Mwenyekiti
wa Chadema, Mh freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini Mh Godbless Lema
wakiwa katika uwanja wa Soweto mchana wa leo wakati zoezi la kuchukua
vipimo mbalimbali likiendelea chini ya usimamizi wa wataalamu toka
Jeshini.
Mbowe na Lema wakishauriana jambo..
Eneo
la maafa. Inaelezwa kuwa wataalamu wa jeshi waligundua kuwako kwa kitu
ndani ya tanki la mafuta na hivyo kuamua kulikata. Taarifa hizo zinadai
kwamba kulikuwa na mabomu yametegwa chini ya gari na hivyo tank hilo
lilishmabuliwa kwa risasi labda utokee mlipuko! Pia gari hii ya
amatangazo ina majeraha mawili mlango wa kushoto yaliyotokana na kitu
chenye ncha mabacho kinaweza kuwa risasi au vipande vya vyuma vya bomu.
Mh Mbowe akiwa nyumbani kwa wazazi wa mmoja wa marehemu (Ramadhani) eneo la Mianzini kuwapa pole kwa kuondokewa na mpendwa wao.
Kamanda
wa Chadema ambaye alikuwa ni mlinzi wa amani (Red Brigade) katika
mkutano huo, Bw Kitumbwizi akiugulia maumivu katika hospitali ya Selian
alikolazwa baada ya kujeruhiwa katika mlipuko huo. Huyu amaumizwa mguu
mmoja, mkononi na sehemu ya kwapani ambapo imegundulika kuwa kuna chuma
ama risasi ndani ambayo imekuwa ngumu kutolewa mapaka sasa.
Mlipuko
wa bomu uliotokea Arusha na kusababisha vifo vya watu watatu na
kujeruhi 70 limezua utata kutokana na hisia tofauti za viongozi
mbalimbali nchini waliozungumzia suala hilo, huku Rais Jakaya Kikwete
akisema haamini kama Watanzania sasa wamefikia hatua ya kuanza
kuhasimiana kwa misingi ya kisiasa.
Hii
ni mara ya pili kwa Jiji la Arusha kushambuliwa kwa bomu baada ya lile
lililorushwa kwenye Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi
kwenye Parokia ya Olasiti wakati wa sherehe ya uzinduzi wake Mei 5,
mwaka huu na kuua watu watatu na kujeruhi 64. Wakati Rais Kikwete
akisema hayo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba wamesema tukio hilo ni la kisiasa na
lilipangwa.
Kufuatia tukio hilo, uchaguzi wa kata nne za Arusha mjini umeahirishwa hadi Juni 30.
Taarifa
iliyotolewa na Ikulu jana imeeleza kuwa Rais Kikwete ambaye yuko nchini
Uingereza kuhudhuria mkutano wa nchi zilivyoendelea kiviwanda(G8),
alisema haamini kama Watanzania ama wafuasi wa vyama vya siasa
wanachukiana kiasi cha kudiriki kufanya matukio ambayo yanahatarisha
usalama wa watu.
“Mimi
siamini kuwa Watanzania au wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana
kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii. Naamini kuwa hiki ni
kitendo cha mtu ama watu wasioitakia mema nchi yetu, watu ambao
wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni mwa raia ama
makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko makubwa.”
Mbowe
Akizungumzia
suala hilo, Mbowe alisema shambulio hilo la bomu ni la kisiasa na
lililenga kumuua yeye na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema.
“Haya
ni mauaji ya kisiasa ya kupanga, tumeokota maganda ya risasi za bastola
na SMG na tumepiga picha na kuwapa polisi katika eneo la tukio, gari
letu lilipigwa mlango na vioo kwa risasi na kesho wabunge wote wa
Chadema watakuwa hapa Arusha na wataondoka baada ya mazishi,” alisema
Mbowe.
Mbowe
alisema pia wamebaini bomu lililorushwa ni la kiwandani na shambulizi
hilo liliandaliwa na kikosi cha watu wengi wenye lengo la kufanya mauaji
makubwa.
Alisema
kilichomwokoa na kifo ni kushuka jukwaani saa 11:43 kabla ya muda wa
kawaida wa saa 12:00 kwani ilipangwa washambuliwe wakiwa juu ya jukwaa.
“Tunasikitika
sana, watu wamekufa wasio na hatia na msiba huu utakuwa wa kitaifa na
tunatarajia kuaga miili katika uwanja huohuo wa Soweto,” alisema Mbowe.
Profesa Lipumba
Kwa upande wake, Profesa Lipumba alisema watu waliohusika kulipua bomu walipanga kuvuruga uchaguzi huo uliyokuwa ufanyike jana.
Alisema
CUF walikuwa na nguvu katika baadhi ya maeneo ya uchaguzi Arusha ndiyo
mana watu wameamua kuvuruga uchaguzi ili usifanyike.
“Sisi
tumewasimamisha wagombea udiwani ambao ni Abbas Mkindi, (Kaloleni),
John Bayo (Elerai) na Labora Ndarvio (Themi) na maeneo haya tulitegemea
leo (jana) tushinde ila baadhi ya watu wameamua kuvuruga kwa malengo yao
binafsi,” alisema Lipumba.
Katika
hatua nyingine, Profesa Lipumba amevitaka vyombo vya dola kufanya
uchunguzi wa kina kuwabaini watu waliohusika na milipuko hiyo ili waweze
kuchukuliwa hatua za kisheria.
Nchimbi na Mwema
Wakati
viongozi hao wakigawanyika Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel
Nchimbi na Inspekta Jenerali wa Polisi(IGP), Said Mwema wamesema tayari
jeshi lake limetuma timu inayoongozwa na Kamishna wa Operesheni na
Mafunzo, Paul Chagonja na Kamishna wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya
Jinai, Isaya Mngulu.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana Dk Nchimbi alisema uchunguzi wa awali umebaini
ya kwamba bomu hilo ni la kurusha kwa mkono (hand grenade).
Hata hivyo, Dk Nchimbi alisema hadi sasa hakuna mtuhumiwa yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.
“Uchunguzi
wa awali umebaini kwamba bomu hilo ni la kutupa kwa mkono. Tunachunguza
kujua mlipuko ule ni wa aina gani,” aliwaambia waandishi wa habari
jijini Arusha.
Dk
Nchimbi alitaja orodha ya vifo katika tukio hilo na kusema hadi sasa
watu wawili wamethibitishwa kufa, huku 70 wakiwa wamejeruhiwa ambapo
kati ya majeruhi hao, wawili wako katika hali mbaya. Alisema kwamba
uchunguzi huo unalishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili
kubaini mlipuko uliojitokeza ni wa namna gani.
Naye
IGP Mwema alisema jeshi litaendesha operesheni kali popote nchini ya
kuwasaka na kuwatia mbaroni wote waliowezesha, kufadhili na waliotenda
uhalifu huo. Alisema Jeshi la Polisi linalaani tukio hilo linaloashiria
vitendo vya kigaidi ambalo limesababisha vifo na majeruhi pamoja na
kujenga hofu kwa wananchi.
“Nawashukuru wananchi walioanza kutupa taarifa za mwonekano, wajihi wa mtu aliyetupa bomu hilo,” alisema.
Mwema
aliweka hadharani simu yake ya mkononi yenye namba 0754 785557 akitaka
wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu huo kumpa mwenyewe taarifa au
kwenye vituo vya polisi vilivyo jirani yao.