Hospitali ya mkoa wa Arusha,Mt Meru inakabiliwa na upungufu
mkubwa wa mashuka ya kujifunikia kwa ajili ya wagonjwa mbalimbali waliolazwa hospitalini
hapo hali ambayo imepelekea baadhi ya wagonjwa hao kulala bila
kujifunika nyakati za usiku.
Kwa sasa hospitali hiyo ina jumla ya vitanda 500 na mashuka
300 wakati wastani wa kitanda kimoja kinatakiwa kuwa na mashuka 8.
Akizungumza na waaandishi wa habari mara baada ya kupokea
msaada wa jumla ya mashuka 100 na katoni kumi za maji kwa ajili ya wagonjwa
waliolazwa hospitalini hapo,muuguzi mfawidhi wa hospitali hiyo,Sifael Masawe
alisema kuwa tatizo la uhaba wa fedha kutoka serikali kuu limechangia kukosekana
kwa huduma mbalimbali hospitalini hapo yakiwemo mashuka.
Alisema kuwa kwa
nyakati tofauti baadhi ya wagonjwa hushindwa kujifunika mashuka nyakati za
usiku kutokana na uhaba wa mashuka hayo na
kuwataka wadau mbalimbali mkoani Arusha kujitokeza kuokoa hali hiyo.
Akikabidhi misaada ya mashuka na maji kwa ajili ya wagonjwa
waliolazwa katika wodi wa akina mama hospitalini hapo ,mwenyekiti wa kikundi
cha Upendo Family,Faustine Mwandago alisema kwamba misaada hiyo imegharimu
kiasi cha zaidi ya sh,2 milioni.
Mwandago,alisema kuwa lengo la kukabidhi misaada hiyo ni
kuonyesha upendo kwa watu wenye mahitaji mbalimbali sanjari na kulienzi jina la kikundi chao kwa vitendo
huku akiwataka wadau wengine kuwaunga mkono.