BREAKING NEWS

Friday, March 23, 2012

MKURUGENZI AKIRI KUNAMTANDAO WA KUHUJUMU FEDHA ZA SEREKALI MONDULI

mkurugenzi wa halmashauri ya monduli samwel Mlay  akiwa anajieleza

MKURUGENZI wa halmashauri ya Monduli, Samwel Mlay amefikishwa mbele ya
kamati ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa (LAAC) kama ilivyoagiza
kujibu tuhuma mbalimbali zilizoibuliwa wakati wa ukaguzi wa miradi
mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Kamati hiyo, chini ya mwenyekiti wake Agustino Lyatonga Mrema iliitaka
serikali wilayani humo kumkamata mkurugenzi huyo aliyeko likizo ya
kustaafu pamoja na mweka hazina wake Julius Masheri  ambaye hata hivyo
hakufika licha ya agizo la kufikishwa kwa kamati hiyo kutolewa.

Akijitetea mbele ya kamati hiyo mkurugenzi huyo  alikiri mbele ya
kamati hiyo kuwepo kwa mtandao wa hujuma za mali za halmashauri ambao
pia  mtandao huo umekuwa ukitishia maisha yake.

Alisema mtandao huo unadaiwa kufanya mambo hayo ikiwa ni kumkomesha mkurugenzi
huyo anayedaiwa kujaribu kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya
watumishi wabadhirifu akiwemo mweka hazina aliyefukuzwa kazi,Julius
Masheri.

Akinyesha hali ya masikitiko mbele ya kamati hiyo na viongozi wengine
wa halmashauri za Monduli,Arusha na jiji la Arusha katika kikao
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa
Arusha(AICC),Mlay alisema pia mtandao huo unatumika
kuhujumu mali za halmashauri hizo kwa kutumia jina lake.

Alisema kufuatia hatua alizochukua dhidi ya baadhi ya watumishi
wanaodaiwa kufanya mambo kinyume na sheria na taratibu za kazi,
ameanza kupokea vitisho mbalimbali juu ya maisha yake.

“Hatua nilizoanza kuchukua dhidi ya mweka hazina na afisa usafirishaji
wa halmashauri ya kufukuzwa kazi kutokana na ukiukwaji wa
sheria,nimepokea vitisho vingi na kuanza kuhujumiwa kwa huku baadhi ya
magari na mali za halmashauri zikitumika kwa shughuli binafsi”alisema
Mlay.

Alisema pamoja na vitisho lakini pia wilaya hiyo imekuwa na mtandao
maalum kwa ajili ya kuhujumu mali na fedha za halmashauri ambazo kwa
makusudi zimekuwa zikimtaja kama mhusika mkuu.

“Mheshimiwa mwenyekiti,mtandao huu unajigamba kwamba kama mimi
nimemwaga mboga wao wanamwaga ugali, umekuwa ukigushi nyaraka
mbalimbali zikiwamo za fedha kwa jina langu,hata hivyo nimetoa taarifa
polisi”alisema Mlay.

 Mlay alisema wapo maadui wakubwa wanaozunguka huku wakimpiga vita
kutokana na kusimamia taratibu na sheria huku pia nikitekeleza
maelekezo ya kamati ya bunge yaliyomtaka kuwawajibisha baada ya
kubainika ni kikwazo cha maendeleo.

Alisema miongoni mwa maagizo ya LAAC ni pamoja na kuisafisha idara ya
fedha hususan mweka hazina, Julius Msheri jambo ambalo alikuwa katika
hatua za utekelezaji ambapo alibaini kuwapo kwa mtandao unaopingana na
hatua hizo.

Mkurugenzi huyo alisema miongoni mwa hujuma zilizokuwa zikifanywa ni
pamoja na  baadhi ya magari na mali za halmashauri kutumika wilaya
jirani kwa shughuli
binafsi..

Kuhusu baadhi ya miradi kutekelezwa chini ya kiwango na taarifa za
miradi hiyo kutopatikana wakati wa ukaguzi, Mlay alisema hali hiyo
inatokana na mtandao uliokuwepo ambao unafanya jitihada za makusudi
kumwingiza matatizoni.

Hata hivyo alisema baada ya maoni na maagizo ya kamati katika kipindi
kilichopita, amefanikiwa kuisafisha idara ya fedha kwa kuhamisha
baadhi ya watendaji ingawa baadaye baraza la madiwani liliagiza
afukuzwe kutokana na tuhuma alizokuwa nazo.

Akizungumzia hali hiyo,mwenyekiti wa LAAC, Augustino Mrema
alimuhakikishia mkurugenzi huyo kwamba mtandao anaodai upo utavunjwa
kwa ushirikiano na viongozi wa wilaya na mkoa kwa ujumla.

Mrema alimuahidi mkurugenzi  huyo kwamba atamkutanisha na mkuu wa
wilaya pamoja na kamati ya LAAC ili kupata fursa ya kujieleza zaidi na
hivyo kutafuta suluhisho la kudumu juu ya suala hilo.

Alisema kuwapo kwa hali mbaya ya kiutendaji katika halmashauri ya
Monduli ambapo kumejengeka uhasama na hivyo kutishia maendeleo na
matumizi sahihi ya fedha za serikali,wahisani na wananchi kwa ujumla.

Naye mkuu wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo alipongeza baraza la
madiwani wa halmashauri ya Monduli kwa hatua zilizochukuliwa dhidi ya
baadhi ya watumishi akiwamo mweka hazina,aliyefukuzwa kazi.

Alisema mkoa unatarajia kufanya mabadiliko makubwa katika nyadhifa
mbalimbali ingawa hakuwa tayari kufafanua kwa madai masuala hayo
yameandaliwa.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates