Zitto Kabwe akiwa anawasili katika viwanja vya shule ya msingi leganga ambapo ndipo chama cha demokrasia na maendeleo chadema walizindulia kampeni
Muhasisi wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema Mzee mrema akiwa anawasili katika viwanja vya Leganga
Freeman Mbowe akiwa anahutubia wananchi waliouthuria mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni katika jimbo la Arumeru mashariki
mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema Freeman Mbowe akiwa anamuombea kura mgombea ubunge wa chama hicho kwa wananchi waliouthuria mkutano huo
Joshua Nassari akiwa anahutubia wanachi waliouthuria uzinduzi huo
Mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema Joshua Nassari akiwa anawatambulisha wazazi wake kwa wafuasi waliouthuria mkutano huo
helikopta ya chadema ikiwa inaingia katika viwanja vya chadema
Zitto kabwe akiwa anawapa mikono wafuasi wa chadema mara baada ya uzinduzi huo kumalizika
kila mmoja alikuwa anahamu ya kuwapa viongozi hao mikono
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kiliuteka mji wa Usa River,
wilayani Meru pale kilipozindua kwa kishindo kampeni za uchaguzi mdogo wa
ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.Shamrashamra za uzinduzi huo
zilianza asubuhi na ilipotimu saa 7.40, helikopta yenye stika ya maneno
CHADEMA, ilianza kuzunguka angani katika jimbo hilo, huku ikisambaza
vipeperushi vinavyomnadi mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari.
Mamia ya wapenzi na wanachama wa chama hicho walifurika katika Uwanja wa
Shule ya Msingi, Leganga, Usa River kuazia saa saba mchana ambako uzinduzi wa
kampeni ulifanyika zikiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbowe na Nassari walifika kwenye Uwanja wa Leganga wakiwa kwenye helikopta
saa 8.45 na kulakiwa na viongozi walioongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
Zitto Kabwe pamoja na wabunge kadhaa wa chama hicho.
Polisi pamoja na walinzi wa kikundi cha usalama cha Chadema, Red Brigade
walipata wakati mgumu kuwadhibiti wafuasi waliokuwa wakitaka kusalimiana na
viongozi hao walipowasili uwanjani hapo.
Hali hiyo pia iliwaathiri wapigapicha wa vyombo vya habari ambao
walikwaruzana na polisi na walinzi wa Chadema walipokuwa katika harakati za
kutekeleza majukumu yao.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa hakuhudhuria uzinduzi huo kutokana
na kile kilichoelezwa na viongozi wa chama hicho kwamba yuko nchini Italia kwa
safari ya kikazi.
Mbowe ambana Tendwa
Katika mkutano huo, Mbowe alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa kutoa tamko juu ya CCM kukiuka Sheria ya Uchaguzi kwa kutumia kiasi cha Sh220 milioni wakati wa mikutano miwili ya kupitisha mgombea wao wa ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki. Mbowe alisema Sheria ya Uchaguzi mdogo imeweka kiwango cha juu cha matumizi ya fedha ambazo zinapaswa kutumika zisizidi Sh80 milioni. “Tunamuomba Tendwa atoe tamko juu ya hili, kwani mkutano wa kwanza wa CCM walikuwa na wajumbe 1,034 ambao kila mmoja alilipwa posho ya Sh50,000 na walitumia zaidi ya Sh100 milioni na mkutano wa pili ulikuwa na wajumbe1,044 ambao walitumia zaidi ya Sh120 milioni,” alisema Mbowe. Alisema chama hicho, kilikuwa na wajumbe 888 na kilitumia kiasi cha Sh6.2 milioni pekee kutokana na usafiri na chakula kwa wajumbe. Akizungumzia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Mbowe aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutambua kuwa uchaguzi huo sio wa Meru pekee bali una sura ya kitaifa. “Taifa zima linafuatilia Arumeru Mashariki kujua mnafanya nini, nawaomba sana mtuchagulie Joshua Nassari ili mtuongezee nguvu bungeni dhidi ya chama cha magamba kwani mbunge mmoja wa Chadema ni sawa na wabunge 30 wa CCM,” alisema Mbowe. Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mbowe alilalamika kwa kitendo cha kukataa vijana wenye umri unaofikia miaka 18 hadi 19 kutopiga kura sambamba na watu waliohamia Meru katika kipindi cha miezi 13 tangu kufanyika uchaguzi mkuu. “Haki ya kupiga kura sio ya Tume ya Uchaguzi au Serikali ni haki ya kikatiba ya wananchi hivyo nimempigia simu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji mstaafu, Damian Lubuva lakini amesisitiza ambao watapiga kura ni wale waliojiandikisha mwaka 2009,”alisema Mbowe. Mbowe pia alieleza kusikitishwa na uamuzi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP) Saidi Mwema kuleta Meru magari zaidi ya 40 ya polisi, magari manne ya kumwaga maji ya kuwasha na shehena kubwa ya mabomu ya machozi. “Mambo yote haya ya nini, tunaomba polisi mtuachie CCM tucheze nao na msitulaumu pale ambao mtasababisha vurugu,” alisema Mbowe. Kauli ya Nassari Kwa upande wake Nassari aliomba wakazi wa Meru wamtume kuwa mbunge ili awatetee ardhi yao, inayomilikiwa na wachache, asaidie kushughulikia tatizo la maji, ajira kwa vijana na masoko ya uhakika ya bidhaa mbalimbali, ikiwepo soko la kila wiki la Mbuguni Nasari pia ambaye alimtambulisha mama yake mzazi na baba yake, jukwaani na kueleza walimsomesha hadi chuo kikuu kwa fedha za mbogamboga huku mama yake akipigwa na askari mgambo wa halmashauri. Alisema hoja ya CCM kuwa asichaguliwe kwa kuwa hajaoa haina msingi.“Mbona wabunge wengine, Zitto Kabwe, John Mnyika na David Silinde ambaye tulikuwa naye chuo kikuu hawajaoa na wala hawana mpango wa kuoa mapema kama mimi, wamechaguliwa na wanafanya vizuri,” alisema Nassari. Nassari(26) alieleza katika uchaguzi wa mwaka huu atahakikisha wanashirikiana na kulinda kura kwani kuna hofu ya kura zake kuibiwa kama ilivyotokea katika uchaguzi uliopita ambapo alichuana na marehemu Jeremiah Sumari. Shamrashamra Mbali na hamasa ya helikopta, uzinduzi huo pia ulishuhudia maandamano kutoka pande mbili za barabara kuu ya Moshi – Arusha, ambako kulikuwa na maandamano ya magari na mamia ya pikipiki zilizokuwa zimepambwa na bendera za Chadema na mabango ya picha za Nassari.Maandamano hayo yalisababisha kufungwa kwa muda kwa barabara hiyo na kukwaza usafiri kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Hali hiyo pia ilijitokeza wakati wa jioni baada ya kampeni kumalizika kwani
misafara mirefu yenye magari na pikipiki ilisababisha msongamano katika
barabara hiyo.
