Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kesho itawasha moto upya bungeni
wakati itakaposoma ripoti maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), ikitarajiwa kuibua kashfa tatu nzito ikiwamo ya
misamaha ya kodi.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana
na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe zilisema kuwa,
tayari kamati hiyo imepokea ripoti ya ukaguzi huo ambayo inaonyesha
ufisadi wa kutisha katika maeneo hayo matatu na mengineyo.
Masuala hayo matatu pia yaliibuka
wakati wa vikao vya kamati za Bunge vilivyomalizika Dar es Salaam wiki
iliyopita, huku bodi ya korosho ikibanwa kuhusu nyumba yake aliyouziwa
Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka.
Kwa mujibu wa habari hizo, ripoti
hiyo inayoonyesha jinsi ufisadi wa kutisha ulivyofanywa katika ujenzi wa
jengo la (VIP Lounge) na Serikali inadai ilitumia Sh12 bilioni
kulijenga, lakini mthamini wa majengo ya Serikali ameeleza kuwa jengo
hilo lina thamani ya Sh3 bilioni.
Katika suala la misamaha ya kodi, PAC
imepokea taarifa kutoka kwa CAG ikionyesha kuwa misamaha hiyo iliyokuwa
imefikia Sh1.5 trilioni mpaka Juni 2013, lakini baada ya mwaka moja
misamaha hiyo imeongezeka hadi Sh1.8 trilioni mpaka Juni 2014.
“Kwa mwaka moja tu, misamaha ya kodi
imeongezeka kwa zaidi ya Sh300 bilioni. Kiasi hiki ni kama escrow fulani
(Fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, Sh306 bilioni),” chanzo cha habari
kilidokeza.
Katika vikao vya kamati hiyo, Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) ilieleza kuwa misamaha ya kodi imepanda kutoka
Sh1.4 trilioni mwaka 2012/13 hadi Sh1.8 trilioni mwaka 2013/14, chanzo
kikiwa ni misamaha ya kodi katika miradi mikubwa. Ilisema kati ya
misamaha hiyo, Sh676 bilioni zinatokana na misamaha ya kodi inayotokana
na Ongezeko la Thamani (VAT) na kuwa hali hiyo itapungua iwapo nchi
itaanza kutumia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia, TRA ilifafanua kuwa mpaka sasa
wafanyabiashara na kampuni kubwa zimefungua kesi katika mahakama ya
rufaa wakipinga kulipa kodi ambayo inafikia Sh1.7 trilioni.
Mvutano mwingine unaotarajiwa kuibuliwa katika ripoti hiyo ni uwasilishwaji wa utata wa uuzwaji wa nyumba ya Bodi ya Korosho.
Awali, hati ya nyumba hiyo ilikuwa ya
Taasisi ya Kilimo Tanzania ambayo ilifutwa mwaka 1963, kabla ya mtu
mwingine kuibadilisha hati na kuiuza kwa Koka mwaka 2011.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mudhihir Mudhihir alisema Koka aliuziwa nyumba na taasisi hiyo ambayo haikuwa mmiliki halali.
Alisema nyumba hiyo iliuzwa kwa Sh300
milioni na katika juhudi za bodi kufuatilia taratibu za kuirudisha,
ikagundulika kuwa hati imeshabadilishwa, kusisitiza kuwa uuzwaji wa
nyumba hiyo ulifanyika kimakosa bila kufuata sheria na taratibu.
Juzi Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi
Ombeni Sefue alikaririwa akiwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu
makusudio ya kuuza nyumba za Serikali na mashirika ya umma, kutokana na
madeni mbalimbali ili ziweze kukombolewa kabla ya kuuzwa.