RASIMU ya Katiba Mpya; CHADEMA yaitisha Kamati Kuu ya dharura
Katika hatua nyingine, CHADEMA imemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutimiza ahadi yake ya kuleta muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya ili kuepusha mkanganyiko kwenye mjadala wa rasimu iliyotolewa.
Msimamo wa kambi hiyo, ulitolewa jana mjini hapa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akisema kuwa Pinda ameshindwa kusimamia maneno yake, hivyo kuruhusu Bunge kupoteza muda wa siku tano tangu Juni 7 hadi 12 pasipo kuleta muswada huo.
“Mtakumbuka Aprili 4 mwaka huu, Kiongozi wa kambi, Freeman Mbowe katika hotuba yake kwa ofisi ya Waziri Mkuu alitangaza mambo mawili akitaka yatekelezwe, vinginevyo CHADEMA ingejitoa kwenye mchakato wa katiba mpya,” alisema.
Mnyika aliyataja mambo hayo kuwa ni kufutwa kwa mabaraza ya katiba kutokana na uchaguzi wake kugubikwa na rushwa na hila, pili ni kuletwa kwa muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alifafanua kuwa hata Msemaji Mkuu kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu kwenye hotuba yake Aprili 30 mwaka huu, alisema wanaipa muda serikali ilete muswada huo kabla ya rasimu kutolewa.
“Waziri Mkuu aliahidi kutimiza sharti la pili la kuleta muswada, lakini hadi rasimu inatolewa ameshindwa kusimama katika maneno yake. Rasimu imetoka, lakini imeibua mjadala na ubovu wa mchakato ukiachwa utaathiri upatikanaji wa katiba mpya,” alisema.
Aliongeza kuwa rasimu hiyo imezua mjadala kuhusu muundo wa muungano kwa wananchi kuhoji ni kwanini rasimu inaleta muundo huo pekee pasipo kueleza mustakabali wa katiba ya Tanganyika.
Mnyika alieleza kuwa ubovu huo waliubaini mapema ndiyo maana viongozi wa chama hicho walipokutana na Rais Kikwete Ikulu mwaka jana, walimweleza kuwa sheria iliyounda tume ya katiba ibadilishwe ili hatima ya Tanganyika iingizwe kwenye mchakato ili maoni yaguse vyote kwa pamoja.
Mnyika alisema kuwa CCM wanajipanga katika mabaraza kujadili rasimu kwa vile wanajua kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo mbovu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatambua kwamba maoni yote ya mabaraza yana uzito sawa, hivyo tume inaweza kuchakachua.
Alisema CHADEMA kwa sasa hawataki kutoa maoni ya jumla kuhusu rasimu hiyo bali waipitie kwanza neno kwa neno pamoja na wanachama wao nchi nzima wakilinganisha na waraka namba moja wa mapendekezo yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya.
“Baada ya hapo, Kamati Kuu itakutana mwanzoni mwa Julai na kutoa uamuzi. Hata Bunge likimaliza muda wake bila serikali kuleta muswada huo, sisi kama kambi tutalirudisha suala hilo kwa Kamati Kuu ili kulitolea uamuzi,” alisema.
Akigusia kwa uchache maeneo yenye kasoro kwenye sheria hiyo, Mnyika alisema mamlaka na madaraka ya wananchi kwenye kura ya maoni yataporwa ikiwa Tume ya Uchaguzi inayolalamikiwa itaendelea kusimamia mchakato huo.
Pia alitaja mamlaka ya uwakilishi wa wananchi kwenye Bunge la Katiba ambalo kwa mujibu wa sheria hiyo ukiacha wabunge wa sasa, rais ndiye atateua wajumbe wengine baada ya kupokea mapendekezo ya makundi mbalimbali akisema yanapokwa.
Mbowe aitisha Kamati Kuu
Katika hatua nyingine, CHADEMA imeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC), ili kujadili na kutoa msimamo wa chama hicho juu ya rasimu ya katiba mpya, iliyotolewa hivi karibuni, huku kikiwataka wananchi wote kuendelea kuichambua kwa makini na kutoa maoni yao kwa ajili ya kuiboresha.
Chama hicho kimesema kuwa kikao cha Kamati Kuu kitafanyika Jumamosi ya wiki ya kwanza, Julai mwaka huu, ambapo kwa muda wote uliobaki kimesema kitaendelea kuichambua rasimu hiyo 'neno kwa neno' kikisema kuwa ni muhimu kufanya hivyo kwani 'shetani hujificha kwenye maelezo'.
