Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS AKABIDHI MSAADA WA NGOMBE KWA WATU JAMII YA WAMASAI MKOANI ARUSHA



 Hapa anawasalimia malaigwanani wa longido
 akiwa amekaa kwenye kiti cha kimasai cha asili kijulikanacho kwa jina la kimasai Lorika huku akiwa amevishwa shuka ya kimasai na fimbo

Hizi ni baadhi ya picha za sherehe ya kukabidhi ngombe kwa jamii ya wamasai ngombe waliokufa wakati wa ukame makabidhiano hayo yalifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Kikwete




RAIS Jakaya Kikwete  alizindua mradi wa uwezeshaji wafugaji wa wilaya tatu za Mkoa wa Arusha ikiwa ni kifuta jasho cha ukame uliozikumba kaya za wilaya hizo mwaka 2008 na 2009.

Wilaya zilizonufaika na mradi huo ni Longido, Monduli na Ngorongoro. Mradi huo umegharimu zaidi ya Sh bilioni 11.2 kwa wilaya hizo zilizokumbwa na ukame mkubwa uliofanya mifugo mingi kufa katika miaka hiyo hasa Wilaya ya Longido yenye tarafa nne za Ketumbeine, Enduimemet, Longido na Engaranaibor.


Kabla ya ukame huo, Longido ilikuwa na mifugo 1,016,313 na baada ya ukame, ilibakiwa na mifugo 555,613.


Katika sherehe zilizofanyika jana wilayani Longido na kuhudhuriwa na mamia ya watu, Rais Kikwete alisema alipotembelea wilaya hiyo Agosti 23, 2009, alijionea mwenyewe hali mbaya ya ukame iliyosababisha maisha ya watu wa wilaya kuwa magumu kwani asilimia 95 ya wakazi wa wilaya hiyo hutegemea mifugo.


Alisema, kutokana na hali hiyo, yeye na Serikali yake walibuni mradi wa kuwasaidia wakazi wa wilaya hizo kwa kuwaanzishia mradi wa ufugaji wa kisasa kwa kuwanunulia mifugo kama kifuta jasho cha kuanza upya maisha ya kifugaji.


Alisema, aliona suala muhimu kwa yeye na Serikali yake ni kutoa mifugo kwa wakazi walioathirika sana na ukame kwani Masai ni ng’ombe na ng’ombe ni Masai, kwa hiyo moja ya ahadi ya kuwasaidia Wamasai wakati wa kampeni ya Uchaguzi Mkuu anaitekeleza sasa.


Alisema, kuchelewa kufanyika kwa mradi huo ni kutaka kupata tathimini ya uhakika ya watu walioathirika katika ukame huo kwa majina na ndio maana tathimini hiyo ilimalizika mwaka juzi.


Rais alianza kwa kutoa ng’ombe 500 na mbuzi 30 kwa kaya 16 zenye vijiji 41 za Wilaya ya Longido ambazo kwa kiasi kikubwa ziliathirika sana na ukame wa miaka hiyo ikiwa ni njia ya kuzindua rasmi mradi huo wa kifuta jasho kwa wafugaji wa wilaya hizo.


Katika hatua ya pili, Rais Kikwete ametoa jukumu hilo kwa halmashauri za wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro kusimamia zoezi hilo kwa kutangaza zabuni kwa kaya zilizoathirika na ukame.


Alisema yeye na Serikali yake watakuwa wakitoa fedha kwa kampuni itakayopata zabuni hiyo kwa kusambaza mifugo aina ya ng’ombe na mbuzi kwa kaya zilizoathirika na ukame.


“Nataka halmashauri za Longido, Monduli na Ngorongoro kusimamia kikamilifu zoezi hilo kwa kupata mzabuni wa uhakika wa kufanya kazi hiyo kwa kutafuta ng’ombe na mbuzi wazuri na Serikali itakuwa ikitoa fedha tu nataka zoezi hilo lifanyike kwa umakini na uhakika,” alisema Rais Kikwete.


Rais aliwataka wananchi wa wilaya hizo kutoka katika ufugaji wa asili na kufuga kisasa zaidi kwani ukame uliowakuta kama wangefuga kisasa, usingewaathiri sana.


Akizungumzia kilio cha kutopatikana kwa maji ya uhakika katika wilaya hiyo, Rais Kikwete alisema suala hilo atalishughulikia kwa kuelekeza wizara husika kwani hatawaangusha kwani ahadi nyingi alizoahidi alizitekeleza kama vile umeme kutoka Namanga nchini Kenya na Barabara ya Arusha hadi Namanga.


Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema, awamu ya kwanza itakuwa kwa Wilaya ya Longido na awamu ya pili kwa Monduli na kumalizia Ngorongoro.


Lukuvi alisema kaya 6,167, vijiji vyote 111 katika wilaya hizo tatu ziliathirika, zitapa ng’ombe watano na mitamba wanne. Alisema kaya 2,852 za Wilaya ya Longido ndizo ziliathirika zaidi kwa ukame kwa vijiji vyote 41 vya wilaya hiyo na kila kaya itapata mitamba wanne na dume mmoja.

 





Post a Comment

0 Comments