Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza vyombo vya dola kuwashughulikia
kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya
uvunjifu wa amani
Akizungumza katika Kipindi cha Maswali ya Papo
kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, bungeni Dodoma jana, Pinda alisema watu
wanapokaidi wanajitakia matatizo na vyombo vya dola.
Alisema hayo
alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM),
Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha
na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue
chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya
dola vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya
maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?”
Waziri
Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema... mwishowe unaona anasema vyombo
vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua
kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote tukubaliane
kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama
wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri
zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna
nyingine... maana tumechoka.”
Pinda alisema Serikali imedhamiria
kurejesha amani nchini ikiwamo mkoani Mtwara na kuwataka Watanzania
waiache Serikali ifanye kazi hiyo. Alisema Serikali ina orodha ya watu
wanaosemekana kuwa ni vyanzo vya vurugu na matatizo yaliyotokea Mtwara
na kushangaa wale wanaopinga kukamatwa kwao.
“Lazima tuwakamate
na kama katika kuwakamata watafanya jeuri, jeuri, watapigwa tu kabla ya
kupelekwa tunapotakiwa kuwapeleka, kwa sababu hatuwezi kuendelea na hali
hii, mkadhani kwamba tutafika tunapokwenda. Nami nasema vyombo vya dola
vijipange imara vihakikishe vinadhibiti hali hii,” alisema.
Hata
hivyo, jibu hilo lilipata upinzani wakati Mbunge wa Konde (CUF),
Khatibu Said Haji alipomwuliza Waziri Mkuu: “Hapo awali umetoa kauli
nzito ya kuliambia taifa hili kwamba wale raia wote, ambao watakaokuwa
wakaidi wapigwe tu na watapigwa tu; naomba ninukuu Katika Ibara ya 13 na
Kifungu cha 6B cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
“Ni marufuku
kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kuteswa kama mtu mwenye
kosa, mpaka itakapothibitika anayo hatia kwa kutenda kosa hilo.
“Pia
ibara hiyohiyo Kifungu cha 6 E; kinasema ni marufuku kwa mtu yoyote,
kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazoweza kumdhalilisha.
Kwa kauli yako uliyoitoa huoni kwamba umevunja Katiba?” Akijibu swali
hilo, Pinda alisema ni lazima kutofautisha kati ya mtu
aliyekwishakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria... “Mimi
ninayemzungumza hapa ni mtu yule ambaye ameamua kufanya vitendo
hajakamatwa na ndiyo maana nilikwambia usiandamane... hapa mahali
hutakiwi kwenda wewe ukaamua kutumia mabavu kwa sababu mko wengi, ndiyo
maana nikasema, hawa watu tutashughulika nao hivyohivyo.”
Mbunge huyo hakuridhishwa na majibu hayo na kumtaka Waziri Mkuu kuyafuta.
Hata
hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliingilia katika na kumweleza
mbunge huyo kuwa kila mtu alikuwa amemwelewa Waziri Mkuu na hakukuwa na
haja ya kuendelea na hoja hiyo.
Kabla ya swali lake la nyongeza,
Mangungu aliuliza: “Ukisikiliza nyimbo nyingi za taifa katika Afrika
zinasema hekima, umoja na amani ndiyo ngao zetu. Je, hali ambayo
imejitokeza katika nchi yetu na matatizo yaliyojitokeza Arusha na maeneo
mengine kama Mtwara. Nini tamko la Serikali?
Waziri Mkuu
alijibu: “Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mangungu ni jambo
linalotugusa sisi wote. Suala la amani, ulinzi, utulivu ndiyo hasa tunu
ya kila nchi ingependa kuwa nayo. Ni kweli hivi karibuni kumejitokeza
vurugu za hapa na pale kwa hiyo angependa tuwaeleze Watanzania kama
Serikali tunafikiria tufanye nini.
Alisema ipo haja ya jukumu
hilo kuachwa kwa viongozi wa kisiasa bila ya kujali itikadi zao... “Yako
mambo ambayo lazima tukubali kwamba ni jukumu letu sisi wote na kila
mmoja lazima azungumze lugha moja.
Ninyi wote ni mashahidi.
Chadema waliposhinda hapa, wao walikuja waziwazi, wakasema tutahakikisha
nchi hii haitawaliki. Sasa, inawezekana pengine ndiyo mwendelezo wa
utekelezaji wa kauli hizo.
“La pili ni upande wa Serikali, lazima
tuhakikishe kwamba wale wote ambao kwa kweli wanajaribu kuvunja amani
kwa namna yoyote ile, kazi kubwa tuliyonayo ni kubanana, kupambana
kwelikweli kwa njia zozote zile zinazoonekana zinastahili.
“Sasa
mimi ninaomba sana Watanzania, maana kila juhudi zinapoonekana
zinaelekea huko, unapata watu wengine wanajitokeza, unajua...unajua.
Acheni Serikali itimize wajibu wake kwa sababu jambo hili ni la msingi,
lazima tulilinde kwa nguvu zetu zote.
“Rai yangu kwa Watanzania
kila mmoja ajue kwamba siku tukiingia katika vurugu, hakuna mshindi.
Wote tutaumia, sasa wote tuhakikishe hili jambo tunalisimamia vizuri.”
Chadema waja juu
Akizungumzia
kauli hiyo, Mkurugenzi Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika
alisema: “Kauli ya Pinda inakiuka Katiba ya nchi na imethibitisha kwamba
matumizi mabaya ya vyombo vya dola na kusababisha mauaji ya raia yana
baraka za Serikali.”
Alisema kauli ya Pinda kama ilivyokuwa ya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi zinatoa mwelekeo kwamba mauaji ya Arusha yana baraka za Serikali.
Wanasheria wakerwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Waziri
Mkuu hakustahili kutoa kauli kama hiyo.
Alisema Pinda hapaswi
kuwa na jazba, bali anatakiwa kuwa na busara na kuzungumza kwa
kuzingatia sheria za nchi badala ya kutoa matamshi ambayo siyo mwafaka
kwa nchi inayoongozwa kwa kufuata sheria na taratibu.
Rais wa
Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Francis Stola alisema kauli
hiyo ya Waziri Mkuu, mbali ya kwenda kinyume cha Katiba na sheria ya
nchi, inaweza kuhatarisha amani.
Stola alisema matumizi ya nguvu kupita kiasi kudhibiti hali yoyote korofi hayaruhusiwi.
CHANZO: MWANANCHI