Mawaziri
waliobadilishwa wizara na Rais Jakaya Kikwete, wameingia ofisini na
kuahidi kutumia muda mfupi uliobaki kuendeleza yale yaliyoachwa na
watangulizi wao.
Mabadiliko hayo yalifanyika baada ya mawaziri
wawili kujiuzulu kutokana na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow. Ni
Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini na Profesa Anna Tibaijuka
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Rais Kikwete alimteuwa George Simbachawene
aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchukua
nafasi ya Profesa Muhongo na Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Sera, Uratibu na
Bunge akimrithi Profesa Tibaijuka.
Simbachawene alifika wizarani hapo Saa tano
asubuhi na kupokelewa na wafanyakazi wa wizara hiyo waliojipanga katika
mistari miwili, huku yeye akipita katikati yao.
“Tutaendeleza pale walipoishia wenzetu,
tutahakikisha umeme unaendelea kusambazwa nchini kwa kutumia Wakala wa
Umeme Vijijini (Rea), mafuta nayo tutashirikiana na (Ewura) Mamlaka ya
Udhibiti wa Nishati na Maji kuona bei zinashuka kulingana na bei za soko
la dunia.”
Aliongeza: “Gesi nayo tutahakikisha inatumika na
kuwanufaisha Watanzania, hususan itakapoanza kutumika kuzalisha umeme
katika Kituo cha Kinyerezi.”
Naye Mwijage alisema: “Nimeletwa katika wizara
ambayo nina uzoefu nayo kutokana na kuwa katika sekta ya nishati tangu
mwaka 1984, hivyo kama ni mchezo umepata mchezaji.”
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na
maendeleo ya Makazi, Lukuvi alisema: “Uamuzi ya kutatua migogoro ya
ardhi haihitaji fedha, hivyo watendaji wanatakiwa kutumia akili ili
mwananchi aweze kupata haki zao za msingi.”
Awali, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka amekabidhi ofisi kwa waziri Lukuvi, huku
akimkabidhi miradi ambayo hajaitekeleza katika kipindi chake cha
uongozi, ikiwamo mradi wa mpango mji wa Dar es Salaam.
Alisema miradi hiyo ameitekeleza kwa kiasi
kikubwa, huku mingine ikiwa na changamoto na kumtaka waziri Lukuvi
kutumia akili ya ziada kuikamilisha.
Hata hivyo, Tibaijuka alisema mipango miji haijapewa umuhimu na kuitaka Serikali kuangalia upya suala la upangaji miji.
Tibaijuka aliitaja miradi mwingine ni mradi wa Mji
wa Kigamboni unaohitaji Sh14.6 bilioni kukamilika, Sera ya Watumishi wa
Sekta ya Ardhi na Sera ya ubia na Serikali kumiliki mashamba makubwa.