KILIMANJARO wauguzi
wa zamu katika kituo cha Afya cha Pasua kilichopo Manispaa ya Moshi, wanatuhumiwa
kumtolea lugha chafu mama mjamzito ikiwamo pia kumnyima kitanda na hivyo
kujifungulia nje ya baraza la nyumba ya jirani muda mfupi baada ya kufukuzwa kituoni hapo.
Mama huyo Josephine Michael (21), Mkazi wa kata ya Kaloleni, Manispa ya Moshi mkoani Kilimanjaro alikumbwa na mkasa huo Novemba
29 mwaka huu, baada ya kufika kwenye kituo hicho kwa ajili ya kupatiwa msaada wa
kujifungua lakini katika hali isiyokuwa ya kiutu aliambulia kufukuzwa na
wauguzi hao wa zamu.
Akizungumza na mwanaharakati , Mama huyo amesema kuwa, baada
ya kufika katika kituo hicho cha Afya, majira ya saa mbili usiku na
kuwaeleza wauguzi hao wa zamu juu ya kile kilichokuwa kinamsibu, alielezwa
kuwa hakuna kitanda kwa watu ambao si wagonjwa.
Amesema
kuwa baada ya kuambulia majibu hayo, aliondoka na kurejea nyumbani kwake na
alipofika nyumbani hali yake ilibadilika na kuwa mbaya na hivyo kukimbilia kwa
majirani kuomba msaada ambapo kabla ya kupatiwa msaada huo na majirani mfuko wa
uzazi ulipasuka.
Miongoni
mwa waliojitoa mhanga kuokoa uhai wa mama huyo pamoja na mtoto wake ni
mwandishi wa habari, Safina Sarwatt (Mtanzania), ambaye alilazimika kutumia
mwanga wa simu yake ya kiganjani kumzalisha mama huyo akishirikiana na majirani
zake.
Sarwatt
amesema licha ya kutokuwa na utaalamu wowote alijikuta katika wakati mgumu
ingawa aliendelea kutoa msaada huo, na kumkimbiza katika kituo cha afya cha
Pasua.
Akizungumza
Mama huyo akiwa katika kituo cha afya cha Pasua wodi ya watoto amempongeza
mwandishi huyo kwa kuwa na moyo wa kipekee kwani ni watu wachache ambao wanaweza
kujitolea.
Hata hivyo Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Shaaban
Ntarambe hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo kwa kile alichodai suala hilo ni
la kitaalamu na kuwataka waandishi wa habari kuandika maswali ili ayawasilishe
kwa wataalamu wake wa Idara ya Afya.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia