KAMPUNI ya madini ya TanzaniteOne imetumia
sh30 milioni kugharamia kupaua na kuezeka mabati ya madarasa ya shule ya
sekondari Naisinyai ya wilayani Simanjiro mkoani Manyara yenye kusomesha
wanafunzi wa kata nne za Tarafa ya Moipo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni ,Ofisa mahusiano wa kampuni ya TanzaniteOne,Halfani Hayeshi alisema kampuni
hiyo pia inatarajia kupaua na kuezeka madarasa mengine mawili ya shule hiyo
mwezi ujao.
Hayeshi alisema huo ni mwendelezo wa
upauzi wa ujenzi wa madarasa kwani awali walipaua madarasa mengine sita ya
shule hiyo,hivyo gharama yake kufikia sh30 milioni katika upauzi wa madarasa
hayo.
“Kampuni ya TanzaniteOne kwa kutumia
kiasi cha sh30 milioni tumelenga kusaidia jamii kwa kupaua na kuezeka mabati ili
wanafunzi wa eneo linalotuzunguka wapate elimu katika mazingira bora,” alisema
Hayeshi.
Aliongeza kuwa ili kuunga mkono
juhudi za maendeleo ya jamii kwenye eneo hilo kampuni yake imeweza kununua
vitanda 400 vya wanafunzi wanaolala kwenye mabweni ya shule hiyo.
“Vitanda hivyo tumeshavikabidhi kwa
uongozi wa shule hiyo tangu mwaka jana na hivi sasa wanafunzi wa shule hiyo
wanaendelea kulala na kumalizia tatizo la kutembea umbali mrefu wa kwenda na
kurudi nyumbani,” alisema Hayeshi.
Naye,Diwani wa kata ya
Naisinyai,Kilempu Ole Kinoka aliipongeza kampuni hiyo kwa juhudi zao za kuunga
mkono maendeleo ya kata hiyo hivyo kutia chachu kwa jamii inayozunguka eneo
hilo.
“Kwa kweli napenda nipongeze juhudi
za kampuni ya TanzaniteOne kwani imekuwa msaada mkubwa wa kuleta maendeleo ya
namna moja au nyingine kwenye kata yetu ya Naisinyai,” alisema Ole Kinoka.
Shule ya sekondari Naisinyai iliyopo
wilayani Simanjiro inasomesha wanafunzi mbalimbali wa kutoka kwenye kata nne za
Naisinyai,Mirerani, Endiamtu na Shambarai zilizopo Tarafa ya Moipo.