BREAKING NEWS

Monday, January 19, 2015

HIVI NDIO VITU AMBAVYO MTUHUMIWA SUGU WA UJAMBAZI ALIEKAMATWA MKOANI SIMIYU

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga SCP Charles Mkumbo akionesha nguo ambazo zilikutwa kwa Mtuhumiwa kiongozi huyo wa genge la uhalifu ambazo zinasemekana ni za baadhi ya watu waliouawa wakiwemo majambazi aliokuwa akishirikiana nao ambao aliwauwa kwa maslahi yake.
"Hii ni mifupa tuliyoikuta nyumbani kwa mtuhumiwa".
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,SACP Valentino Mlowola akiwa na makamanda wenzake SACP Charles Mkumbo (Shinyanga) na  SACP Justus Kamugisha (Simiyu) wakati wakizungumza na waandishi wa habari kufuatia kutiwa mbaroni kwa mtuhumiwa wa ujambazi ambaye pia ni mfanyabiashara aitwaye Njile Samweli (46) marufu kwa “John” wa mjini Bariadi mkoani Simiyu, aliyekuwa akifanya matukio ya uhalifu katika Mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida na Tabora.
Sehemu ya vitu vilivyokutwa kwa mtuhumiwa huyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu,SACP Justus Kamugisha akiwasilisha taarifa kwa waandishi wa habari.

PICHA NA HABARI NI KWA HISANI YA GSENGO BLOG.
JESHI la Polisi limefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa wa ujambazi ambaye pia ni mfanyabiashara aitwaye Njile Samweli (46) marufu kwa “John” wa mjini Bariadi mkoani Simiyu, aliyekuwa akifanya matukio ya uhalifu katika Mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida na Tabora.

Wakizungumza na waandishi wa Habari jijini Mwanza, Makamanda wa Polisi SACP Valentino Mlowola (Mwanza),SACP Charles Mkumbo (Shinyanga) na  SACP Justus Kamugisha (Simiyu), walisema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ni mfanyabiashara wa mjini Bariadi mkazi wa kijiji cha Lyoma alikamatwa  Januari 5 mwaka huu wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.

Kamanda Mlowola alieleza kuwa kukamatwa kwa kiongozi huyo hatari wa kundi la ujambazi katika mikoa hiyo kumetokana na kukamatwa kwa mmoja wa washirika wa kundi lake Januari 5 jijini Mwanza kutokana na taarifa za siri kutoka kwa raia wema waliotoa kwa Jeshi la Polisi,hali iliyopelekea kuundwa kikosi kazi kushirikisha mikoa hiyo cha kufatilia mtandao huo na kufanikiwa kuwakamata.

Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Mabula Lyanga (36) maarufu kwa jina la Magana mkazi wa kijiji cha Bugarama wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu akiwa na jeraha la kupigwa risasi na jambazi mwenzake aitwaye Njele (Kiongozi wa kundi) kwenye bega lake la kulia kutokana na raia wema kumtilia mashaka na kuanza kumfatilia na kunaswa na polisi.

“Baada ya kumkamata mtuhumiwa huyu wa ujambazi katika mahojiano na askari wetu alimtaja mtuhumiwa mwenzake Njile kupiga risasi wakiwa katika harakati za tukio la ujambazi wa kutumia silaha katika kijiji cha Idukilo Kata ya Luhumbo Mwadui wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga Januari 5 mwaka huu,”alieleza.

Kamanda Mlowola alisema kuwa watuhumiwa hawa baada ya kufanya uhalifu huo na uporaji na kutofautiana na kiongozi wake Njile,alimfyatulia risasi mbili na kumjeruhi kwenye bega, tuliwatuma askari wa Idara ya Upelelezi kutoka Mwanza kwenda kufatilia na kufanya msako mkali kwa kushirikiana na wenzao wa Bariadi mkoani Simiyu.

“ Kikosi kazi chetu kilifanikiwa kumkamata Njile na katika mahojiano naye binafisi alikiri kuhusika na tukio hilo na kuelezea kufanya matukio mengine mengi katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora ikiwemo kuwauwa washirika wenzake na kuwataja wengine ikiwemo alipokuwa amehifadhi silaha (SMG) risasi 331 na Magazine tisa vilivyotumika,”alisema.

SACP Mlowola alitaja matukio kadha waliyofanya watuhumiwa hao katika Mkoa wa Mwanza kuwa ni pamoja na kuvamia na kupora fedha kiasi cha Sh milioni 3,500,000/= katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Samba katika Kisiwa cha Bulubi wilayani Ukerewe Agosti mwaka 2014, Oktoba 2 mwaka 2014 katika Kijiji cha Mahaha walivamia maduka kadhaa na kupora fedha kiasi cha Sh milioni 3 na Pikipiki moja na kumuua mtu mmoja.

Tukio jingine lilifanyika Oktoba 2014 eneo la Malya wilayani Ngudu ambapo walivamia na kupora fedha kiasi cha Sh milioni 2 na kumjeruhi mtu mmoja na wahusika wa matukio yote hayo walioshiriki ni Njile (kiongozi), Lyagwa (aliyepigwa risasi na Njile), Magingi Doto “Kafuru”,Thomas, Daniel Pastory, Mashauri Ngulyati, Kipisto Chenya.

Naye Kamanda SACP Mkumbo ( Simiyu), alisema kwamba baada ya kikosi kazi kufanya ufatiliaji kutokana na maelezo ya mtuhumiwa Njile walifanikiwa kukamata bunduki moja ya kivita (SMG) yenye namba BP 3402, risasi 331, Magazine tisa, mifupa na nguo zinazosadikiwa kuwa  ya marehemu waliouwawa na mtuhumiwa huyo.

Alisema mtuhumiwa huyo na washirika wake waliafanya matukio mengine ya uhalifu katika wilaya ya Itilima ,Maswa, Meatu ,Bariadi ambapo walipora Sh.20.5 milioni.

Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga, SACP Kamugisha,alisema watuhumiwa hao walifanya uhalifu katika wilaya ya Kishapu walikopora Sh.3.2 na simu aina ya Nokia pia walimjeruhi mwenzao (Mabula Lyagwa) kwa risasi kabla ya kumbeba na kumtelekeza mjini Maswa.

Alisema walifanya matukio mengine katika wilaya ya Igunga,kwa kupora simu na fedha,pia walipora mkoani Singida kiasai cha Sh.1.5 na hadi sasa jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa watano na wengine bado wanatafutwa, mara baada ya taratibu kukamilika watafikishwa mahakamani.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates