Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe |
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewaaga wapigakura wake
kuwa hatakuwa tena mbunge wao, akisema kuwa kesi ya dhidi ya Chadema
ilitupwa na Mahakama Kuu kutokana na baadhi ya majaji kutajwa kwenye
kashfa ya escrow.
Chadema ilimvua Zitto uanachama saa chache baada
ya Mahakama Kuu kutupa shauri lake alilofungua akitaka chombo hicho cha
sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa nyaraka za mwenendo
wa vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote, huku akifanikiwa
kupata amri ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika
Kata ya Mwandiga mkoani Kigoma jana, Zitto alisema hatakuwa mbunge wa
jimbo hilo baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, na akatumia fursa
hiyo kueleza safari yake ya kisiasa ndani ya Chadema na mtazamo wake
baada ya kufukuzwa uanachama.
“Nimejifunza mengi nikiwa mbunge. Katika utumishi
wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi yetu inavyoendeshwa. Katika
kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya kujivunia na mengine ni
makosa,” alisema Zitto ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa Chadema.
“Nimejifunza kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu
na kuwatumikia watu wa nchi hii. Ndiyo maana hamkunisikia tu nikitetea
watu wa Kigoma pekee, bali watu maeneo mengine ya nchi yetu na makundi
mbalimbali ya kijamii.”
Alisema safari yake ya ubunge ilikuwa ngumu yenye mafunzo makubwa na imemfanya apevuke kifikra na kupata mafunzo.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Zitto
alisema: “Bado nina nia ya dhati ya kuendelea kuwatumika Watanzania kama
mwakilishi wao kupitia jimbo lolote nchini.
Nitaendelea kuwapo kwa uwezo wa Mungu katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. Itakuwa kwa tiketi gani na jukwaa gani watu
watayajua hayo wiki hii.”
Akizungumzia sakata la escrow lililowahusisha
watendaji mbalimbali wa Serikali, wakiwamo majaji na hukumu ya kesi
yake, Zitto alirudia tena kauli yake kuwa hukumu hiyo imetolewa bila
yeye kujua. “Kwa kazi ninazozifanya kuna miguu ya watu wengi
ninayoikanyaga.
Moja ya ninaowakanyaga ni mahakama. Kuna majaji
ambao taarifa ya kamati ya PAC imewataja kuhusika na escrow na
wanatakiwa kuchunguzwa,” alisema.
Alisema inawezekana ndani ya mahakama wameona hukumu ya kesi hiyo ndiyo eneo zuri la kumkomoa.
“Inawezekana pia watu ambao kupitia kazi za PAC,
nimesababisha wachukuliwe hatua nao pia wanaweza kuwa wameshiriki kwa
njia moja au nyingine. Lakini pia inawezekana ni taratibu za kawaida za
mahakama. Mpaka hukumu inatolewa kuna maswali mengi hayana majibu,”
alisema.
cHANZO:MWANANCHI
cHANZO:MWANANCHI
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia