VIKUNDI VYA ULINZI SHIRIKISHI VYATAKIWA KUFANYA KAZI BILA KUBUGUZI WANANCHI


Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha MrakibuwaPolisi (SP) Jumanne Muliro amevitaka vikundi vya ulinzi shirikishi pindi wanapokuwa katika kazi za doria kutowabughudhi wananchi badala yake wanatakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata sheria.
Alisema utendaji bora wa kazi kwa kuzingatia nidhamu na sheria utaongeza imani kwa wananchi hali ambayo itawafanya wajitolee na kuendelea kuvichangia vikundi hivyo hatimaye kuboresha maslahi yao wenyewe na vikundi hivyo kwa ujumla kwa maana ya vifaa.
 “Hakuna sheria inayomkataza mtu yoyote kutembea usiku lakini pia ni jukumu lenu nyinyi askari kumhoji yeyote mtakayekutana naye usiku kwa kutumia taaluma mlionayo nayo ili kuweza kubaini ukweli” Alifafanua Mkuu huyo wa Polisi.
Hayo aliyasema wakati wa Uzinduzi wa vikundi viwili vya Ulinzi Shirikishi uliofanyika juzi katika kata ya Moshono ambapo jumla ya askari 50 wa vikundi hivyo walihudhuria. Alisema ili kazi zao ziende vizuri na kuendelea kujenga imani kwa wananchi wanatakiwa wanapoingia kazini wasiwe wamelewa hali ambayo itaendelea kuleta uelewa na masikilizano baina ya wanaohoji na wanaohojiwa na kuepusha matukio ya kutojichukulia sheria mkononi.
Aliongeza kwa kusema, kuwepo na kuongezeka kwa vikundi hivyo kutasaidia kuimarisha ulinzi katika wilaya ya Arusha na kutumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi pamoja na askari wa vikundi hivyo na pia kutoa wito kwa maeneo mengine kuiga mfano huo.
“Usalama wa eneo lolote usitegemee askari toka Kituo kikuu cha Polisi ila kila mtaa unatakiwa uwe na vikundi hivyo kwani eneo lolote ambalo halina ulinzi linatoa mwanya kwa wahalifu”.Alisema Mkuu huyo wa Polisi.
Alimalizia kwa kuwataka askari wa vikundi hivyo kuratibu maeneo korofi ili Jeshi la Polisi wilayani hapa liweze kuongeza nguvu katika operesheni hizo ambazo zitasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Moshono Paulo Mattysen alivipongeza vikundi hivyo pamoja na viongozi wao na kuahidi kushirikiana nao.
Awali wakitoa elimu kwa vikundi hivyo hivyo Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Arusha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Maria Maswa pamoja na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi katika Tarafa ya Suye Frimina Massao waliwaeleza wanavikundi hao umuhimu wa ulinzi shirikishi na hali hii inatokana na uchache wa askari wa Jeshi la Polisi na kuwataka wawe na mipaka katika utendaji wao wa kazi.
Wana vikundi hao walitakiwa kuendelea kutoa taarifa za uhalifu hali ambayo itasaidia kuimarisha ushirikiano baina yao na Jeshi la Polisi na kuwasisitiza watumie falsafa ya ukamataji salama.
Uzinduzi huo wa vikundi hivyo vilivyopewa majina ya Sekei Moivaro Polisi Jamii na Mbung’o Moshono kaskazini Polisi Jamii uliambatana na utoaji wa filimbi,tochi na vitambulisho ambavyo vitasaidia katika utendaji wao wa kazi.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post