ASKARI Polisi wa Idara ya Upelelezi
wa Kituo cha Polisi Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara amefukuzwa kazi
kwa kosa la kupiga risasi matairi ya matrekta mawili yaliyokuwa yanakwenda
kulima Wilayani Kiteto mkoani humo.
Uchunguzi wa libeneke umebaini
kuwa askari polisi huyo amefukuzwa kazi kutokana na kupiga risasi matairi ya matrekta
hayo na katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa kati ya madereva na wasaidizi
wao waliokuwa wamepakia.
Uchunguzi huo umebaini kuwa askari polisi huyo
wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (CID) wa kituo cha polisi Mirerani
ametambulika kuwa ni mwenye namba G.2668 D/C Nathanael.
Hata hivyo,Kamanda wa polisi Mkoani
Manyara,Kamishna msaidizi Liberatus Sabas alithibitisha kufukuzwa kazi kwa
askari huyo wa idara ya upelelezi Nathanael ambaye alikuwa askari kwenye kituo
cha polisi Mirerani.
Kwa mujibu wa rafiki wa askari polisi
huyo ambaye jina lake tunalihifadhi Nathanael amefukuzwa kazi kutokana na kitendo
chake cha kupiga risasi matairi ya trekta zilizopita pembeni ya kituo hicho cha
polisi yakienda shambani.
Alisema trekta hizo zilikuwa zinaendeshwa
kutoka eneo la Ngarenairobi wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro zikielekea
wilayani Kiteto mkoani Manyara kwa ajili ya kulima mashamba ya wakulima kwa
kulipwa fedha.
Hata hivyo chanzo chetu cha habari
kimeeleza kwamba baada ya askari huyo Nathanael kupiga risasi matairi ya
matrekta hayo madereva hao waliwasiliana na mmiliki wake ambaye aliwasiliana
mara moja na Mbunge wa jimbo lao.
Inadaiwa mbunge huyo ambaye pia ni
Naibu Waziri wa wizara moja nyeti nchini na pia Waziri mchapakati mwenye
ushawishi mkubwa kwa jamii aliwasiliana na kigogo mmoja mkubwa wa polisi ili
askari huyo achukuliwe hatua.
“Bosi huyo wa polisi alipiga simu
mara moja kwa mmoja wa madereva wa matreka hayo aliyekuwa kituo cha Mirerani na
kumtaka ampe simu askari huyo Nathanael ambaye alizimia baada ya bosi huyo
kujitambulisha kwake,” alisema.
Alisema usiku huo huo wa tukio hilo
askari huyo Nathanael alilazwa mahabusu kwa muda wa siku tatu kwa amri ya mkuu
wa kituo cha polisi Mirerani (OCS) Elisha Saenda na baada ya muda wa siku
kadhaa ndipo akafukuzwa kazi.
Mwaka juzi,askari polisi wa kituo cha
Orkesumet makao makuu ya wilaya hiyo ambaye alikuwa analinda benki ya makabwela
ya NMB Tawi la Orkesumet alifukuzwa kazi baada ya kupiga risasi hewani bila
sababu ya msingi.
Inadaiwa askari polisi huyo alivuta
bangi na kulewa hivyo kuanza kupiga risasi hewani bila sababu yoyote hivyo
kutishia watu waliokuwa karibu na eneo hilo huku akitaka kuonana na Kamanda wa
polisi wa mkoa huo au IGP.