KAMATI kuu ya chama
cha mapinduzi kwa kuamua kurejesha majina ya Wiliamu Sarakikya na Siyoi
Sumari kwa lengo la kupigiwa upya kura
na wana ccm ili kupata mgombea ubunge wa ccm katika jimbo la Arumeru mashariki
kumerejesha mtifuano ndani ya chama hicho kwa makundi hasimu mkoani Arusha.
Makundi hayo hasimu ni yale ya wanaotajwa kuwa na nia ya
kugombea urais mwaka 2015 ambapo Arusha imekua kama
kitovu kikuu cha kujipanga ndani ya ccm kwa wagombea hao kuwa na kambi rasmi.
Awali kabla ya kumalizika kwa kura za maoni ambazo
zilishirikisha wagombea 6 kuwania kuteuliwa na chama hicho tayari kuliisha kua
na dhana ya makundi hayo na yakimuhusisha Siyoi Sumari kwa upande mmoja na mkurugenzi wa AICC
Elishilia Kaaya kwa upande wa pili.
Siyoi alikuwa akitajwa kuwa anawakilisha kundi la Mbunge wa
Monduli Edward Lowasa huku Kaaya akitajwa kuwakilisha kundi la Bernad Membe
katika uchaguzi huo huku akiungwa mkono na baadhi ya viongozi wa chama na
serikali ngazi ya mkoa wa Arusha.
Kufuatia hali hiyo kundi kubwa la Vijana wa Arumeru
wakiungwa mkono na umoja wa vijana mkoa walilazimika kufanya kampeni kali
kuhakikisha Kaaya hachomozi katika uchaguzi huo kwa kuwa tayari alikua hana
mahusiano mazuri na kambi za vijana mkoani Arusha.
Hali hiyo ilipelekea kushika nafasi ya nne licha ya kuwa ni
maarufu katika jimbo hilo la Meru akizidiwa hata
na Elirehema Kaaya ambae ni katibu mweenezi wa ccm Wilaya ya Nyamagana mkoani
Mwanza na hivyo kuacha makundi ya vijana yakishinda kampeni yao ya kumuangusha.
Toka kutangazwa kwa matokeo hayo ya awali tayari kampeni
zilianza za chini kwa chini kwa baadhi ya makundi kuungana kwa lengo la
kuhakikisha wanashughulikiana na habari za ndani ya makundi hayo zikasema kuwa
tayari kundi la Elishilia Kaaya na baadhi ya viongozi wa mkoa lilijiunga katika
kambi ya Sarakikya.
Kujiunga kwa kundi hilo kwa Sarakikya kunasemekana
kunatokana na mahusiano ya wazi yaliyopo baina ya Siyoi Sumari na kundi linalotajwa kumuunga mkono
Lowasa na hivyo kundi la Shilia linaloaminika kuunga mkono kambi ya Bernadi
Membe kuamua kuunganisha nguvu kwa Sarakikya ili kuhakikisha wanapata ushindi.
Makundi haya mawili kwa hivi sasa yamewagawa vijana wa
Arumeru kwa kiasi kikubwa kutokana toka awali kila mmoja alikua na kundi la
vijana linalomuunga mkono hivyo hivi sasa Sayakikya kupata kuungwa mkono na
kundi la Elishilia Kaaya huku kukiwa na taarifa za ndani kuwa kundi la
Elirehema nalo likihusishwa kuungana na kundi la Siyoi.
Kwa mtazamo huo mchuano huu wa marudio baina ya Sarakikya na
Sumari unaweza ukatafsiri kwamba sasa unataka kudhihirisha ni kundi gani lenye
nguvu katika mkoa wa Arusha baina ya makundi mawili yanayotajwa kuwa ngome za
wanaotajwa kuwa katika mbio za urais 2015,Bernadi Membe na Edward Lowasa.
Ukiangalia kura za awali walizopata katika uchaguzi
uliokwisha Siyoi Sumari alipata kura 361 na Sarakikya akipata kura 259 huku
Elirehema akipata kura 205 na Elishilia akipata kura 176 na ukiunganisha
makundi hayo ambayo yameungana la Siyoi na Elirehema utapata kura 566 na la
kaaya na Elishilia utapata kura 435 na kwa idadi ya wajumbe waliopiga kura 1034 utakuta Siyoi anamatumaini ya kushinda.
Hali hiyo hivi sasa inafanya mchuano kuwa mkali kwa kambi ya
Sarakikya kuhakikisha inaligawa kundi la Elirehema ili ipate baadhi ya wajumbe
watakaomuunga mkono na hivyo kuibuka mshindi kwa kupata kura zaidi ya nusu ya
wajumbe.
Na mchuano huo hivi sasa umegeuka kuwa kati ya viongozi wa
chama ngazi ya mkoa dhidi ya viongozi wa umoja wa vijana ngazi ya mkoa ambao
kwa muda mrefu sasa wamekua katika kambi tofauti katika harakati za kuunga
mkono makundi ya wanaotajwa kuwania urais 2015.