Kutoka upande wa Moshi maandamano ya pikipiki yaliongozwa na Mbunge wa
Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, wakati kutoka mjini Arusha maandamano
yaliongozwa na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema.
Muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano huo, aliingia farasi ambaye alikuwa amebeba mabango ya picha za Nassari na bendera za Chadema.
Viongozi wengine
Zitto aliwaomba wananchi wa Arumeru kuenzi msingi ulioasisiwa na wazee wao kwa kusimama kutetea haki dhidi ya uonevu akitaja tukio la mwaka 1951 walipochanga fedha na kumtuma Mzee Japhet Kirilo kwenda Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN), kudai ardhi ya Meru iliyokuwa ikikaliwa na walowezi wa kikoloni.
“Meru mlimtuma Mzee Kirilo UN kudai ardhi yenu, sasa ni wakati wa kumtuma
kijana wenu Nassari (Joshua) kuwatetea bungeni. Ubora wa Nassari hauko kwenye
ujana wala elimu yake, bali chama chake cha Chadema anachotoka ambacho kimejipambanua
kuwa mtetezi wa haki Tanzania,” alisema Zitto
Zitto aliwataka wana Arumeru kuonyesha kuwa wanachukia vitendo vya kifisadi vinavyofanyika nchini pamoja na maisha magumu yanayowakabili kwa kumpigia kura mgombea wa Chadema na kumnyima kura yule wa CCM ambaye chama chake ndicho kinawajibika kwa yote mabaya yanayowakuta Watanzania. Meneja wa kampeni za ubunge katika jimbo hilo, Mchungaji Yohana Natse, amewataka viongozi wa dini na madhehebu yote nchi kuliombea taifa ili viongozi waweze kutenda haki kuepuka nchi kuingia kwenye migogoro na migomo kila kukicha unaosababishwa na watu kukosa haki.
Natse ambaye ni Mbunge wa Karatu, alisema taifa lisilotenda haki hugubikwa
na mambo ya aibu, migogoro na mifarakano isiyokwisha na alitumia fursa hiyo
kumwomba Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva
kutumia uchaguzi mdogo wa Arumeru kuonyesha tofauti kati yake na uongozi
uliopita uliotuhumiwa kukibeba chama tawala, CCM.
Kwa upande wake, meneja mwenza wa kampeni hizo, Vicent Nyerere aliwataka
wana Arumeru Mashariki kupiga na kulinda kura zao siku ya uchaguzi ili
kudhibiti wizi na hila unaoweza kufanyika kukibeba CCM huku akijinadi kuwa mtu
mpole lakini asiye mwoga.
Naye Kamanda wa Oparesheni za Chadema katika uchaguzi huo, John Mrema aliomba NEC kuleta fomu namba 17 kwa wingi katika jimbo hilo kuruhusu waliopoteza shahada zao za kupigia kura kushiriki uchaguzi huo na hivyo kudhibiti tabia ya kununua shahada inayofanywa na baadhi ya watu.
Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, alitamba kushiriki kampeni za Meru
bila kujali vitisho vya yeye kupigwa marufuku vilivyotolewa na mtu aliyemtaja
kama ndugu wa mgombea wa CCM, Siyoi Sumari akibainisha kuwa kuanzia kesho
atapiga kambi Arumeru hadi ushindi utakapopatikana huku akivionya vyombo vya
dola kutotumia nguvu dhidi ya maamuzi ya umma katika uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la vijana Chadema (Bavicha), John Heche
aliwataka vijana wa chama hicho kuwa watulivu na kuepuka vurugu kipindi chote
cha kampeni lakini wasiwe wanyonge wala kukubali kuonewa.
Wabunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Rebeca Mngodo na Joyce Mukhya kwa
pamoja waliwaasa wana Arumeru Mashariki kutokubali kurubuniwa na kutopiga kura
kwa ushawishi wa fedha huku wakiuchekesha umati uliohudhuria mkutano huo kwa
kuwaambia ‘wale CCM lakini kura wapige Chadema.’ | |||||||||||||||||
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia