Balozi wa kujitolea wa kampeni ya mapambano
dhidi ya mauaji ya albino, Henry Mdimu (wa pili kulia) akizungumza na
vyombo vya jhabari. Kampeni hiyo inajulikana kwa jina la Imetosha. Mchoraji maarufu na mmoja wa wanakamati wa
kampeni za imetosha Masoud Kipanya (kulia) akizungumza na DW Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN),
Joachim Mushi (kushoto) akihojiwa na DW mara baada ya mkutano wao. TBN
imeunga mkono kampeni hizo zinazoongozwa na balozi wa kujitolea wa
mapambano hayo, Henry Mdimu. Baadhi ya wajumbe wa kampeni za imetosha
wakipata picha za ukumbusho mara baada ya kuzungumza na
wanahabari Mkutano na wanahabari ukiendelea
Na Mwandishi Wetu
MMOJA wa watu wenye ulemavu wa ngozi, albino na
mwanahabari shupavu kutoka kampuni ya Mwananchi Communication, Henry Mdimu
amejitolea kuwa balozi wa hiyari kupinga mauaji ya kikatili ya watu wenye
albino yanaoendelea nchini.
Bw. Mdimu ambaye ameungwa mkono na baadhi ya marafiki na watu wanaokerwa na
vitendo hivyo, ikiwemo Chama cha Bloggers nchini, Tanzania Bloggers Network
(TBN) amesema ameamua kufanya hivyo baada ya kushuhudia ndugu zake
wakiteseka kwa muda mrefu dhidi ya mauaji hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Balozi Mdimu
amesema lengo lake kuu ni kuhakikisha anazunguka pamoja na marafiki watakao
muunga mkono na kutoa elimu kwa kuanzia Kanda ya Ziwa ili tatizo hilo
lisiendelee kuenea nchi nzima.
Akifafanua zaidi alisema mauaji ya watu wenye albino yanaichafua Tanzania
hivyo atahakikisha anaisaidia Serikali kupambana na watu wenye imani hizo
za kipuuzi ili kuondoa doa linaloichafua nchi yetu ambayo imekuwa na sifa
ya amani dunia nzima.
"...Nimeamua kufanya hivi baada ya kushuhudia ndugu zangu wakiteseka kwa
muda mrefu. Awali nilishindwa kuanzisha harakati hizi nikiamini kuna vyombo
vinavyohusika na utetezi wa watu wenye ulemavu wa ngozi."
"...Hivyo nimeamua niweke jitihada zangu binafsi niisaidie Serikali yangu
katika kuondoa doa hili linaloichafua Nchi yetu yenye sifa ya Amani duninia
nzima. Hivyo nawaomba Watanzania wenzangu mniunge mkono tukishirikiana na
Serikali ili mauaji haya yakome," alisema Mdimu.
"Kutokana na ushawishi nilionao kama Mwandishi, Mtangazaji wa redio na
Blogger naamini nitaleta mabadiliko makubwa katika kuhakikisha haki ya
kusihi kwa ndugu zangu inaheshimiwa na kubaki historia. Salamu zangu
ziwafikie wanyanyasaji, wauaji na wenye kufanya dhihaka kwa watu wenye
ulemavu wa ngozi kuwa IMETOSHA."
Akifafanua zaidi alisema kwa uchunguzi wake wa awali umebaini ukosefu wa
elimu juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi ndio chanzo cha tatizo hilo kukua
na hatimaye kuuana kwa imani za kishirikina. "...Hivyo basi, silaha ya
Elimu ni sehemu kubwa ya haraki hizi," alisisitiza Balozi huyo wa kujitolea.
Aidha alisema kuendesha harakati hizo alizozipa jina la 'IMETOSHA' elimu
itatolewa kwa njia ya sanaa, na washauri nasaha pamoja na kundi la
wanamuziki ambao pia wataandaa nyimbo mbalimbali za kutoa mafunzo ya
kutokomeza ukatili huu.
Alisema wasanii ambao hadi sasa wamejitokeza kuunga mkono kampeni hizo ni
paoma na Jhikoman, Kassim Mganga, Profesa J, Ray C, Fid Q, Roma Mkatoliki
na Dami Msimamo.
Hata hivyo alisema bado pia anaamini nguvu ya vyombo vya habari ikiungana
na kampeni hizo wanaweza kufanikiwa zaidi hivyo kuomba ushirikiano katika
kuhakikisha vinapaza sauti kutokomeza mauaji hayo ya kikatili.
**Imeandaliwa na www.thehabari.com *
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia