LIPUMBA ASEMA DIRA YA MABADILIKO ITAONEKANA KWENYE KWENYE CHAGUZI ZA UDIWANI ARUSHA



Chama cha wananchi (CUF)kimesema dira ya mabadiliko ya kweli itaanzia kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata nne za jimbo la Arusha na kata nyingine zenye uchaguzi kama huo hapa nchini kwa kuendeleza kunadi sera za kuwaletea wananchi maendeleo badala ya kuhubiri vurugu na visasi.

Uchaguzi huu wa udiwani kwenye jimbo hili ndio dira ya kuelekea mabadiliko na kuonyesha je watanzania watajikomboa kwenye hali ngumu ya kimaisha kwani mtanzania anaishi maisha yake chini ya dola moja kwa sasa hali ni ngumu sote tumepigika na bakora za ccm.

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa chama hicho taifa prof;Ibrahim Lipumba kwenye muendelezo wa kampeni za chama hicho kuomba ridhaa ya wananchi kukichagua chama hicho kuweza kupata madiwani kwenye halmashauri ya jiji la Arusha.

Prof.Lipumba alisema kuwa uchumi imara huleta maendeleo kwa wananchi wa hali za chini kwani kijografia nchi hii inakubali mazao ya aina zote lakini kutokana na sera mbaya za ccm  ndio maana wananchi wamekuwa wakikosa chakula hadi kuletewa chakula cha msaada kwa madai ya mvua.

 Akawataka wanasiasa kunadi sera za vyama vyao badala ya kujenga chuki kwa wananchi ambazo zinachochea kuwagawa wananchi kiitikadi, kisiasa na kidini na huku hakutatufaisha badala yake kutabomoa umoja wetu na amani kwani mahala pasipo na amani hakuna maendeleo ya kiuchumi.

Ndugu zangu hapa Arusha ni jiji la kitalii na wageni huwa hawapendi mahala pa vurugu sasa hawa wenzetu wamekuwa wakihubiri vurugu hii itawafanya uchumi kuyumba na matokeo yake ni kukosa maendeleo na hivyo kuishi kwa kuomba omba hili ni tatizo kubwa hivyo nawataka kuangalia sera na watu wenye kuangalia matatizo yenu na kuona uchungu hawa wanapatikana kwenye chama cha wananchi.

“Sera nzuri za maendeleo zinapatikana kwenye chama cha wananchi(CUF)naombeni muwape ridhaa wagombea wa chama cha wananchi ili waingie Halmashauri kuwatetea na kuweza kuwaletea maendeleo kwani maendeleo hayaletwi na meya pekee bali na madiwani wote” alisema professor Lipumba.

Alisema kuwa kama kilimo kitatumika vizuri kitaweza kuwakomboa watanzania na kuondokana na kilimo cha mazoea cha adamu na hawa ambacho mkulima mdogo ataendelea kuwanufaisha wakulima wakubwa huku mkulima huyo akiendelea kubaki alipo na hizi ni sera za chama cha mapinduzi.

“Arusha mna madini,mbuga za wanyama na ardhi nzuri yenye rutuba sasa mnashindwaje kuwa na chakula hadi mletewe chakula cha msaada kwa madai ya uhaba wa mvua  tatizo hapa ni sera sio mvua inayowakosesha maendeleo”alisistiza Lipumba

Kwa upande wake mgombea wa chama hicho kwenye Kata ya Elerai John Gibert Bayo alisema kuwa akiingia halmashauri ataendeleza mambo yote aliyoyaanza kwani yeye hakuchaguliwa na mafuriko ya (CHADEMA) bali na wakazi wote waliokuwa wakiitakia mema kata hiyo ndio waliomuamini na kumpa kura hivyo siku ya uchaguzi muwaonyeshe kuwa nyinyi ndio mlioniyuma na si vingine.
Bayo alisema kuwa michango ya kuwaumiza wananchi ikiwemo ya ununuzi wa madawati na majembe kwa wanafunzi wa shule za sekondari hapa jijini kitakuwa ndio kipaumbele chake kwani majembe yanakwisha baada ya miaka minne huu ni wizi wa mchana kweupe ntapambana na kero hii.
Nawaomba mniunge mkono tarehe 16 niwe diwani wenu kwenda kuendeleza kazi niliyoanza kwenye halmashauri mbona waliponivua udiwani je walikuja kuwauliza watanivuaje bila ya kuja kuwaambia watu wa aina hii hawatufai hata kidogo hawakuwapa heshima na imani mliowapa muowanyeshe kuwa nyinyi ndio wenye maamuzi ya kumchagua diwani mnayemtaka.
“Mimi nimejiandaa kupokea matokeo yeyote kwani kuna msemo wa Kiswahili unaosema asiyekubali kushindwa si mshindani na nitaheshimu maamuzi ya wananchi wa Elerai”Bayo alisema hayo alipoulizwa na wanahabari atayapokeaje matokeo ya uchaguzi huo.
Uchaguzi mdogo wa marudio wa madiwani unafanyika siku ya jumapili kote nchini kwenye kata 26 na hapa Arusha unafanyika kwenye kata Tano za Kimandolu,Elerai,Kaloleni na Themi zote za jiji la Arusha huku Makuyuni ikiwa wilayani Monduli huku wagombea wa vyama vya CUF,CHADEMA,na chama cha Mapinduzi wakipigana vikumbo kuwania nafasi za uwakilishi wa wananchi kwenye halmashauri.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post