Diamond Platnumz
Na Mwandishi Wetu
MKOA wa Kigoma ni hazina kubwa ya vipaji hapa
nchini Tanzania. Tangu zamani kulishuhudiwa vipaji vingi toka mkoani humo hasa
vya wanamichezo na wasanii. Mfano kwa upande wa kandanda tutaona kwamba mkoa
huo ulitingisha kwa vipaji vya wanasoka.
Kina Manara, Kitwana Manara,
Sunday Manara, Kassim Manara na ndugu zao wengine wanatoka Kigoma. Baadaye kikafuatia
kizazi cha kina Edbily Lunyamilla, Nteze John, Omari Mavumbi, Itutu Kigi na
wengineo wengi.
Kwa upande wa wasanii wa
muziki Kigoma imetoa watu wengi wenye majina makubwa katika sanaa hiyo, kama Shem Karenga, Hassan Rehan Bitchuka,
Marijani Rajabu, Zahir Ally Zorro, Banana Zorro, Wema Abdallah, Nyota Waziri na
wengineo wengi.
Kwa upande wa muziki wa kizazi
kipya Kigoma imetoa vijana wengi wa muziki huo wakiongozwa na mtaalamu wa
muziki, kwa maana ya kutunga, kuimba, kucheza kila ala ya muziki na kutengeneza
muziki, Emmanuel Bizimana Ntavyo ‘Bizman’. Wapo wengine kama Ally Kiba, Banana
Zorro, Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lynn’ na wengineo.
Lakini pamoja na wote hao
makala hii ni mahususi kwa moja ya vipaji hivyo vya mkoa wa Kigoma ikiwa
imemlenga chiriku wa muziki wa kizazi kipya kwa sasa hapa nchini, Nassibu Abdul
‘Diamond Platnumz’.
Diamond kadhihirisha kipaji
cha sanaa ya muziki kutokana na mafanikio aliyoyapata kwa muda mfupi alioutumia
katika sanaa. Hiyo ni tofauti na kipindi alichokitumia mfalme wa muzuki wa POP duniani,
Michael Jackson, kuwa kileleni mwa mafanikio kwa zaidi ya miaka 10 kati ya 1967
– 1979.
Lakini ndani ya miaka mitatu
Diamond ameweza kuibeba Tanzania na kuiweka kwenye chati ya kimataifa kwenye
fani hiyo ya muziki wa kizazi kipya. Na ninaposema ngazi ya kimataifa sina
maana ya kuvuka tu mipaka ya nchi na kuingia nchi za jirani kama Kenya, Uganda,
Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Msumbiji wala Kongo, kama ambavyo wameweza
kufanya wasanii wengine wa muziki huo wa hapa nchini, ninamaanisha kimataifa
kwa maana halisi. Nalenga nchi za mbali na Tanzania.
Muziki wa Diamond kwa sasa
unapigwa kwenye nchi mbalimbali za Afrika, ukiondoa nchi za Kiarabu kwa upande
wa Afrika Kaskazini, ambako sina uhakika kama muziki wa kizazi kipya una
mashabiki kulingana na utamaduni wa huko.
Kwa maana hiyo Diamond kaiweka
Tanzania kwenye chati ya kimataifa kwa maana halisi kimuziki. Kwa sasa msanii huyo anakula sahani moja na
wasanii wa kimataifa kama kina Peter Okoye na Paul Okoye, Wanigeria wanaounda kikundi
cha P Square, ambao mara kadhaa wamemuomba watoe naye vibao vya pamoja. Pia
yuko kwenye kiwango cha wanamuziki kama Youssou N’Ndour wa Senegal na wengine
wa aina hiyo.
Kwa eneo hili la Afrika
Mashariki, nashindwa kumtofautisha Diamond na Joseph Mayanja ‘Chameleone’. Kwa
sasa wanamuziki hao wanafanana.
Tanzania iliwahi kuvuma sana
duniani miaka ya nyuma kupitia kwa wanamichezo, hususan wanariadha, kina
Filbert Bayi, aliyewahi kuwa bingwa wa mbio za mita 1500 duniani, ambaye mpaka
sasa anashikilia rekodi ya mbio hizo kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola
aliyoiweka mjini Christchurch nchini New Zealand mwaka 1974. Wengine ni Seleman
Nyambui, Adventina Mtakyawa, Juma Ikangaa, Gidmas Shahanga na wengine wengi.
Lakini kutokana na umri
kuwatupa mkono nyota hao, jina la
Tanzania limefifia katika tasinia ya michezo na kuifanya nchi yetu isahaulike
kabisa kana kwamba haipo kwenye nyanja ya michezo na burudani!
Hivyo Diamond ni kijana
aliyedhamiria kulipandisha tena jina la nchi yake kupitia tasnia ya burudani.
Na niseme kwa uhakika kabisa kwamba ameweza. Hilo linashadidiwa na tuzo
mbalimbali za kimataifa anazozipata kwa sasa kwa upande huo wa burudani baada
ya kushindanishwa na wasanii wengine wa kimataifa toka nchi mbalimbali.
Kitu cha kipekee nilichokigundua
kwa Diamond na kuhisi kwamba pengine ndicho kinachochochea mafanikio yake ni
tabia yake ya kusikiliza ushauri na kuufanyia kazi.
Wakati fulani nilimpa
changamoto, ambayo vilevile niliwahi kuitoa kwa Chameleone nilipokutana naye
Jijini Mwanza, Mei mwaka jana, kwamba kwa kiwango alichopo hapaswi kuendelea
kuimba muziki kwa kutumia mtindo wa “Play back”, kwamba anatakiwa kuwa na vyombo vyake na
kupiga muziki live. Diamond kanielewa na kusema kwamba hilo analifanyia kazi
kwa bidii kubwa.
Kingine ni namna anavyoendesha
mahusiano na jamii aliyomo. Kawaida kuna dhana ya kwamba wasanii ni watu
wasioeleweka vizuri ndani ya jamii, wahuni na huo kuwa mwanzo wa neno usanii,
kwamba fulani kanifanyia usanii ikiwa na maana ya kanifanyia uhuni.
Lakini hilo ni tofauti kwa Diamond. Yeye anapenda kuwasaidia wenye
mahitaji kulingana na hali halisi ilivyo. Kipindi fulani kwa mfano, kwa
kuuthamini mchango wa Baba wa Muziki hapa nchini, Marehemu Muhidini Maalim
Gurumo, aliamua kumpatia gari jipya. Huo ni usanii kwa upande wa pili
anaouonyesha Diamond tofauti na upande uliozoeleka kwa jamii.
Diamond anasema kwamba
amejipangia kila mwezi kuwa anatembelea vituo vya watoto yatima na kutoa
misaada mbalimbali kadri inavyowezekana. Huo ni mchango mwingine katika jamii
anaoufanya kijana huyo.
Anawashauri vijana wenzake,
hasa wasanii, wanaojiingiza kwenye ulevi uliopindukia pamoja na matumizi ya
dawa za kulevya waache mambo hayo mara moja. Anasema kwamba yanaharibu vipaji
na wakati mwingine kupoteza maisha. Anasema ili kulinda kipaji chake yeye
anahakikisha anaepukana na mambo hayo yasiyo na maana na yaliyo hatari kwa
maisha ya binadamu.
Diamond anasema kwamba
alizaliwa Septemba 22, 1990, Kigoma.
Anasema kwamba kilichomfanya
aingie kwenye muziki ni kipaji chake kilichojitokeza tangu akiwa shule ya
msingi. alikuwa akiimba kwenye kwaya ya shule na burudani nyingine za shuleni.
Huyo ndiye Diamond Platnumz,
ambaye wasanii wengine vijana wanapaswa wamtumie kama kipimo ya mafanikio
katika muziki wa kizazi kipya wanaoufanya. Bila shaka watakaofuata mwenendo
wake watafanikiwa kama yeye alivyo.