MBUNGE wa
Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, amemshambulia Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Abdurahman Kinana, kuwa ni kiongozi aliyepigwa changa la macho
jimboni hapa kiasi cha kujikuta akiingizwa kwenye udhalilishaji na aibu na
hivyo kuonekana katika jamii kuwa hafai.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa jana, Lema (Chadema), alisema
ziara nyingi za Katibu Mkuu Kinana anazozifanya mikoani zimekuwa ni maigizo na sawa
na wachekeshaji katika vipindi vya runinga.
Akizungumzia ‘changa
la macho’ alilopigwa, Lema alisema katibu mkuu huyo kwa kutojua aliwapokea
wanachama waliofukuzwa Chadema huku akidai bado walikuwa viongozi wa chama
hicho.
“Katika
mikutano ya ukoo wa CCM ambayo chama hicho hufanya kazi ya ziada kusomba watu
kwenye malori kutoka maeneo mbalimbali ili wahudhurie kwa wingi, alikuwa
akionekana Kinana akiwapokea wanachama tuliowafukuza uanachama, wakati huo huo
akidai kuwa wamewapokea viongozi toka Chadema, haya ni maigizo.
“Ukiona Katibu
Mkuu wa CCM anaingia katika udhalilishaji na aibu kama hii maana yake wananchi
wanamuona kuwa hafai,” alisema na kuongeza, “jana (juzi) alienda Soko la
Kilombero akamkuta mtu anafagia, akaanza kuigiza kwa kufagia kwa lengo vyombo
vya habari viweze kumwoshesha.
“Mwenendo wa
Kinana unaonyesha CCM kinafanyakazi kama chama kinachoanza leo…ni mambo
yasiyoeleweka na sio utawala bora kwa yeye kuwatukana mawaziri wa chama chake
hadharani,” alisema.
Alisema Kinana
aliyepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya
vyama vingi 1995, hana kitu ambacho anaweza kujivunia kwamba alileta maendeleo
ya jimbo hili.
Akitoa mifano,
Lema alisema Kinana alimpokea aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Monduli
aliyefukuzwa, Mchungaji Amani Silanga Mollel, kujiunga na CCM huku akidai kuwa alikuwa
bado ni mwenyekiti wa chama hicho.
Alisema ukweli
ni kwamba Silanga alifukuzwa uanachama wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema,
Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari kwa
niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha Novemba 30, 2013.
Aliongeza
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ngorongoro, Revocatus Palapala, naye
alifukuzwa na chama hicho na kuhamia chama cha Alliance for Change and Transparency
(ACT) na baadaye kuhamia CCM na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa wa Kijiji cha
Waso, wilayani humo.
Alisema ni
ajabu kuona kiongozi mkubwa wa chama akimpokea Palapala kama mwanachama mpya wa
CCM aliyeacha wadhifa wa mwenyekiti wa Chadema, wakati ukweli unaonyesha
alikuwa ni mwanachama wa CCM.
Aidha alisema
aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chadema, Kata ya Olorien, Godfrey Mfinanga, naye
pia alifukuzwa wakati wa uchaguzi wa marudio wa kata nne zilizopo katika jimbo
la Arusha Mjini, baada ya kubainika kwamba alikuwa akifanya kazi ya kukisaidia CCM
na Cuf katika uchauguzi huo uliofanyika Oktoba 2013.
Lakini alisema
alipopokelewa na CCM katika ziara ya Kinana, alitajwa kama mtu aliyetoka
Chadema.
Akizungumzia
zaidi ziara za Kinana mikoani, Lema alisema mara nyingi amekuwa akiwadhalilisha
hadharani mawaziri wa serikali yake pamoja na watendaji wengine huku akijua
kwamba anayo fursa ya kuonana na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, na
kuyashughulikia masuala hayo kichama na kiserikali.
“Huu ni mwenendo
wa Kinana wa maigizo anaoendelea nao nchi nzima, maigizo hayo yameingia Arusha,
kitendo chake cha kwenda kwenye mikutano ya hadhara na kuanza kuchambua
mienendo ya mawaziri walioteuliwa na mwenyekiti wake kinaonyesha uwezo wake
ulivyo…Kinana ni katibu mkuu wa chama, ni mtu mkubwa sana ana fursa zote za kuonana
na mwenyekiti wake na hata kuwaita mawaziri katika vikao vya faragha,” alisema.
Akizungumzia
madai ya kujimilikisha kiwanja ambacho marehemu Nyage Mawalla, alikitoa kwa
ajili ya chama hicho ili kijenge hospitali ya wanawake na watoto, Lema alisema,
madai hayo sio ya kweli na upotoshaji.
Alisema kiwanja
hicho hajajimilikisha, na utaratibu unaendelea ndani ya chama na wanatarajia
kuanza ujenzi kabla ya bunge hili kumaliza muda wake.
“Tumepata
wafadhili wa kujenga na makadirio ya awali ya gharama za ujenzi ni dola za
Marekani milioni 3.8,” alisema na kuongeza, watajenga pia chuo cha uuguzi.
Kuhusu ujenzi
wa Soko la Kilombero, alisema litaboreshwa na kuwa la ghorofa tano hadi nane liwe
la kisasa litakaloweza kutosheleza hata wafanyabiashara wa Soko Kuu.
Alisema
wamepata kiwanja eneo jirani na Soko la Kilombero hali ambayo itawawezesha sasa
kuliboresha soko hilo liwe la kisasa kwa gharama za Sh. Bilioni 25.
“Kinana
anakwenda kufanya upotoshaji kwa kudai kuwa sisi tulisema tutavunja soko hilo.
Tunataka kuboresha ili wafanyabiashara waweze kufanya shughuli zao katika
mazingira bora,” alisema.