Mbali ya kuwataka wananchi kuisoma kwa makini rasimu hiyo, chama hicho pia kimewaagiza wanachama wote nchi nzima kupitia kwenye mfumo wake wa uongozi kuanzia ngazi ya chini ambayo ni misingi katika ngazi ya vitongoji, kuichambua rasimu kwa kuzingatia waraka namba moja wa chama hicho juu ya maudhui ya katiba mpya ya Tanzania, kisha wawasilishe maoni yao ili yazingatiwe kwenye maamuzi ya kikao hicho cha Kamati Kuu.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe juzi mjini Ifakara, kwenye mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Ifakara, alipokuwa akimnadi mgombea wa chama hicho, Peter Lijualikali.
Mbowe alisema kuwa tangu Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya itoe rasimu hiyo, chama hicho hakijatoa kauli yoyote, ili kupata muda wa kuisoma na kuichambua kwa makini 'neno kwa neno' nyaraka nzima, kisha kufanya mashauriano ya kitaalamu ndani ya chama, huku kikifanya maandalizi ya vikao kwa ajili ya maamuzi na hatimaye msimamo wao kwenye hatua hiyo ya mchakato wa katiba mpya.
“Ndugu zangu wananchi wenzangu wa Ifakara, katika mkutano huu wa kampeni za kumnadi mgombea wetu, naomba pia nitumie fursa ya kutoa tamko la kitaifa kuhusu suala muhimu sana na nyeti la katiba mpya. Tangu Tume imetoa rasimu ya katiba mpya, chama chenu kimekuwa kimya, kwa maana hakijazungumza, hii ni kwa sababu kadhaa.
“Kwanza kabisa tangu siku ya kwanza hadi leo, tumekuwa tukiipitia rasimu hiyo neno kwa neno, kipengele kwa kipengele, maana wanasema 'the devil lies in the details' yaani mzimu hujificha kwenye maelezo, sasa sisi kama mnavyojua tumekuwa chanzo na chachu kubwa ya mchakato huu hadi kufikia hapa ulipo, lazima tuwe makini katika msimamo wetu kama ambavyo imekuwa mara zote.
“Ilikuwa lazima pia tufanye mashauriano, wataalamu wetu waangalie mambo yote ya kitaalamu, neno kwa neno, kisha tukae vikao na kutoa msimamo wa chama chenu. Kama mnavyojua CHADEMA si Mbowe, si Slaa, wala si mtu mwingine yeyote, chama ni vikao. Hivyo tumeitisha kikao cha Kamati Kuu siku ya Jumamosi, wiki ya kwanza ya mwezi wa saba, kisha tutatoa tamko na msimamo wa CHADEMA katika rasimu hii ya katiba,” alisema Mbowe.
Aliongeza: “Wakati tunaendelea kuipitia rasimu hii hadi Kamati Kuu ikae, tunawataka Watanzania wote waendelee kuisoma kwa makini na kutoa maoni yao, lakini pia kwa msisitizo mkubwa kabisa, tunawaagiza wanachama wote wa CHADEMA katika ngazi ya msingi, kwenye vitongoji nchi nzima kukaa vikao, kuisoma na kuichambua rasimu kwa makini, kisha watuletee maoni yao kabla ya kikao hicho ili tuyazingatie kwenye maamuzi na utoaji wa msimamo wetu kama chama.
“Tunawakata wanachama wetu kuipitia rasimu yote kwa kurejea Waraka Namba Moja wa mwaka 2013 uliopitishwa na Baraza Kuu la chama mapema mwaka huu, hasa sehemu ya pili ambayo ilikuwa inaelezea maoni ya CHADEMA juu ya maudhui ya katiba mpya ya Tanzania.”
Mbowe akirejea kwa kutoa mifano namna chama hicho kilivyosukuma agenda ya katiba mpya kwa ajili ya mabadilio ya kimfumo na kiutawala kwa muda mrefu na kuweka msisitizo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, alisema kuwa watu wengi, hasa walioko madarakani leo, waliibeza CHADEMA, lakini leo wanakubali kuwa kiliona mbali.
Akitumia kaulimbiu maarufu ya chama hicho 'nguvu ya umma', Mbowe aliwataka Watanzania kuendelea kukiunga mkono katika kusimamia na kuhakikisha nchi inapata katiba mpya, huku akisema hawako tayari kuona wakuu wa wilaya na mikoa wakiendelea kuwemo kwenye katiba mpya.