SHULE ya sekondari ya Naisinyai
iliyopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa
nishati ya umeme hivyo kufanya wanafunzi wake washindwe kujisomea ipasavyo
nyakati za usiku.
Changamoto hiyo,imeelezwa na
Diwani wa kata ya Naisinyai,Kilempu Ole Kinoka wakati akizungumza na wageni
mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kutoka nchini Marekani na China
waliotembelea shule hiyo.
Wageni hao waliofika nchini kupitia
Kampuni ya TanzaniteOne na kutembelea shule za msingi New Vision ya mji wa Mirerani,Oloshonyokie
na Naisinyai na waligawa zawadi za vifaa vya masomo na kuangalia mazingira ya
shule hizo.
Kinoka alisema kutokana na ukosefu wa
nishati hiyo pia walimu wa shule hiyo wanaendesha maisha yao katika mazingira
magumu hivyo kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo wa kuwasomesha wanafunzi
hao.
Hata hivyo,wageni hao kupitia Mkurugenzi
wa mfuko wa Tanzanite Foundation wa kampuni ya TanzaniteOne,Hayley Henning
waliahidi kuisaidia shule hiyo gharama za kuweka nishati ya umeme wa jua
(sola).
Kabla ya kufika kwenye shule hiyo wageni hao walitembelea shule tatu
za msingi za New Vision,Oloshonyokie na Naisinyai na kuwagawia wanafunzi zawadi
za kalamu,madaftari na mabegi ya kubebea vifaa hivyo.
Glory Kayombo mwanafunzi wa shule ya
msingi New vision,inayomilikiwa na Diwani wa viti maalum Tarafa ya Moipo,Rachel
Kinariki alisema shule hiyo yenye baadhi ya watoto yatima inakabiliwa na
changamoto mbalimbali.
Kayombo alizitaja baadhi ya changamoto
hizo ni uchache wa madarasa wanayosomea,jengo la utawala na upungufu wa chakula
lakini wamejenga madarasa manne ambayo hayajakamilika.
Naye,mmiliki wa shule hiyo Diwani
Kinariki,aliishukuru kampuni ya TanzaniteOne ambayo hivi karibuni ilitoa msaada
wa chakula kwa wanafunzi wa shule hiyo na baadhi ya viongozi wa kampuni hiyo
wakashiriki kula pamoja nao.
Pia wageni hao,walipofika kwenye
shule ya msingi Oloshonyokie walipewa zawadi za jadi ikiwemo mavazi ya jamii ya
kimasai aliyovishwa Naomi Saran na urembo wa kimasai aliovishwa Henning.