Wabunge nao wanajitokeza kwa wingi kumnadi mgombea wao
wananchi bado wanaendelea kufatialia kampeni hapo ni Kijiji cha Akeli Arumeru Mashariki ambapo CHADEMA
Wamemsimamisha Joshua Nassari Kuwa Mgombea wa kiti cha Ubunge Arumeru
mashariki.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza mkakati wa
kutotegemea ruzuku ya Serikali pamoja na fedha chafu katika harakati
zake za kisiasa kwa kuwa utegemezi huo unavidumaza vyama vya siasa.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman
Mbowe, alitangaza mkakati huo juzi usiku mjini hapa alipokuwa akizindua
mpango wa Movement for Change (M4C), ambao unalenga kuwafanya wananchi
wa kada zote kukichangia ili kiweze kuendesha harakati za mageuzi ya
kidemokrasia.
Alisema amepata taarifa kwamba Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kinalenga kufuta ruzuku kwa vyama vya siasa kwa lengo
la kukikomoa chama chake, akieleza kwamba serikali inataka kuafiki hila
hiyo kwa kuwa vyama vingi vinategemea ruzuku kujiendesha.
"Tumebaini hila hii mbaya yenye lengo la
kuviumiza vyama vya siasa na sisi tumeamua kuzindua Movement for Change
ili kuwapa fursa Watanzania wenye mapenzi mema na taifa letu kuchangia
harakati za ukombozi wa demokrasia kama walivyofanya babu zetu wakati wa
kudai uhuru wetu," alisema.
Alisema kupitia mpango huo, Chadema
inalenga kutoa elimu ya uraia pamoja na ya Katiba nchi nzima, kuanzia
ngazi ya Kijiji, Kata, Tarafa hadi Taifa.
Alisema "tunataka chama chetu kitokane na
watu, wanaoongozwa na viongozi wasafi waliochaguliwa na watu wenye
mapenzi mema, ambao hawatokani na fedha za mafisadi."
Mbowe alisema M4C, hautapokea fedha chafu
ama za mafisadi kwa kuwa fedha zitakazopatikana zinalenga kuwafundisha
wananchi haki zao na namna ya kuzidai.
"Hatutavunja sheria, tutaheshimu serikali
na vyombo vyote vya dola lakini hatutakubali kuonewa, tutawaambia
Watanzania kwamba haki haiombwi bali inadaiwa na wawe jasiri kuidai,"
alisema.
Mbowe aliongeza kwamba "leo tunazindua
mpango wa kuondoa woga kwa Watanzania kwa sababu wengi wanaishi kwa hofu
wakidhani kusaidia upinzani ni kufilisika."
Alisema “tunajua wanajipanga kufuta
ruzuku…tunawaambia wameshachelewa, wakiamua kufuta ruzuku waanze hata
kesho. Chadema imejengwa na wanachama wenye moyo, ilikuwa hivyo, imekuwa
hivyo, itakuwa hivyo na itaendelea kuwa hivyo.”
Uzinduzi wa mpango huo ulihudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwemo wabunge pamoja na
wafanyabiashara wa Jiji la Arusha.
Katika uzinduzi huo, M4C iliweza
kuchangisha fedha taslimu Sh. milioni 150 ambazo zilichangwa papo hapo,
hundi na kupitia mitandao ya simu za mkononi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk. Wilbrod Slaa, alisema chama hicho kimeendelea kupata mafanikio ya
kisiasa kutokana na mfumo wa kiongozi kilichojiwekea hususani uwakilishi
unaofanywa na wabunge wake ndani na nje ya Bunge.
"Tutapambana na tunasema safari hii
hatutakubali kuibiwa kura, tunasema kabisa kwamba Arumeru kama haki
haitatendeka patachimbika," alisema.
Dk. Slaa amvaa Lowassa
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa
amemshambulia Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, anayedaiwa
kuwasili jimboni Arumeru Mashariki kimya kimya kwa ajili ya kukiongezea
nguvu chama chake akifanya kampeni za chini chini kwa ajili ya kumsaidia
mgombea wa CCM, Sioi Sumari.
Akihutubia mikutano ya hadhara katika
Kata za King'ori, Leguruki, Makiba na Usa River jana, Dk. Slaa alisema
Lowassa hana sababu ya kujificha kwa kufanya kampeni za chini na badala
yake amemtaka apande jukwaani ili washindane kwa hoja.
"Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu kwa
kashfa ya wizi, leo anapita chini chini kuwaambia nini? Mwambieni apande
jukwaani tumpe haki yake...tumkaange," alisema.
Alisema inashangaza kumwona Lowassa
akijipendekeza kwa wananchi wa Meru wakati huu wa uchaguzi ilhali
alikuwa na nafasi ya kuwaletea maendeleo alipokuwa mtumishi serikalini
hasa alipokuwa Waziri Mkuu.
"Ninyi mna shida ya maji, zahanati,
barabara, shule na viongozi wenu wa Halmashauri wanafuja fedha zenu na
hajawahi kuwasaidia, leo atawezaje? Kama anabisha mwambieni apande
jukwaani anadi sera sio kuzungumza na mtu mmoja mmoja," alisema.
NASSARI NA MFUKO WA JIMBO
Kwa upande wake, mgombea ubunge katika
jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, alisema Tanzania na hususani
mkoa wa Arusha, inautajiri mwingi wa madini pamoja na ardhi lakini
wananchi wake wanakabiliwa na umasikini uliokithiri.
"Nimekwenda Kata ya Magadini, mama mmoja
akaniambia alijifungulia kwenye gari linalokokotwa kwa Punda akiitafuta
hospitali, Arumeru Mashariki inakabiliwa na changamoto nyingi wakati
tumekuwa tukitengewa mamilioni ya fedha kila mwaka, nichagueni mimi
nikazisimamie kwa manufaa ya Meru," alisema.
Alisema kila mwaka kwa miaka mitatu
mfululizo, mfuko wa maendeleo ya jimbo (CDF), ambao umekuwa ukitengewa
fedha zinazosimamiwa na mbunge wa jimbo husika, umekuwa ukitengewa Sh.
milioni 47 lakini matumizi yake hayaonekani.
"Mkinichagua niwawakilishe, nitarudi
kwenye kila kata tuainishe kwa pamoja mahitaji ya kila eneo ili
tuyatekeleze kwa awamu, tunahitaji maji, barabara, madawati na dawa
kwenye zahanati na sio kufutana machozi," alisema Nassari.
Nassari aliwataka wananchi wa jimbo hilo wamchague kwa kuwa "siendi bungeni kulala wala kuzomea, bali kuwawakilisha ninyi."
MJADALA WA AJIRA WAIBUKA TENA
Suala la mjadala wa tatizo la ajira kwa
vijana limeibuka tena katika kmpeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Arumeru Mashariki baada ya Mbunge wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi
(UVCCM), Ester Bulaya kuwataka wapiga kura kutoona tatizo hilo limeletwa
na Serikali ya chama hicho.
Bulaya aliyasema hayo wakati akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari katika viwanja vya Patandi kwenye mkutano wa kampeni za CCM.
Alisema kuwa tatizo la ajira ni tatizo ambalo linaikabilI hata nchi zilizoendelea zaidi ya Tanzania.
Alitoa mfano wa nchi ya Afrika ya kusini ambayo ina vijana zaidi ya milioni tatu ambao hawana ajira.
Alisema watanzania wanapaswa kuacha kuwa
watumwa wa maneno ya uongo yanayosamabazwa na wapinzani wa Serikali ya
CCM ya kuwa imewaacha vijana.
Alisema kuwa matatizo yanayowakabili
vijana hayajasababishwa na CCM ambayo kwa nia njema inatengeneza sera na
mipango mbalimbali ya kusaidia kupunguza tatizo hilo.
Naye Sioi akiomba kura aliwataka vijana
kumuunga mkono kwa kumpa kura zote ili ashirikiane nao katika kuanzisha
miradi ya kupunguza makali ya umasikini.
Aliwataka kutokubali kudanganywa na
wapinzani wake kisiasa ambao hawana serikali na kuwataka kuiunga mkono
CCM kwa kumpa kura. “Eneo hili ndio nyumbani vijana msiniangushe na
mimi sitawaangusha mkinipa kura zenu,” alisema.
Na katika hatua nyingine mgombea huyo wa
CCM alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuelezea kwa undani sera
na mikakati yake ya kushughulikia matatizo mbalimbali yanayowakabili
wananchi wa jimbo hilo ikiwa atafanikiwa kupata nafasi ya uwaikilishi
bungeni.
Alisema kuwa tatizo la maji na ajira kwa vijana ni mambo ya msingi sana atakayoshuhulikiwa ikiwa atapata nafasi hiyo.
“Vijana wafahamu wakinipa kura
nitawahamasisha waanzishe vikundi vya ujasiriamali ,uanzishawaji wa
viwanda vidogo vidogo ili kutoa fursa za kiuchumi”alisema Sioi.