Utata mpya umeibuka kuhusu matokeo ya Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa baada ya wagombea watatu waliotangazwa washindi
kuwekwa kando ikidaiwa kuwa badala yake walioshindwa waliapishwa
kuchukua nafasi zao, hali iliyozua vurugu kubwa zilizotulizwa na polisi
kwa mabomu ya machozi Ubungo jana.
Kutokana na hali hiyo, wafuasi wa CUF wanaodai
wagombea wa chama chao ndiyo walioshinda, waliibuka na kutanda nje ya
Hoteli ya Landmark kupinga kuapishwa kwa baadhi ya wenyeviti wa Serikali
za Mitaa wa CCM katika Wilaya ya Kinondoni, hatua iliyosababisha baadhi
ya wagombea na mashabiki kushushiwa kipigo hadi polisi walipoingilia
kati kwa kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.
Vurugu hizo zilizodumu kuanzia saa tatu hadi saa
tano asubuhi, zililenga kuzuia wateule watatu wa mitaa ya Ukwamani,
Pakacha na King’ong’o kuapishwa kwa madai kuwa siyo walioshinda.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa
Msisiri, Juma Mbena alivamia eneo hilo akidai kuwa Gasper Chambembe
(CUF), ambaye alishinda katika mtaa huo hakustahili kuapishwa, kitendo
kilichosababisha ashushiwe kipigo na wafuasi wa CUF.
Licha ya Mbena kupigwa na kuchaniwa nguo, pia
Sultan Jetta (CCM) ambaye alitangazwa kushinda katika Mtaa wa Ukwamani,
Kawe alizuiwa na wafuasi wa CUF kuapishwa, wakidai kuwa mgombea wao,
Nasri Mohammed Mashaka ndiye aliyestahili kuapishwa. Alipogoma,
walimkamata na kumshushia kipigo hadi alipookolewa na polisi.
Baadaye Jetta alirudishwa ukumbini chini ya ulinzi
wa polisi na kuapishwa pamoja na wenyeviti wenzake 153 kati ya 191 wa
Wilaya ya Kinondoni.
Aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa Pakacha Kata ya
Tandale, Hussein Juma Mpeka (CUF) alidai kuwa licha ya uchaguzi huo
kuvurugika, alipewa barua ya kuitwa kuapishwa lakini baada ya kufika
eneo hilo alikataliwa kuingia ukumbini, badala yake aliyeruhusiwa ni
Nassib Omary Kalenga wa CCM.
Hali ilivyokuwa
Shughuli ya kuapisha wenyeviti hao ilianza saa
mbili asubuhi na baada ya saa moja, wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya
manispaa hiyo walikusanyika eneo hilo ili kushuhudia uapishwaji huo.
Kati yao walikuwapo viongozi wa vyama vya CCM na
CUF wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na wagombea walioeleza kuwa walishinda
katika uchaguzi na matokeo yao kutangazwa lakini hawakupewa barua za
uthibitisho kutoka kwa mamlaka husika.
Waendesha bodaboda na wananchi wanaofanya biashara
zao kando ya hoteli hiyo nao walikusanyika kwa lengo la kushuhudia
kinachoendelea hali iliyowafanya polisi waliokuwa katika magari mawili
aina ya Landrover Defender kuwataka wananchi hao kuwa watulivu.
Mmoja wa wakazi wa Kawe, Anna Cheupe aliyekuwa
eneo hilo alisema licha ya kuwa ni mwanachama wa CCM, hakufurahishwa na
kitendo cha matokeo ya Mtaa wa Ukwamani kubadilishwa, kauli ambayo
iliungwa mkono na watu waliokuwa karibu yake.
CHANZO:mwananchi
CHANZO:mwananchi
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia