Wachimbaji wadogo wa madini ya
Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,wameiomba
Serikali kuipatia kibali kampuni ya kizalendo ya Tan Youth Mining Ltd,ili
wauziwe zana za milipuko kwa bei nafuu.
Wachimbaji hao wakizungumza juzi
mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Kaimu
Mwenyekiti wake Anne Kilango Malecela walisema kampuni hiyo ikipatiwa kibali na
kufutiwa kodi watachimba madini kwa urahisi.
Mmoja kati ya wachimbaji wa
madini,Abubakary Madiwa alisema kampuni hiyo chini ya Mkurugenzi wake,Mohamed
Karia ingepatiwa kibali cha kuwasambazia wachimbaji wadogo zana za milipuko
wangekuwa na unafuu mkubwa.
“Kampuni ya kutoka nje ya nchi ya South
Africa,inatuuzia zana za milipuko kwa bei ghali hivyo tunaomba kampuni ya
kizalendo ya Tan Youth Mining Ltd kupitia Mkurugenzi wake Karia ipewe kibali
atuuzie kwa bei nafuu,” alisema Madiwa.
Hata hivyo,Kamishna Msaidizi wa
madini kanda ya kaskazini,Benjamin Mchwampaka aliieleza Kamati hiyo kuwa
alishaidhinisha kampuni ya Tan Youth Mining,ipatiwe kibali hicho ila
kinachokwamisha ni makao makuu wizarani.
“Kampuni hiyo ingeweza kuwasaidia
wachimbaji wadogo kwa suala la milipuko na nilishasaini yote yanayonihusu,ila
wizarani bado hawajasaini na alishahojiwa mpaka na kamati ya ulinzi na usalama
ya mkoa,” alisema Mchwampaka.
Akizungumzia kuhusu hilo,Kaimu
Mwenyekiti wa kamati hiyo,Anne Kilango Malecela aliwataka wachimbaji hao
kuandika barua kwenye kamati hiyo wakutane na wizara mwezi ujao ili kampuni
hiyo ipatiwe kibali hicho.
“Kama mnaona kampuni hiyo ya
kizalendo, itawanufaisha wachimbaji wadogo kwa kuwezesha upatikanaji na unafuu
wa bei ya zana za milipuko andikeni barua sisi tutawasaidia kwa kuwakutanisha
na wizara,” alisema Malecela.