Makamu wa Rais,Dk Mohammed Billal amesema ya kwamba matatizo
ya rushwa na ufisadi katika baadhi ya nchi barani Afrika
yamechangia
kudumaza uchumi na hata kuwatisha wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali
ya nje kuwekeza barani Afrika na kutoa wito kwa wakuu wa nchi hizo
kupiga vita changamoto hizo.
Billal,alitoa kauli hiyo wakati akifunga kongamano la
tatu la viongozi vijana barani Afrika ambapo zaidi ya vijana 400 kutoka Afrika
na China walishiriki kongamano hilo mkoani hapa.
Akifunga kongamano hilo makamu huyo wa Rais alisema kwamba
baadhi ya nchi za Afrika zimeshindwa kupiga hatua kiuchumi kutokana na vikwazo
vya rushwa na ufisadi.
“Rushwa na ufisadi bado ni tatizo kubwa barani Afrika kwani
baadhi ya nchi uchumi wake umeshindwa kukua kutokana na changamoto hii”alisema
Bilal
Hatahivyo,alisema kuwa mbali na rushwa pia matatizo ya
uongozi dhaifu,utawala wa kimabavu,ukabili sanjari na kuminywa kwa demokrasia
kumechangia baadhi ya wawekezaji kutoka mataifa ya nje kushindwa kuwekeza
Afrika.
Awali akitoa shukrani zake kwa wajumbe mbalimbali katika
mkutano huo,mwenyekiti wa Uvccm mkoani Arusha,Robinson Meitinyiku alisema kuwa
ni muda wa bara la Afrika kwa pamoja kupinga ukandamizaji unaofanywa na mahakama ya
kimataifa ya kesi za jinai (ICC).
Alisema kuwa kitendo
cha wakuu wa nchi Afrika kupitia mkutano wao
uliofanyika nchini Ethiopia hivi karibuni kupinga udhalilishaji wa
mahakama hiyo kwa viongozi waliopo barani Afrika ni kitendo cha kijasiri na kinapaswa kuungwa mkono
na bara zima la Afrika.
“Kazi iliyofanywa na viongozi wetu wa Afrika kupitia mkutano
wao ilikuwa nzuri kwa kuwa kwa pamoja walipaza sauti kupinga ukandamizaji wa
mahakama hii ya ICC”alisema mwenyekiti huyo na kuibua shangwe kwa wajumbe wa
mkutano huo
Naye,katibu mkuu wa chama cha Kikomunisti cha China,Zhou
Changkui akitoa shukrani zake alisema kuwa China itaendelea kushirikiana bega
kwa bega na Tanzania katika kuhakikisha
wanawasaidia vijana mbalimbali walipo katika nchi hizo mbili hususani
katika sekta ya ajira.