Balozi wa
Kujitolea wa Harakati za 'Imetosha Movement', Henry Mdimu (kulia)
akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya taasisi ya 'Imetosha Movement' na viongozi
wakizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni
Na Mwandishi Wetu
ASASI ya Harakati za Imetosha ilioanzishwa kupinga mauaji
na vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watu wenye u-albino inatarajiwa
kufanya matembezi makubwa ya hisani kuchangisha fedha kwa ajili ya
kuendelea kutoa elimu kwa uma juu ya imani potofu zinazoendelea za mauaji
ya albino.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa
Kujitolea wa Harakati za 'Imetosha Movement', Henry Mdimu amesema matembezi
ya hisani kuchangia fedha zitakazowezesha kutolewa kwa elimu kwa mikoa ya
Kanda ya Ziwa juu ya imani potofu zinazoendelea na mauaji ya albino
yanatarajia kufanyika Dar es Salaam Machi 28, 2015.
Alisema matembezi hayo yataanzia katika Viwanja vya Leaders na kuzunguka
maeneo yaliyopangwa kisha kurejea viwanjani hapo kwa ajili ya shughuli
maalumu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya harakati maalumu za imetosha
zitakazo kwenda kwa jamii ya kawaida na kueneza elimu ikiwa ni juhudi za
kuhamasisha kila mwana jamii kupaza sauti na kusema 'Imetosha Mauaji ya
Albino'.
"...Baada ya taratibu kukamilika, matembezi sasa yatafanyika Tarehe 28
Machi kuanzia saa 12 Alfajiri, kutoka Leaders Club tutazunguka na kurudi
hapo, karibuni sana tuchangie harakati hizi zenye lengo zuri kwa
mustakabali wa Taifa letu lenye sifa ya amani na utulivu," alisema Mdimu
katika taarifa yake.
Aidha akizungumzia uvumi ulioenea hasa katika nchi za nje, unaodai kwamba
serikali imekataza watu wenye ulemavu wa ngozi kuandaa matembezi au
maandamano alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote na kuongeza kuwa kuna
taratibu za kufuata kabla ya uandaliwa shughuli hizo.
"...Hili suala sio kweli, ili ufanye mambo kama haya ni lazima upitie
taratibu za kisheria ili upate kibali. Hii ni nchi na ina taratibu zake kwa
hiyo tulipaswa kuzifuata na ndio kilichosababisha hata matembezi yetu
kuahirishwa.
"Tulikuwa tunafuata taratibu na leo rasmi tumepata usajili wa
Imetosha...sasa imetosha imekuwa taasisi kamili inayoitwa IMETOSHA
MOVEMENT. Napenda kuchukua wasaa huu kuwashukuru marafiki wote wanaoniunga
mkono, na kunipa moyo, msinichoke kwa sababu safari bado ni ndefu,"
Hata hivyo aliwataka wananchi na wadau mbalimbali yakiwemo makampuni
kujitokeza katika matembezi hayo ya hisani ili kuunga mkono juhudi sa
mapambano ya kukomesha mauaji na vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa
watu wenye ualbino maeneo mbalimbali ya nchi.