HATIMA ya
kesi ya ugaidi inayowakabili makada watano wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), sasa ipo mikononi mwa Mahakama Kuu baada ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora ilikofunguliwa kusema haina uwezo wa
kusikiliza kesi ya ugaidi.
Wakati
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Tabora, Issa Magoli, akiisukumia Mahakama
Kuu kesi hiyo, wakili wa watuhumiwa hao, Peter Kibatala, aliliambia
Tanzania Daima kuwa wameshafanya utaratibu wa kupeleka shauri lao
Mahakama Kuu baada ya kupewa nakala ya uamuzi huo.
Makada hao
wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi ni Katibu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Henry Kilewo, Evodius Justinian, Oscar Kaijage , Seif Kabuta na
Rajab Daniel, wanaotuhumiwa kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha,
katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mwaka 2011.
Akitoa
uamuzi huo jana, Hakimu Magoli alisema mahakama hiyo haina uwezo
kisheria kusikiliza kesi hiyo, hivyo akaiahirisha kesi hiyo hadi Julai
22, mwaka huu.
Hakimu
Magoli kabla ya kuahirisha shauri hilo aliwashauri mawakili wa upande wa
utetezi wawasilishe hoja zao Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo watapatiwa
ufumbuzi wa kisheria.
Akizungumza
kwa simu na gazeti hili, wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala, saa
chache baada ya uamuzi huo, alisema wameshapeleka Mahakama Kuu Kanda ya
Tabora maombi kwa hati ya dharura ya kutaka iipitie upya kesi hiyo ya
ugaidi.
Aliongeza
kuwa maombi hayo yamepokewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na
wanasubiri kupangiwa tarehe nyingine na Mahakama Kuu ili kesi hiyo
isikilizwe.
Alisema
katika maombi yao wameomba Mahakama Kuu ipitie shauri hilo, pia kuona
kama ni halali kisheria kwa washtakiwa hao kufunguliwa kesi hiyo baada
ya awali watuhumiwa wanne (isipokuwa Kilewo), mashtaka yao yaliondolewa
na kisha kukamatwa na kufunguliwa mashitaka mapya.
Kwa mara ya
kwanza watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi Juni 24, mwaka huu,
wakidaiwa walimteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha,
katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Awali kabla
ya kusomewa shitaka la ugaidi ambalo kwa sasa mahakama inasema haina
uwezo wa kusikiliza, mwanzoni walifunguliwa shitaka la kushambulia na
kudhuru mwili, ambapo Mahakama ya Wilaya ya Igunga iliwaona hawana
hatia, hivyo kuwaachia huru lakini walikamatwa tena.
Kesi hiyo
ilisikilizwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mjini.
Jocktan Rushwera, ndiye aliyesikiliza hoja za mawakili wa utetezi,
waliomtaka kuifuta kesi hiyo. Hata hivyo haijulikani kwanini kesi
ilisikilizwa halafu baada ya kubadilisha hakimu, kwa kesi hiyo hiyo
mwingine akasema mahakama hiyo haina uwezo wa kuisikiliza.
Upande wa serikali uliwakilishwa na Wakili Juma Massanja na Ildefons Mukandara.
Awali
watuhumiwa hao waliposomewa shitaka, jopo la mawakili wa utetezi,
Abdalah Safari na Peter Kibatala, liliomba mahakama hiyo iyafute
mashitaka hayo kwa sababu ya kutokuwa na uhai.
Mawakili hao
wa utetezi walidai kuwa mashitaka hayo hayana uhai kwa sababu
yamefunguliwa bila ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Pia mawakili
hao walidai kuwa sheria za uendeshaji wa makosa kama hayo hapa nchini
zinadai kuwa mashitaka kama hayo yanapofunguliwa ni lazima ridhaa ya DPP
iwepo, lakini ridhaa hiyo haipo, hivyo yatupwe.
Waliongeza
sababu ya pili kuwa maelezo hayaoneshi kosa husika ni la kigaidi,
tofauti na makosa mengine ya kawaida kwa mujibu wa sheria za Tanzania,
hivyo waliomba yafutwe au yafunguliwe kama kosa la kawaida.
Upande huo
wa utetezi pia ulidai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai,
inaelekeza kuwa mshitakiwa ashitakiwe katika mahakama yenye mamlaka na
hadhi kama ile waliyopelekwa katika maeneo yale walikokamatwa.
Hivyo
mawakili waliiomba mahakama itupilie mbali shitaka, kwani washitakiwa
kama walikuwa na hatia walipaswa kushitakiwa katika maeneo yao
walipokamatwa.
Upelelezi wa Lwakatare bado
Wakati huo
huo, mkoani Dar es Salaam, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha
kesi ya kula njama na kutaka kumuua kwa sumu Mhariri Mtendaji wa gazeti
la Mwananchi, Denis Msacky, inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Wilfred Lwakatare na
Ludovick Joseph.
Hakimu Mkazi, Alocye, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, mwaka huu kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Ponsia Lukosi, aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Lwakatare
yupo nje kwa dhamana, Ludovick bado yupo gerezani baada ya kushindwa
kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni mshitakiwa kuwa na wadhamini
wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika kisheria ambapo kila mdhamini
atatakiwa asaini bondi ya sh milioni 10 pamoja na washitakiwa wenyewe.
Pia
mshitakiwa anatakiwa kusalimisha hati yake ya kusafiria mahakamani na
kutotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama.
Taarifa hii imeandaliwa na Happiness Katabazi (Dar), Thomas Murugwa na Josephat Isango (Tabora).