WANAKIJIJI WAWAUA SIMBA WA HIFADHI TA TAIFA YA TARANGIRE, WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII ACHACHAMAA.


















Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inakadiriwa kuwa na Simba kati ya 200 hadi 250 na Tembo wanaokadiriwa kufikia 3,000 na wanyama wengineo zaidi ya 10,000.

Simba wanane waliotoka nje ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuingia eneo la Kijiji cha Kibaoni wilayani Babati mkoani Manyara, wameuawa kwa kuchomwa mikuki na wananchi.

Kijiji cha Kibaoni kipo hatua chache kutoka Hifadhi ya Tarangire ambayo ni mojawapo ya vivutio vya kitalii na mara nyingi wanyamapori huzagaa kijijini hapo, hasa nyakati za masika kuepuka majani marefu hifadhini.


Tukio hilo linaloelezewa kuwa ni janga kubwa kwa sekta ya uhifadhi na utalii nchini, lilitokea jana alfajiri na hadi Saa 6.00 mchana na mizoga saba ya Simba ilipatikana, huku mmoja akiaminika kufia kwenye vichaka baada ya kukimbia alipojeruhiwa.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ameziagiza mamlaka zinazohusika kuwasaka na kuwatia mbaroni wote waliowahamasisha na kuwaongoza wakazi wa kijiji hicho kuwaua Simba hao.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Nyalandu alitoa maagizo kwa polisi kuchunguza uhalali wa bunduki inayomilikiwa na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho iliyotumika kuwaua Simba wawili kati ya saba.


“Kuua idadi kubwa ya Simba kwa wakati mmoja, tena katika siku ya kwanza ya Mwaka Mpya ni jambo la kusikitisha na linastahili kulaaniwa na wote wenye mapenzi mema na uhifadhi ndani na nje ya nchi,” alisema Nyalandu na kuongeza:


“Hatuwakamati wakazi wote 100 walioshiriki kuwaua simba hawa, bali tutashughulika na wale waliochochea mauaji ili kutoa fundisho kwa wale wanaochukua sheria mkononi kwa kuwaua wanyamapori,” alisema Nyalandu.


Hifadhi ya Taifa ya Tarangire inakadiriwa kuwa na Simba kati ya 200 hadi 250 na Tembo wanaokadiriwa kufikia 3,000 na wanyama wengineo zaidi ya 10,000.


Mmoja wa wanakijiji aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa sababu za kiusalama, alisema Simba hao waliuawa baada ya kudaiwa kumla punda kihongwe kwenye moja wa maboma ya wakazi wa kijiji hicho ambao ni jamii ya wafugaji wa Kimasai.


“Usiku kundi la Simba zaidi ya 12 walionekana wakizunguka katika maeneo ya karibu na kambi ya Watalii ya Zion Campsite. Ilipofika alfajiri, watu wakaanza kupiga mayowe kuashiria hatari baada ya Simba hao kusambaa kijijini,” alisema na kuongeza;


“Kelele hizo ziliwashtua Simba na kuwafanya waanze kuunguruma, hali iliyozua taharuki na vijana (Morani), wakaanza kupambana nao na kuwaua mmoja baada ya mwingine hadi kufikia Simba saba na mmoja alikimbia akiwa na mkuki mwilini.”


Alisema vijana wawili walijeruhiwa vibaya baada ya Simba mmoja kuwashambulia.


Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete alisema mara nyingi mauaji ya wanyamapori wakali wakiwamo simba, chui, chita huambatana na kisasi cha wafugaji baada ya mifugo yao kujeruhiwa au kuliwa.


“Katika tukio hili, Simba hawakuvamia mifugo wala maboma ya wafugaji.


“Hawa walionekana tu kijijini. hawakuwa na madhara, wamewaua kwa makusudi,” alisema Shelutete.


Alisema hata kama kungekuwepo uvamizi, askari wa TANAPA wangefika eneo hilo ndani dakika zisizozidi tano iwapo wangetaarifiwa kwa sababu eneo hilo liko hatua chache kutoka makao makuu ya hifadhi ya Tarangire.


Mkuu wa mkoa wa Manyara, Joe Bendera, aliyeripoti kituo chake hicho kipya cha kazi wiki iliyopita alitembelea eneo la tukio jana asubuhi na kushuhudia mizoga ya Simba hao ambayo baadaye yalihamishiwa makao makuu ya hifadhi ya Tarangire.


Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas licha ya kukiri kupata taarifa za tukio hilo, alisema linapaswa kuzungumziwa ni Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, Mrakibu Mwandamizi Christopher Fuime. Eneo la tukio liko mpakani mwa mikoa ya Arusha na Manyara.


Akizungumza kwa njia ya simu jana mchana, Kamanda Fuime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulizungumzia tukio hilo baada ya kukamilisha ukusanyaji wa taarifa zote muhimu kutoka eneo hilo

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post