CHAMA CHA MAPINDUZI CHATOA OVYO KWA MGOMBEA WAKE WA ARUMERU

CHAMA cha mapinduzi (CCM)wilayani Arumeru,mkoani Arusha,kimempa karipio kali mgombea wake,Sioi Sumari ambaye ni mtoto wa marehemu ,Jeremia Sumary kwa hatua yake ya kuanza kucheza rafu kwa kumwaga fedha jimboni huo kwa lengo la kujiwekea mazingira mazuri ya kuteuliwa  .
Aidha CCM inamtuhumu mgombea huyo kujipitisha  majumbani kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya wenye dhamana ya kupitisha jina moja la mgombea kwa kuwamwagia fedha ili kuwashawishi kupitisha jina lake.
Katika kinyangányiro cha kuwania uteuzi wa kugombea katika jimbo la Arumeru mashariki lililoachwa wazi kufuatia kifo cha mbunge wake ,Jeremia Sumari,na tayari ccm imeiomba taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wilayani humo,TAKUKURU kumchunguza.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Katibu  mkuu wa  ccm wilaya ya Arumeru,Edson Lihweuli alisema kuwa ofisi yake ilifikia hatua hiyo ya kwa kumwita ofisini na kumpa karipio kali baada ya kuwepo taarifa kuwa, Sumary amekuwa akicheza rafu kwa kumwaga fedha kwa wajumbe hao ili kujitengenezea  mazingira ya kuchaguiliwa.
Lihweuli alifafanua  kuwa chama cha mapinduzi hakita mwonea haya mgombea yoyote wa chama hicho, atakayeonekana kwenda kinyume na taràtibu za cha chama ,na  kwamba iwapo itabainika kwa mgombea yoyote  hatua kali zitachukuliwa ,ikiwa ni pamoja na kuliengua jina lake .
‘’CCM awamu hii hatutaki aibu kabisa kama mtu anawashwa na fedha zake ni bora azipeleke  kwa wenye uhitaji wa kusaidiwa hasa watoto yatima na wasiojiweza,ikibainika mgombea wetu amecheza rafu tunaengua jina lake mara moja’’alisema Lihweuli.
Aidha,ametumia fulsa hiyo kuiomba taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa mkoani Arusha,TAKUKURU kuhakikisha inajipanga vyema katika uchaguzi huo mdogo, kukabiliana na vitendo vya utoaji rushwa vinavyofanywa na wagombea wenye uchu wa kuhitaji  madaraka kwa nguvu ya  fedha .
 Ameiomba  TAKUKURU kuhakikisha inakuwa karibu  na wagombea wote wa ccm waliotangaza nia ya kuwania kinyangányiro cha kuteuliwa  kugombea katika jimbo hilo lililoachwa wazi kufuatia kifo cha mbunge wake ,Jeremia Sumari ,ambapo wagombea zaidi ya watano wa ccm wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania kiti hicho.
‘’sisi ccm hatuna uwezo wa kujua jinsi mgombea wetu anavyotoa rushwa ila hawa takukuru wanautaalamu wa kujua na kuwawekea mitego,tunawaomba sana waje wawe karibu na wagombea wetu ili watuisaidie ,tumepata malalamiko kuwa baadhi ya wagombea wetu wameanza mchezo mchafu‘’alisema Lihweuli
Aliwataka wagombea wote wa ccm kuacha chuki binafsi za kuchukiana na badala yake wapendane ili pindi mmoja wapo atakapoibuka kidedea  katika jimbo hilo,wengine wamuunge mkono na kuacha kuendeleaza makundi ya kumpinga ama kukimbilia vyama vingine vya upinzani.
CCM inatarajiwa kufanya uteuzi wa mwakilishi wake siku ya jumatatu,  februari 20 mwaka huu katika ukumbi wa fikiri kwanza uliopo Usa River wilayani humo ,ambapo  hadi jana wagombea wane kati ya sita walikuwa wamechukua fomu ,walirudisha.
Wagombea waliojitokeza kuchukua fomu hadi sasa ni pamoja na ,William Sarakikya,Sioi Sumari,Elishiria Kaaya ,Elirehema Kaaya ,Rishiankira Urio na Anthony Musani.
               habari hii imeandikwa na Josephy Ngilisho wa Libeneke la Kaskazini 

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post