BREAKING NEWS

Tuesday, February 7, 2012

SIMANJIRO WAKABILIWA NA UKAME

HALI ya ukame uliosababishwa na kutokunyesha mvua kwa muda mrefu Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,kumewaathiri kwa kiasi kikubwa wafugaji wa wilaya hiyo hadi kusababisha baadhi yao kuhama kwenye vijiji vyao.

Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya maadhimisho ya sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Februari 5 yaliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Landanai Kata ya Naberera wilayani Simanjiro mbele ya mgeni rasmi Mlezi wa CCM wa mkoa huo,Mohamed Seif Khatibu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uzini,Mbunge wa jimbo la Simanjiro Christoper Olonyokie Olonyori Ole Sendeka amesema hivi sasa mifugo yao ina wakati mgumu kutokana na hali ya ukame uliyopo wilayani humo.

Ole Sendeka amesema kutokana na hali hiyo halmashauri ya wilaya ya Simanjiro imetenga fedha kwa ajili ya kuchimba visima viwili kwenye kata ya Naberera na kisima kimoja kitachimbwa kwenye kijiji cha Landanai ili kuwapatia wafugaji maji.

Ameongeza kuwa pamoja na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji wilayani humo lakini hata hivo kuna baadhi ya mafanikio waliyoyapta wilayani humo tangu Serikali ya awamu ya nne iingie madarakani ikiwemo kuongeza shule za sekondari kutoka tatu changa hadi 16.

"Pia kiwango cha wanafunzi kufaulu kimepanda kutoka wanafunzi 180 hadi 2,700 kwa mwaka na zahanati na vituo vya afya vingi vimejengwa pamoja na visima vya maji na umeme ulikuwa haupo makao makuu ya wilaya hiyo hivi sasa upo," alisema Ole Sendeka.

Kwa upande wake,mgeni rasmi wa maadhimisho hayo,Mohamed Seif Khatib amesema tangu CCM izaliwe imefanya mambo mengi mazuri ikiwemo kupatikana kwa elimu bora,maji,kilimo  na ufugaji pamoja na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Khatib ameongeza kuwa kupitia chama hicho Tanzania imefanikiwa kupata Katiba yake mwaka 1977 huku mchakato wa kupatikana katiba mpya ukiendelea na demokrasia nchini imeongezeka hivi sasa kwani kuna vyama vingi.

Mlezi huyo wa CCM mkoani ManyarAmedai kuwa CCM imezaliwa na vyama vya TANU na ASP hivyo vina wazazi lakini vyama vingine ni wana haramu kwani havina wazazi.

Aidha,Sherehe hizo zimehudhuriwa na mkuu wa mkoa huo Elaston John Mbwilo,wakuu wa wilaya za Simanjiro Khalid Mandia na Mbulu Anatory Choya,Mwenyekiti wa CCM mkoani Manyara,Lucas Ole Mukusi wenyeviti na makatibu wote wa CCM wa wilaya zote za mkoa huo,pia wenyeviti wastaafu wa wilaya walipatiwa vyeti.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates