Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mh. Alexandre
Lévêque akimkabidhi tuzo ya kwanza Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Wanahabari Wanawake Tanzania-TAMWA,Bi. Valerie Msoka kwa kufanikisha
kampeni dhidi ya ndoa za utotoni.(Picha zote kwa hisani ya mtandao wa hivisasa.co.tz).
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania
(TAMWA) Valerie Msoka, amekuwa mtu wa kwanza kutunukiwa tuzo ya CEFM
Champion, na Ubalozi wa Canada nchini.
Katika
sherehe fupi iliyofanyika Serena Hotel 24 Februari 2015, Balozi wa Canada
nchini Bwana Alexandre Leveque alisema kuwa Valerie Msoka amekuwa
mwanaharakati wa kwanza kutunikiwa tuzo hiyo na ubalozi wake kama ishara ya
kukubali mchango wake kupiga vita ndoa za utotoni, za kulazimishwa na
ukeketaji kwa watoto wa kike nchini.
"Watoto wa kike na wanawake wamevumilia machungu ya ndoa
za utotoni na za kulazimishwa hivyo wanahitaji mtu wa kuwasemea: mtu ambae
ataelezea taarifa zao zinakazosaidia kuwaweka watu pamoja na kuleta
mabadiliko yenye tija,"amesema Balozi Lévêque. Valerie Msoka atakuwa
mtetezi. Ninafuraha kumtangaza kuwa Mtetezi wa CEFM wa Ubalozi wa Canada
nchini Tanzania."
Valerie ametumia ujuzi wake kama mwanahabari aliyebobea,
mwanaharakati na mpenda maendeleo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali bila
kujali litakalomtokea au kueleweka vibaya na jamii.
Ameandika taarifa zenye kuvuta hisia, huruma na
kuhamasisha kasi ya mabadiliko Katika jamii na watunga sera," alisema
Balozi Leveque.
Wapili kutoka kushoto ni Balozi wa Canada nchini
Tanzania Alexandre Lévêque , Mkurugenzi mtendaji wa TAMWA Valerie Msoka,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna Maembe
na wawakilishi mbalimbali kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa wa masuala
ya wanawake, UNFPA na UN Women.
Watoto
wa kike milioni 14 duniani huozeshwa kila siku katika umri mdogo chini ya
18 jambo ambalo ni kinyume cha haki za mtoto na ukiukwaji wa haki za
binadamu. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ndoa za utotoni na
mikoa husika ni Shinyanga, Tabora, Mara, Lindi, Mbeya na
Morogoro.
Balozi
Leveque ameahidi kuunga mkono jitihada zinazomlinda mtoto wa kike ili
kuendeleza kampeni ya Zero Marriage kwa mkoa wa Mara iliyozindiliwa mwaka
2014 na aliyekuwa mke wa Hayati Rais wa Kizalendo wa Afrika ya Kusini
Nelson Mandela, Graca Machel.
Akitoa
shukrani baada ya kupokea tuzo hiyo, Valerie Msoka alisema kuwa ndoa za
utotoni za kulazimishwa na ukeketaji vyote vinaenda pamoja na ni wajibu wa
wadau mbalimbali ikiwemo serikali na vyombo vya habari kuendeleza kutoa
elimu, kufanya tafiti ili kuwa na rekodi inayofahamika kuhusu ukubwa wa
tatizo, kufuatilia mwenendo na mafanikio ya kampeni mbalimbali na
kuendeleza hamasa kwa jamii kwa nini ndoa za utotoni
zikomeshwe.
"Tukitaka kufanikisha kampeni hii ni lazima tufanye kazi
kwa pamoja na kwa moyo mmoja, kuelewa nani anafanya nini kwa kiwango gani.
Serikali nayo bado tunaitegemea sana kwa hali na mali katika kubadilisha
sera zinazomkandamiza mtoto wa kike kwa kuzingatia mabadiliko ya katiba
mpya", alisema Valerie.
Wadau mbambali wa masula ya wanawake na waandishi wa
habari wakongwe (Ma-Veterans), kutoka kushoto ni Fatuma Aloo pamoja na Mama
Rose Haji Mwalimu wakihsuhudia tukio hilo.
"Tuzo
hii ni yetu wote, kama sio kwa ushirikiano wenu wadau wa maendeleo, vyombo
vya habari ambavyo tumefanya kazi kwa karibu sana na jamii kwa ujumla. Ni
matumaini yangu kuwa tutaendelea kushikamana kuhakikisha kuwa hadhi ya
mtoto wa kike inalindwa ipasavyo".
Hii ni
mara ya pili kwa kiongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA)
kupata tuzo ya kutambulika. Mwaka 2010 Ubalozi wa Marekani ulimtunuku
Mkurugenzi aliyemaliza muda wake Ananilea Nkya tuzo ya Mwanamke Jasiri
kutokana na mchango wake wa kuendeleza usawa, fursa na haki kwa wanawake wa
wasichana wa Kitanzania.
Akitoa
nasaha zake kwa niaba ya serikali, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Watoto na Jinsia Bi Anna Maembe amempongeza Msoka kwa kazi nzuri na
chama anachokiendesha kwa ujumla na kusema kwamba tuzo hii imetolewa wakati
ambapo dunia na taifa kwa ujumla linatafakari matokeo ya Beijing +20 ambako
Katika maazimio 20 yaliyoainishwa, Tanzania ilipendekeza kulifanyia kazi
azimio moja ambalo ni la kumlinda mtoto wa kike.
Maembe
amesema tuzo hii itatoa hamasa kwa wengine na itakuwa kielelezo cha
serikali Katika jitihada za kutekeleza tamko la CEDAW linalolenga kumlinda
mwanamke na mtoto wa kike.
Mmoja wa wafanyakazi wa Chama cha wanahabari wanawake
Tanzania TAMWA akiwakilisha zawadi ya ua kwa Mkurugenzi wao Valerie Msoka
baada ya kukabidhiwa tunzo ya umahiri na utambuzi wa kupinga ndoa za
utotoni na Ukeketaji nchini Tanzania kutoka nchini
Canada.
Amesema serikali itaendeleza jitihada hizo kwa
kuhakikisha watoto wa kike hawaolewi katika umri mdogo kwa kulazimishwa kwa
kujenga mazingira mazuri shuleni yatakayovutia watoto wa kike kubaki
mashuleni, kuongeza hamasa za uelewa wa tatizo na kuhakikisha wale wote
wanaohusika na kuwalazimisha watoto wa kike kuolewa Katika umri mdogo
wanachukuliwa hatua za kisheria. Lakini pia kuharakisha kubadilisha sharia
ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo haimlindi mtoto wa kike chini ya umri wa miaka
18 kuolewa.
"Watoto 2 kati ya 5 hujikuta wako Katika mazingira ya
kuozeshwa kwa nguvu kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kutokuwa na
elimu ya kutosha, maisha duni vijijini, umaskini na mila na desturi potofu
zinazoendelezwa na baadhi ya makabila na mahari", amesema
Maembe.
Tafiti
zinaonyesha kwamba asilimia 39 ya watoto wa kike wenye elimu ya msingi
wameolewa katika umri usiotarajiwa chini ya miaka 18 wakati wale wenye
elimu ya kutosha wa mjini wameolewa baada ya kufikisha miaka
18.
Mkurugenzi wa mtendaji wa TAMWA akiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Chama hicho.
Ndoa
za utotoni ni pale mtoto wa kike anapoozeshwa kwa lazima akiwa katika umri
chini ya miaka 18 na wakati mwingine yuko shuleni. Madhara yake ni makubwa
kwa afya ya mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na kupoteza uhai wake na mtoto
mwenzake, kukosa maendeleo kimaisha na kuendeleza utamaduni wa kuwa
tegemezi na kudumaza fikra na kumfanya kuwa duni Katika
taifa.
Katiba
ya nchi inamlinda mtoto wa kike kwa kutambua kwamba mtoto ni yule ambaye
huko chini ya miaka 18 na hana sifa za kupiga kura. Lakini wakati huo huo
Sheria ya Ndoa 1971 inasema mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 16 anaweza
kuoa na msichana mwenye miaka 14 anaweza kuolewa kwa ridhaa ya
wazazi.
Sheria
hizi mbili zinakinzana na hivyo hazimlindi mtoto wa kike moja kwa moja.
"Tutahakikisha kwamba sheria ya ndoa inafanyiwa marekebisho ili iende
pamoja na Katiba ya nchi, jitihada zinaendelea kwa kuungana na wanaharakati
wote nchini kuleta mabadiliko hasa baada ya kuzindua kampeni ya "Ukanda
Huru wa Ndoa za Utotoni" (Child Marriage Free Zone) na Graca
Machel.
Tuzo
ya CEFM Champion ilishuhudiwa na wadau mbalimbali kutoka serikalini na
mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa kuchangia maendeleo, Umoja wa
Kimataifa, waandishi wa habari na wanajamii.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia