KIONGOZI UPINZANI BUNGENI MBOWE NA WABUNGE WENGINE WAWILI AKIWEMO LEMA WAZUIWA KUINGIA BUNGENI



Licha ya kanuni za Bunge kuruhusu vazi la safari suti yenye mshono kama kombati zinazovaliwa na baadhi ya wabunge wa CHADEMA, kwa mara ya kwanza Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe na wenzake watatu jana walizuiwa kuingia bungeni.

Mbowe na Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walizuiwa na askari kwa madai kuwa wamevalia sera za chama.


Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni katika viwanja vya Bunge, Lissu alisema walishangazwa na uamuzi huo wakati mavazi hayo wamekuwa wakiyavaa na kuingia nayo bungeni kwa miaka mingi sasa.


Lissu alisema kuzuiwa kwao wanakuchukulia kuwa ni mkakati maalumu wa serikali ya CCM kutaka kuwazima na kuhakikisha hawapati nafasi ya kuingia bungeni ili wasijibu mashambulizi ya tuhuma wazosingiziwa kuhusiana na mlipuko wa bomu jijini Arusha.


“Sisi hali hiyo tulianza kuishtukia tangu asubuhi tulipoingia kwenye eneo la Bunge, kama mligundua kulikuwa na askari wengi sana kila kona kuliko kawaida kana kwamba nchi imepinduliwa. Kinyume cha utaratibu na kanuni, askari wa kawaida wameingiza hadi bungeni.


“Tulipofika wakati wa kuingia ukumbini mimi, Mbowe, Lema na Wenje tuliambiwa haturuhusiwi kwa kuwa tumevaa sare za chama. Tulipouliza nani kawapa maagizo hayo walidai ni uongozi wa juu, yaani Spika wa Bunge,” alisema Lissu.


Aliongeza kuwa kitendo hicho ni kichekesho kwani wakati wote tangu mwaka 2010 Mbowe amekuwa akivalia vazi hilo, achalia mbali wabunge wenzake baadhi ambao mara moja moja nao walikuwa wakivaa suti hizo lakini hawajawahi kuzuiwa.


Hata hivyo, pamoja na uamuzi huo, kanuni za Bunge hakuna mahali zinazuia mbunge kuvaa sare ya chama chake isipokuwa kanuni limeainisha aina za mavazi ya kuvaliwa na wabunge wanawake na wanaume.


Kwa mujibu wa kanuni ya 149 (3)(a) Kwa wanawake na (b) Kwa wanaume inasema: (a) Kwa wanawake;- (i) Vazi lolote la heshima yaani ambalo si la kubana mwili, lisiloonesha maungo ambayo kwa mila na desturi za Kitanzania hayapaswi kuoneshwa na ni refu kuvuka magoti.

(ii) Gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au sketi ya rangi yoyote (iii) Kilemba cha kadiri au mtandio (iv) Suti ya kike; au (v) Vazi linalovaliwa wakati wa eda.
(b) Kwa wabunge wanaume;-(i) Suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia; (ii) Vazi la kimwambao yaani ka nzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubadhi au viatu; (iii) Suti kamili ya Kimagharibi ya rangi kadiri isiyomeremeta; (iv) Koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au (v) Tarbushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au mila.

source: Tanzania daima

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia