BAWACHA WAISHANGAA SERIKALI KWA KUJIVUNIA KWA MANENO KUMKOMBOA MWANAMKE



WAKATI dunia ikitarajia kuadhimisha siku ya wanawake duniani kesho Baraza la wanawake wa Chadema(Bawacha),limetamka ya kwamba serikali chini ya chama tawala cha  CCM imekuwa ikijivunia mengi katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru kwa kumkomboa mwanamke wa kitanzania kwa maneno badala ya vitendo.

Pia,ameiponda vikali kauli mbiu ya siku ya wanawake nchini inayosema”Ushiriki wa wanawake unachochea maendeleo”huku akisisitiza ya kwamba kauli mbiu hiyo haiedani na hali halisi  kwa kuwa wanawake nchini bado wanakeketwa na kuolewa katika umri mdogo huku serikali ikifumbia macho vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na katibu wa baraza hilo,Naomi Kaihura alisema kwamba  alisema kwamba katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru serikali iliyo chini ya chama tawala imekuwa ikijivunia mengi kwa kumkomboa mwanamke wa kitanzania kwa maneno mengi badala ya vitendo.

Alisema kwamba wanawake nchini wamekuwa wakinyanyasika kwa kukeketwa sanjari na kuolewa katika umri mdogo huku sheria zikiwa bado hazijarekebishwa kuwalinda ipasavyo.

“Serikali chini ya chama tawala inajivunia katika kipindi cha miaka 50 imefanya mengi kwa wanawake lakini ukweli wamezungumza zaidi kwa maneno badala ya vitendo ,kwa mfano kauli mbiu ya mwaka huu haiendani na  ukweli wowote”alisema Kaihura

Alisisitiza ya kwamba mila potofu bado ni kikwazo kwa mwanamke wa kitanzania hivyo aliitaka serikali ibadilishe baadhi ya sheria ambazo zimekuwa zikimkandamiza mwanamke huyo ikiwa ni pamoja na kutunga sheria za kuhakikisha mwanamke anamiliki mali katika familia.

Kaihura,ambaye pia ni waziri kivuli wa wizara ya maendeleo ya jamii,jinsia na watoto alisema kwamba elimu imekuwa ni kikwazo kwa mwanamke wa kitanzania ambapo mwanamke huyo amekuwa akisoma katika mazingira magumu hali inayopelekea kushindwa kufikia malengo yake.

Naye,mwenyekiti wa baraza hilo,Susan Lyimo  alisema kwamba mtoto wa kike ni tunu ambayo inahitaji kutunzwa kwa hali na mali ndani ya jamii mbalimbali hapa nchini.

Alisema watoto wengi wa kike wamekuwa wakikabiliwa na vikwazo vingi kuliko watoto wa kiume ndani ya familia na kuitaka jamii kuwapunguzia  mzigo wa majukumu watoto wa kike ili wapate nafasi ya kupata elimu.

“Mtoto wa kike amekuwa na vikwazo vingi kuliko mtoto wa kiume,mtoto wa kike apatiwe elimu kwa kuwa mazingira ya elimu kwa mtoto wa kike yamekuwa magumu sana hapa nchini”alisema Lyimo

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post