Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu akiwaonyesha waandishi wa habari
miwani yake aliyodai kuvunjiwa na polisi. Lissu alipata dhamana katika
Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati, jijini Arusha jana baada ya kukamatwa
juzi.
..............
Wabunge wanne wa Chadema, ambao waliachiwa
na polisi kwa dhamana wamesimulia mateso waliyoyapata wakiwa rumande
baada ya kukamatwa juzi.
Vigogo hao; Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi, Tundu Lissu
(Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti
maalumu), walikamatwa juzi baada ya wao na wafuasi wa chama hicho
kutawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi kwenye Viwanja vya Soweto,
Arusha.
Wabunge hao waliachiwa baada ya kujidhamini wenyewe huku watu wengine
65 waliokamatwa pamoja nao wakiachiwa baada ya kudhaminiwa.
Wote wanatakiwa kuripoti kwenye kituo hicho Julai 22, mwaka huu na wataelezwa hatma ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Operesheni wa
Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jeshi lake linaendelea kuwasaka
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha,
Godbless Lema na kuwaonya kuwa wanatakiwa kujisalimisha mara moja.
Chagonja alisema Mbowe na Lema wanatafutwa kwa kosa la
kufanyakusanyiko lisilo halali katika viwanja hivyo vya Soweto
walipokuwa wakitaka kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi,
Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki dunia baada ya kuumizwa kutokana
na mlipuko wa bomu, Jumamosi iliyopita.
Pia aliwaamuru Mbowe na Lema kuwasilisha mara moja ushahidi wa
kuwahusisha polisi na shambulio la bomu na kama hawana imani na Polisi,
basi wawasilishe ushahidi wao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Lissu
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, alilalamikia kitendo cha polisi kumwagia maji ya kuwasha baada
ya kumkamata.
“Walinimwagia maji ya kuwasha kwa mfululizo nikalazimika kulala chini
kifudifudi huku nikiwa nimefunika macho kukwepa yasiingie maji. “Kuna
askari walitaka kunipiga lakini niliokolewa na mwenzao mmoja
aliyenikinga nisishambuliwe. Kwa kweli ilikuwa hali ya hatari,” alisema.
Alisema polisi hao waliomkamata walivunja miwani yake kwa makusudi akisema aliikabidhi kaunta ikiwa haijavunjika.
“Wakati naingia mahabusu nilikabidhi miwani yangu lakini ajabu wakati
tukiachiwa ilikuwa imevunjika.” Alilalamikia hatua ya polisi
kuwashambulia kwa mabomu, kuwamwagia maji ya kuwasha walipokuwa
wakiwatawanya watu waliokusanyika Soweto akisema awali, waliwaruhusu.
“Kwa maoni yangu na maoni ya wenzangu, hakukuwa na sababu ya polisi
kupiga mabomu, risasi na kumwagia watu maji ya kuwasha kwani ni wao
ndiyo walituomba tubebe dhamana ya uongozi kwa kwenda kuwaomba wananchi
waliokusanyika pale uwanjani kutawanyika,” alisema Lissu.
Alisema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Gilles Mroto ndiye
aliyewaruhusu kuzungumza na wananchi ili watawanyike baada ya viwanja
hivyo kuzuiwa kutumika kwa shughuli ya kuaga miili ya waliopoteza maisha
kwenye tukio la bomu.
Alisema pamoja na ruhusa hiyo, polisi waliwaruhusu Chadema kuchukua
magari yao yenye vipaza sauti ili wavitumie kuwatawanya wananchi hao
lakini ajabu polisi ikawapiga mabomu mara baada ya Arfi kuwataka
wananchi watawanyike kwenda Hospitali ya Mount Meru kutoa heshima za
mwisho kwa marehemu.
“Kama ule mkusanyiko haukuwa halali, kwa nini polisi haohao walikaa
na wananchi wale tangu asubuhi na wakaturuhusu kuzungumza nao ili
watawanyike?”
Alisema kisheria, mkusanyiko usio halali unastahili kusambaratishwa
kwa mabomu baada ya polisi kutoa ilani kwa wahusika kutawanyika tofauti
na juzi akisema hawakutoa ilani yoyote.
Akunaay
Akunaay alisema polisi wanapaswa kubadilisha mbinu za kukabiliana na
watu wanaodhani wamevunja sheria badala ya kukimbilia kupiga mabomu na
kufyatua risasi.
“Mabomu na risasi ni kukomaza watu na kuwafanya wazoee milipuko.
Itafikia hatua wananchi watajenga usugu na kuanza kupambana na polisi,”
alisema na kuongeza:
“Polisi baada ya kutukamata na kutuweka chini ya ulinzi walitupiga
hadi tukiwa kituoni bila sababu yoyote. Nadhani askari wetu wanapaswa
kuacha kumalizia hasira zao za magumu yao yanayowakabili kwa kuwapiga
watuhumiwa.”
Mukya
Mukya amelalamikia kitendo cha polisi kukataa kumpa fursa ya
kumnyonyesha mtoto wake mchanga akisema malaika huyo alilazimika
kushinda njaa kutwa nzima ya juzi na usiku kucha.
“Niliwaomba polisi wanikubalie kujidhamini au wanisindikize
nikamnyonyeshe mtoto lakini walinikatalia kama vile ninakabiliwa na kesi
ya mauaji,” alisema Mukya.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyeki wa Baraza la Wanawake wa Chadema
(Bawacha), Susan Lyimo alisema: “Ni kinyume cha taratibu za haki za
binadamu kwa mwanamke kunyimwa nafasi ya kunyonyesha mtoto wake.”
Polisi wajibu
Akizungumzia malalamiko ya wabunge hao, Kamishna Chagonja alisema
hakuna mtuhumiwa ambaye anaweza kutoka mahabusu akaimwagia sifa kwa
sababu siyo mahali pa kusifiwa, bali ni mahali penye kizuizi cha muda
ili kuwezesha mkondo wa sheria kuchukua nafasi yake.
“Hatuna (polisi), roho ya Adolph Hitler (dikteta wa zamani wa
Ujerumani), tupo kwa ajili ya kulinda wananchi na mali zao,” alisema.
Aidha, alikanusha madai ya Mukya ya kunyimwa ruhusa ya kumnyonyesha
mwanaye akisema: “Siku hizi kuna dawati la jinsia katika vituo vyetu vya
polisi kwa hiyo kama ni kunyonyesha lazima wangesimamia utaratibu wa
kumwezesha kufanya hivyo, siyo kweli kwamba amekataliwa, haya ni maneno
ya kulichafua jeshi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema
wanaojihusisha na uhalifu wowote huwa na imani kuwa watafanikiwa
kujificha au kukwepa mkono wa dola na inapotokea wamekamatwa na
kuchukuliwa hatua, huanza kujitetea kwa kuwashushia lawama polisi.
“Hasa wanasiasa na wanaharakati wakikamatwa na kuwekwa rumande, wengi
hutoa manung’uniko mengi yakiwamo ya uongo, ilimradi kuchafua polisi
mbele ya wananchi . Hatupo kwa ajili ya kusifiwa, bali kutimiza wajibu
wetu,” alisema Sabas.
Kifo chaongezeka
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mlipuko huo imefikia
wanne baada ya mtoto Fahad Jamal (7), aliyekuwa amelazwa katika
Hospitali ya Seliani kufariki dunia jana. Kaimu Mkurugenzi wa hospitali
hiyo, Paul Kisanga alithibitisha jana kufariki kwa majeruhi huyo
aliyekuwa ameumia kichwani na kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa wenye
kuhitaji uangalizi maalumu (ICU).
Mmoja kuagwa leo
Kiongozi wa Chadema, Judith Moshi aliyefariki kwenye tukio hilo la
bomu, leo anatarajiwa kuagwa kwa heshima zote za chama hicho katika moja
ya makanisa jijini Arusha baada ya polisi kukizuia chama hicho
kuendesha shughuli hiyo katika eneo la wazi.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema
baada ya kuagwa, marehemu Moshi atazikwa Arusha badala ya kusafirishwa
kwenda mkoani Kilimanjaro kama ilivyokuwa imepangwa awali ili kutoa
fursa kwa wananchi wa jiji hilo kushiriki katika mazishi yake.
“Kanisa gani na makaburi yapi tutamuagia na kumzika marehemu,
tutatangaza baadaye au kesho asubuhi baada ya mashauriano kati ya
viongozi na ndugu wa marehemu ambaye atazikwa kwa heshima zote za
chama,” alisema Mnyika.
Awali, marehemu Moshi alitarajiwa kuagwa kwenye Viwanja vya Soweto
kabla ya kusafirishwa kwenda Kilimanjaro lakini Jeshi la Polisi lilizuia
shughuli hiyo kufanyika kwenye viwanja hivyo baada ya kupokea maelekezo
kutoka kwa wamiliki wake ambao ni Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
Arusha (AICC).