WAKILI maarufu jijini Arusha , Median Mwalle anayeshikiliwa
katika gereza kuu la Kisongo mjini hapa,kwa tuhuma za uhujumu uchumi,amedai maisha yake yako hatarini , kufuatia hatua ya
mawakili wa serikali kumfuata mara kwa mara katika gereza hilo, wakitaka
wamchuke wampeleke kusikojulikana jambo alilodai kuwa na mashaka na usalama wa maisha yake .
Mwale ambaye yupo
rumande kwenye gereza hilo kutokana na kesi inayomkabili kutokuwa na
dhamana, alitoa malalamiko hayo leo mbele ya hakimu mkazi ,
Devotha Msofe aliyekuwa akiahirisha kesi hiyo ya
jinai namba 330/11 kwa niaba ya hakimu mkazi mfawidhi , Charles Magesa
anayesikiliza shauri hilo ambapo upande wa serikali uliwakilishwa na mawakili
Fredrick Manyanda na Neema Ringo .
Akiongea mahakamani hapo, wakili wa Mwale , Loom
Ojare alisema kuwa amelazimika kutoa taarifa hiyo ili kuweka kumbukumbu
mahakamani hapo,kutokana na jambo linalomsibu mteja wake, kwani jambo lolote
linaweza kumpata wakati wowote kutokana na matukio ya kufuatwa gerezani siku
na mawakili hao wakati kesi inayomkabili
ipo mahakamani.
Hata hivyo hakimu Msofe alisema kuwa ni vema
suala hilo akaliwasilisha mbele ya hakimu Magesa anayesikiliza shauri hilo ili
aweze kufanya maamuzi, ambapo alipangia shauri hilo lirudi mahakamani kwa ajili
ya kutajwa machi 28 mwaka huu .
Malalamiko ya wakili huyo yamekuja siku chache
baaada ya mahakama hiyo kuwaagiza Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai nchini (DPP), Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha kurudisha mali za wakili hiyo zilizokuwa
zikishikiliwa na mamlaka ya mapato TRA,yakiwemo magari saba na simu za mkononi
kwa mshtakiwa Mwale, anayetuhumiwa kupatikana na fedha chafu.
Uamuzi wa
kurudishiwa mali zake ulitolewa na
Hakimu Mkazi Mfawidhi Magesa ambaye alisema baada ya kupitia ushahidi wa
pande zote, mahakama yake imeridhika kuwa mamlaka hizo zilikamata magari
hayo kinyume cha sheria ya matunda ya uhalifu (Proceeds Crimes Act) pamoja na
vifungu namba 41 na 44 vya sheria ya mwenendo wa kesi za jinai.
Hukumu ya hakimu Magesa ilisema kuwa Ukamataji huo ulikuwa ni kinyume
cha sheria kutokana na kitendo cha upande wa mashitaka cha kukamata magari
hayo, hivyo mahakama iliamuru kuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini,
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa TRA nchini na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha ambao
walihusika katika zoezi la ukamataji wa mali hizo kuhakikisha wanazirudisha kwa mshitakiwa haraka iwezekenevyo.
Magari
ambayo mahakama hiyo iliamuru kurudishwa nyumbani kwa mshitakiwa ni T 690 BEW
aina ya Range Rover, T 643 BTS Land Rover Discovery, T 907 BTS BMW, T 118 BRS
Cadillac Escalade, T 499 APX Land Cruiser, T 520 BBJ BMW, ambayo yalichukuliwa
Novemba mosi pamoja na gari T 660 BCG Toyota Chaser lililokamatwa Desemba
8, mwaka jana.Kesi hiyo inarajia kutajwa tena machi 28 mwaka huu.
Wakati
huo huo mfanyabiashara maarufu nchini na mkaazi wa jijini Arusha,Salimu Alii
(70)anaendelea kusota katika gereza kuu la ukonga jijini Dar es salaam, baada
kukamatwa na polisi kwa tuhuma za kupatikana na hatia za kuhujumu uchumi
na kufanya biashara ya kuuza binadamu nje ya nchi kinyume cha sheria.
Salimu
Alii anasifika kwa kuasaidia watu mbalimbali jijini Arusha,alikamatwa jijini
hapa ,mwanzoni mwa mwaka huu,na kusafirishwa kwenda jijini Dar es salaamu
alikofunguliwa mashitaka ya kuhumu uchumi kwa kupatikana na fedha chafu na
kusafirisha binadamu.
Kwa mujibu wa sheria
za hapa nchini,kosa la kuhujumu uchumi na biashara ya watu hayana mdhamana.