WAHAIDI KUCHUKUWA JIMBO


MBUNGE wa Jimbo la Uzini visiwani Zanzibar,Mohamed Seifa Khatib amesema CCM ina uhakika wa kushinda uchaguzi mdogo wa kumchagua Mwakilishi wa jimbo hilo kwenye Baraza la Wawakilishi,unaotarajia kufanyika jumapili ijayo.

Khatib ambaye pia ni mlezi wa CCM wa mkoa wa Manyara,aliyasema hayo juzi kwenye maadhimisho ya sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa CCM yaliyofanyika kimkoa katika kijij cha Landanai kata ya Naberera wilayani Simanjiro.

Alisema mgombea uwakilishi kupitia CCM,Mohamed Raza ana uhakika wa kushinda kiti hicho kwa asilimia kubwa kwani kwenye Jimbo hilo CCM inakubalika zaidi na yeye huwa anapata ushindi hapo kwa zaidi ya asilimia 95. 

“Kuna vyama vitano vilivyoweka wagombea wao kwenye uchaguzi huo ikiwemo CCM,CUF,Chadema na TLP lakini kati ya vyama vyote vinavyogombea ni CCM peke yake ndiyo ina uhakika wa kutwaa ushindi wa jimbo hilo,” alisema Khatib.

Alisema chama hicho bado kina mvuto kwa jamii kutokana na kuwa na umoja,mshikamano na huwa wanakosoana ndani ya vikao vyao pale mmoja wao anapokosea kwa kuambiwa ukweli naye kuomba msamaha.

“Sisi huwa tunakosoana siyo kama vyama vya upinzani vurugu tupu juzi tu hapa Maalim Seif Sharif wa CUF,amemfukuza mwenzake Hamad Rashid kwa sababu anataka kugombea nafasi aliyonayo Seif ya ukatibu mkuu,” alisema Khatib.

Kwa upande wake,Mbunge wa jimbo hilo Christopher Ole Sendeka alisema Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema bila CCM imara nchi itayumba hivyo viongozi wa CCM wanatakiwa kuwa waadilifu ili chama hicho kizidi kuongoza nchi ipasavyo.

Ole Sendeka alisema hivi sasa chama hicho kinaelekea kufanya uchaguzi mkuu na kwenye jumuiya zake na wanachama wake wanatakiwa wasimame kidete ili kuhakikisha wanawachagua viongozi walio makini na wenye uadilifu.

Naye,Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo,Lucas Ole Mukusi alisema changamoto za leo ndiyo fursa za kesho hivyo viongozi wanatakiwa kuzitatua changamoto zilizopo ili wananchi wasizione kuwa ni kero.

Ole Mukusi alisema viongozi wa CCM wanatakiwa kuisimamia Serikali iliyopo madarakani ili kuhakikisha inatekeleza ahadi zote zilizotolewa kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005 hadi 2015.



Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post