMINA INAYOHUSIANA NA MATUMIZI YA GESI ASILIA HAPA NCHINI YAZINDULIWA NA NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: KITWANGA

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga akifungua rasmi semina kuhusu matumizi ya gesi asilia iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Japan Tanzania, Masaki Okada akizungumza na wadau na wataalamu wa gesi asilia (hawapo pichani) waliohudhuria semina ya matumizi ya gesi asilia iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam.
Wataalamu na wadau wa gesi asilia kutoka Japan na Tanzania wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa semina ya matumizi ya gesi asilia iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Kamishna Msaidizi Nishati (Gesi), Mhandisi Norbert Kahyoza (wa kwanza kulia) akifuatilia uwasilishaji wa mada kwenye semina iliyohusu matumizi ya gesi asilia iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Na Mohamed Saif
Wizara ya Nishati na Madini imeishukuru Serikali ya Japan kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Japan (JICA) kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo nchini na kuahidi kuuendeleza ushirikiano huo.

Shukrani hizo zilitolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga kwa Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada wakati akifungua semina kuhusu matumizi ya gesi asilia iliyoandaliwa na JICA kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini na kuhudhuriwa na wadau na wataalamu wa masuala ya gesi kutoka nchini Japan na Tanzania.

Naibu Waziri Kitwanga alieleza kuwa Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na wa muda mrefu na Watu wa Japan na Serikali yao. Aidha, alibainisha kuwa uhusiano huo ulianza tangu mwaka mwaka 1966 na akisisitiza kuuenzi na kuuendeleza uhusiano uliopo.

Akizungumzia umuhimu wa semina hiyo, Kitwanga alisema ni wakati muafaka kwa wataalamu wa Tanzania kuwa na uelewa mpana zaidi kwenye masuala mbalimbali yanayohusu gesi asilia na mafuta kwa manufaa ya taifa.

“Semina hii ni fursa nzuri kwa wadau na wataalamu wetu wa masuala ya gesi kwa kuwa imelenga kuainisha matumizi mbalimbali ya gesi asilia. Ni imani yangu kupitia wadau na wataalamu mliohudhuria semina hii, Watanzania wataelewa namna gani watafaidika na gesi asilia. Tuitumie semina hii vizuri kwa ajili ya kuliletea maendeleo taifa letu,” alisema Kitwanga.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanafaidika na rasilimali ya gesi asilia kutokana na fursa mbalimbali zinazotokana na uwepo wa gesi asilia nchini ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali katika kampuni zinazojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi.

Aidha, Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada alimuhakikishia Naibu Waziri Kitwanga kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika miradi mbalimbali ya kiuchumi.

Balozi Okada alisisitiza umuhimu wa Tanzania kujipanga vizuri katika kuhakikisha gesi asilia inaleta maendeleo makubwa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwatumia wataalamu kutoka Japan.

“Semina hii itahusisha mada mbalimbali ambazo zitatolewa na wataalamu waliobobea katika masuala ya gesi asilia, ni matumaini yangu wadau na wataalamu mbalimbali mtanufaika na mada ambazo wataalamu hawa kutoka Japan wameandaa,” alisema Balozi Okada.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates