Ijumaa
iliyopita itajulikana kama siku mlango mdogo ila muhimu sana
ulipofungua kitasa chake kwa baadhi ya wananchi wanaojituma kikazi na
kibiashara Tanzania. Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda alitembelea
soko la mboga na matunda lililoko Leytonstone, mashariki ya London.
Matembezi yalidhihirisha mahusiano ya ujirani mwema kati yetu
Watanzania na Kenya yenye kampuni iliyoshajijenga ndani ya soko hili
maarufu na kubwa sana.
Soko
hilo linaloitwa Spitalfields si sehemu inayofahamika na wengi wanaoishi
Uingereza licha ya kwamba jina hilo si rahisi kutamka au kuandikwa.
Lakini Spitalfields (tamka “Spitol-fildz”), itakua eneo muhimu sana kwa
vijana, wakulima na wafanyabiashara Tanzania, miaka ijayo.
Hapa
ndipo mboga na matunda toka sehemu mbalimbali duniani huletwa halafu
zikasambazwa maduka makubwa ya vyakula Uingereza. Hivyo basi mlango
kufunguliwa ni “uwanja muafaka” kwa wote wanaojituma na kutaka
maendeleo kiuchumi.
Spitalfields
ina zaidi ya miaka mia tatu. Ingawa ilipoanzishwa makao yake yalikuwa
mtaa wa Brick Lane karibu na Liverpool Street, leo tawi jipya, New
Spitalfields Market limehamishwa karibu uwanja yalipofanyika mashindano
ya Olimpiki mwaka jana. Tawi hili lilifunguliwa rasmi 1991 na
linaongoza Ulaya nzima kwa usambazaji wa matunda na mboga toka nchi
zenye joto duniani.
Kati
ya nchi hizo ni ndugu zetu wa Kenya kupitia kampuni ya SACOMA(“Sahara
Communities Abroad”) iliyoanzishwa mwaka 2000 kuendeleza wananchi
wasiojiweza kiuchumi na kielimu walioko jimbo la kusini ya jangwa la
Sahara wanaozungumza Kiswahili. Licha ya kusafirisha bidhaa na kuziuza
New Spitalfields, SACOMA , anasema msemaji wake Bi Perez Ochieng hutoa
ajira kwa takriban watu 30,000 Ulaya na Kenya.
Perez
Ochieng, mumewe Sam Ochieng (mkurugenzi SACOMA) na meneja mwendeshaji
New Spitalfields, Bw. Nigel Shepherd walimtembeza Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akiongozana na Balozi wetu Ungereza , Mhe Peter Kallaghe,
mkurugenzi wa Kituo cha Biashara Tanzania, London, Yusufu Kashangwa na
maofisa wengine. Ubalozi wa Tanzania Uingereza ndiyo ulioratibu na
kuandaa tukio zima.
Waziri
Mkuu na wenzake walikuja London kuhudhuria mkutano wa kimataifa
unaoangalia namna ya kuondoa njaa na umuhimu wa lishe bora kwa kina mama
na watoto ulimwenguni. Mkutano umeandaliwa na asasi za serikali na
zisizo za kiserikali kukutanisha mataifa makubwa (yaani G8),
wachangiaji, wadhamini na watoaji misaada kwa lengo la kutokomeza njaa
na kusaidia kuwapatia kina mama na watoto lishe bora.
Baada
ya matembezi ndani ya ghala, SACOMA iliandaa kikao kifupi kuonyesha
namna na pia mazao gani huuzwa. Baadhi ya mazao yaliyowekwa mezani
kilipofanyika kikao ni pamoja na mahindi ya kuchemsha, ndizi kisukari,
juisi za matunda, viazi vitamu, maembe sindano na mboga maarufu ya
Sukumawiki ambayo hutumiwa zaidi Kenya. Sukuma Wiki (iliyo ndani ya
familia ya mboga za kabeji) huuzwa tayari imefungwa kwenye mifuko na
SACOMA.
Wakati
wa kikao hicho wazungumzaji wahusika walieleza namna ambavyo soko
litawafaidi wakulima , vijana na wafanyabiashara wa Tanzania hasa wale
wanaojituma.
Meneja Mwangalizi wa soko, Nigel Shepherd na Wana SACOMA walifafanua baadhi ya masharti yanayotakiwa kufikiwa kuleta bidhaa hizi sokoni. Mojawapo ni kuzingatia taratibu za uuzaji wa mazao uliowekwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU). Taratibu hizo ni mathalan upandaji mazao unavyofanywa kusudi umudu safari ya muda mrefu, hifadhi yake katika makasha ya baridi, usafi wa jumla, ufungaji na utangazaji (branding).
Kufuatana
na takwimu zilizotolewa na idara ya habari ya CNN mwaka jana, ingawa
uchumi wa Afrika unatazamiwa kukua kwa asilimia 4.5 idadi ya vijana
inatazamiwa kuongezeka mara mbili barani mwaka 2045. Leo asilimia 30 ya
vijana walio na umri kati ya miaka 18 hadi 29 hawana ajira katika jamii nyingi za Afrika.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia