Ikulu
imesema pamoja na kuwa Rais Jakaya Kikwete amekwishapokea maazimio ya
Bunge kuhusu wanaotuhumiwa kuchota Sh306 bilioni katika Akaunti ya
Tegeta Escrow, hawezi kuwachukulia hatua mpaka hapo uchunguzi kuhusu
suala hilo utakapokamilika.
“Rais lazima
aagize vyombo vya uchunguzi kufanya kazi yake na baada ya hapo ndipo
atapata mahali pa kuanzia. Watu wengi walitaka Rais Kikwete achukue
hatua baada ya kupewa maazimio ya Bunge. Jambo hilo haliwezekani,”
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana na kuongeza kuwa
hatua zitachukuliwa kwa watakaobainika kuwa na makosa ya kimaadili au
jinai baada ya uchunguzi.
Alisema
uchunguzi kuhusu uchotwaji wa mabilioni hayo uliofanywa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) pia utazingatiwa na Rais katika kutoa
uamuzi.
“Maazimio ya
Bunge ni mazuri ila inatakiwa muda kwanza ili Rais naye apate taarifa
za uchunguzi zaidi. Maazimio hayo ni muhimu na si ya kupuuzwa hata
kidogo,” alisema.
Alisema vyombo vinavyofanya uchunguzi kuhusu suala hilo ni vile ambavyo vilitajwa kufanya hivyo katika maazimio manane ya Bunge.
Bavicha wamtaka Kikwete achukue hatua
Baraza la
Vijana wa Chadema (Bavicha), limemtaka Rais Kikwete kuacha kuhamisha
wakuu wa mikoa na badala yake atoe uamuzi wa kuwashughulisha watuhumiwa
wote waliohusika na kashfa ya escrow.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Katibu wa Bavicha, Mwita Julius alisema: “Wakati huu
si mzuri wa kuanza kuhamisha wakuu wa mikoa kwa kuwa ni gharama, ni
muda wa kuwachukulia hatua wahusika wote waliotajwa bungeni wakihusika
na sakata la escrow.”
Alisema Rais
anatakiwa kuwashughulikia wateule wake wote waliotajwa bungeni kwani
wananchi wanasubiri kuona mabadiliko hayo kwa haraka.Juzi, Rais Kikwete aliteua mkuu mmoja wa mkoa na kuwahamisha wengine sita.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia