KIKWETE ALONGA KUHUSIANA NA ASKARI SABA WALIOWAWA DARFUR
Kwa hakika, Rais amesikitishwa sana
na kitendo hicho ambako wanajeshi wengine 14 wa Tanzania wamejeruhiwa na waasi
wa Sudan na ametuma salamu za rambirambi za moyoni mwake kwa Jeshi la Wananchi
wa Tanzania na kwa familia za wafiwa wote.
Aidha, Rais Kikwete anaungana na
Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na familia za wafiwa
kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa Tanzania. Rais pia anaungana na
Watanzania wote kuwaombea wale walioumia katika tukio hilo waweze kupona haraka
na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Katika salamu zake za rambirambi kwa
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Adolf Mwamunynge na familia za
wafiwa, Rais Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu amesema:
“Sina maneno ya kutosha ya kuelezea
mshtuko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo vya vijana wetu hao
ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa
majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia
ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na
waassi.”
Rais Kikwete ameongeza kumwambia
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na familia za wafiwa ”Napenda kwa niaba ya Watanzania
wenzangu niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea
walipokwenda Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania
ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri
sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi
yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi yao.”
Amesisitiza Mheshimiwa Rais Kikwete:
“Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo
wangu kuomboleza vijana wetu hawa. Kupitia kwao, natuma salamu za rambirambi
kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na wapigaji wote wa Jeshi letu kwa
kupotelewa na wenzao. “
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia