BREAKING NEWS

Monday, March 12, 2012

MKUU WA MKOA WA ARUSHA AONYWA


mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo
KAMATI tendaji ya jumuiya ya tawala za mitaa nchini(Alat) imemwonya mkuu wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo  kuacha  kujichukulia sheria mikononi  kwa kuamuru mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Monduli kukamatwa na kuwekwa ndani kitendo ambacho  wamedai ni udhalilishaji dhidi ya mtumishi huyo wa umma.

Pia,imesikitishwa na kitendo cha serikali kufuta ruzuku za jumla kwa halmashauri mbalimbali nchini kwa kuzitaka halmashauri hizo kukusanya fedha zao kupitia kodi za leeni na kusema kwamba kitendo hicho kinaleta changamoto katika shughuli za uendeshaji wa halmashauri zao.

Hivi karibuni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Monduli mkoani Arusha,Samwel Mlay alikamatwa na jeshi la polisi na kisha kuwekwa ndani kwa agizo la mkuu wa mkoa wa Arusha baada ya kudaiwa kushindwa kuwawajibisha watumishi waliohusika na uchakachuaji wa mashine ya Excavator.

Akitoa tamko jijini Arusha,mwenyekiti wa Alat taifa,Didas Masaburi ambaye meya wa jiji la Dar es salaam mbele ya wajumbe wa jumuiya hiyo kutoka kila kanda nchini alisema kwamba kamati tendaji ya chama chao imesikitishwa na kitendo kilichofanywa na mkuu wa Arusha kuagiza kukamatwa mkurugenzi wa halmashauri ya Monduli na kisha kuwekwa ndani.

Alisema kwamba kitendo kilichofanywa na mkuu huyo wa mkoa wa Arusha kinawapa mashaka mazito huku akisisitiza kuwa kuwa mkurugenzi wa halmashauri isiwe chanzo cha kuwekwa kizuizini.

“Inapofikia mkuu wa mkoa anaagiza mkurugenzi  akamatwe inatupa mashaka sana,naomba ieleweke kwamba   kuwa mkurugenzi wa halmashauri isiwe chanzo cha kuwekwa kizuizini”alisema Masaburi

Hata hivyo  alisisitiza ya kwamba kuna taratibu mbalimbali za kiutawala za kuwawajibisha watumishi wa halmashauri mbalimbali nchini   vikiwemo vikao vya kiutawala na kushangaa kitendo kilichofanywa na mkuu huyo wa mkoa.

Alisema kwamba jumuiya yao haina lengo la kutetea uovu wa iana yoyote lakini umejidhatiti kutetea haki za wanachama wao pale zinapominywa huku akibainisha kuwa wamejipanga kusimamia haki za wanachama wao kikamilifu.

Katikaa hatua nyingine,Masaburi alilaani  mauaji ya wenyeviti wawili wa halmashauri ya Rukwa na Uyui hivi karibuni na kusema kwamba jumuiya yao imesikitishwa na mauaji hayo na kuitaka serikali ichukue hatua kukomesha mauaji hayo.

Alisema kwamba jumuiya yao imesikitishwa na mauaji ya wenyeviti hao yaliyofanyika katika kipindi cha miezi sita huku akisema kwamba serikali inatakiwa ichukue jitihada kukomesha mauji hayo ama sivyo huenda yakazidi kuendelea.

Wakati huo huo,mwenyekiti huyo alisisitiza kwamba wana wasiwasi kwamba serikali ina nia ya kuua halmashauri mbalimbali nchini  kwa kuwa  awali walianza kuwanyang”anya madaraka,kuwazuia kuajiri na sasa wanazinyima ruzuku katika halmashauri zao.

Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mulongo alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya mkononi na gazeti hili simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.


Share this:

1 comment :

  1. Mkuu wa mkoa tafadhali tumia busara katika kufanya maamuzi yako usisikilize upande mmoja. Hata wewe akija ghafla waziri ambaye wewe uko chini yake lazima atakuta kuna madudu mengi ambayo watu wa chini yako wameyafanya bila wewe kujua. Usiendeshe mkoa kimabavu

    ReplyDelete

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates