WAZEE WASEMEWA NA LOWASA
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu
Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa akizungumza wakati wa majadilino yaliyohusu
namna ya kuingiza suala la wazee katika ajenda mpya za Maendeleo baada
ya mwaka 2015. Mkutano huo ulioambatana na chakula cha mchana ulifanyika
siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na ulioandaliwa
na United Nations Foundation kwa kushirikiana na Mashirika mengine ya
Kimataifa. katika mchango wake, Mhe. Lowassa amesisitiza umuhimu wa ubia
kati ya serikali na sekta binafsi katika kuzikabili changamoto za
ongezeko la idadi ya wazee duniani. Inasemekana miaka michache ijayo
idadi ya wazee duniani itazidi idadi ya watoto wadogo chini ya miaka
mitano. Pamoja na Mhe. Lowassa wengine waliochangia majadiliano hayo ni
Bi. Ann Pawliczko kutoka UNFPA wa pili kutoka kushoto, Bw. Jack T.
Watters kutoka Pfizer, Bw. Paul Ong HelpAge International, Bw. Sharig
Khoja kutoka United Nations Foundation, aliyeketi karibu na Mhe. Lowassa
ni Bi. Jane Barratt aliyeratibu majadiliano hayo.
Mhe.
Lowassa akipeana mkono na mmoja wa waandaji wa majadiliano hayo kuhusu
Wazee, takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (
UNFPA) zinazonyesha kwamba mwaka 1950 idadi ya wazee duniani waliokuwa
na miaka 60 au kuzidi ilikuwa milioni 205, 2012 idadi hiyo iliongezeka
hadi kufikia 810 milioni. Inakadiriwa kwamba idadi hiyo itaongezeka hadi
kufikia Bilioni 1 si zaidi ya miaka kumi ijayo na ifikapo mwaka 2050
idadi ya wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea itafikia bilioni 2.
Aidha duniani kote wanawake ndio wanaokadiriwa kuishi umri mrefu zaidi
kuliko wanaume.
Sehemu ya washiriki wa majadiliano hayo wakiwamo pia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa.
Mhe. Edward Lowassa akibadilishana mawazo na Balozi wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa, Bw. Chitsaka Chipaziwa.
Mh. Lowasa akiwa na mmoja wa washiriki wa majadiliano kuhusu mstakabali wa wazee.
Na Mwandishi Maalum
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu
Mstaafu Mhe. Edward Lowassa ( Mb) amesisitiza haja na umuhimu wa kuwapo
kwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika kuzikabili changamoto
zinazotokana na ongezeko kubwa la idadi ya wazee.
“
Maisha Zaidi ya miaka 60 hayapashwi kuwa ya utegemezi, unyonge,
kutojiweza au kutokuwa na matumaini. Wazee bado na wanao mchango
mkubwa ndani ya jumuiya, jamii, na familia zao ili mradi tu
wawezeshwe”.
Na kwa
sababu hiyo anasema Mhe, Lowassa, juhudi mbalimbali zinazofanywa na
serikali katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea Tanzania ikiwamo za
utoaji wa huduma za msingi kama vile Afya , pensheni na uwezeshwaji
zinapashwa kuchagizwa na sekta binafsi.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mambo ya Nje, na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward
Lowassa(Mb ), ameyasema hayo siku ya jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja
wa Mataifa wakati aliposhiriki majadiliano kuhusu namna gani suala la
Wazee linavyoweza kuingizwa katika ajenda za maendeleo baada ya mwaka
2015.
Majadiliano
hayo yaliandaliwa na United Nations Foundation kwa ubia na
International Federation of Ageing, Help Age International, AARP,
Global Coalition on Aging, mHealth Alliance na Pfizer
“Kama
kundi hili la wazee likiwezeshwa na kusaidiwa ipasavyo , linaweza
kuipatia jamii soko jipya, ujasiriamali, utoaji wa maamuzi, utoaji wa
huduma na utalaamu anuai katika maeneo ya sayansi, teknolojia na
upatanishi” anasema Lowassa.
Na
kuongeza, ili hayo yote na mengine mengi yaweze kufanikiwa panahitajika
bajeti ya kutosha kwa ajili ya kundi hilo la jamii ikiwa ni pamoja na
kuimarisha mifumo ya pensheni, huduma za afya ambazo zitakidhi mahitaji
ya wazee, huduma za kisaikolojia na huduma za ulinzi jamii.
Hata
hivyo anasema, inasikitisha kwamba, katika nchi nyingi za Afrika na
nyinginezo hata zile zilizoendelea bado haziwezi kutoa huduma za
uhakika na zenye viwango vya kukidhi mahitajio ya wazee.
“Mara
nyingi huduma kwaajili ya wazee inabidi zishindane na huduma za makundi
mengine kama vile ongezeko la vijana wasiokuwa na ajira, upunguzaji
wa vifo vya watoto wachanga na wanawake wajawazito. Hata hivyo pamoja
na changamoto zote hizi za vipaumbele hatuwezi kuendelea na utaratibu
huu wa kuchagua. Lazima tutumie maandalizi ya ajenda za maendeleo baada
ya 2015 kuwahudumia wazee” anasisitiza Lowassa.
Akasema
Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kujikumbusha na kujifunza kwa kosa la
kutoingiza suala la Wazee katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya
Millenia ( MDGs) yanayoelekea ukingoni, kwa kuhakikisha kwamba Wazee
wanaingizwa katika malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015 kwa kuwa
ni suala ambalo haliepukiki.
Akizungumzia
hatua mbalimbali zinazochuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika kuwahudumia wazee, Mhe. Lowassa anasema kama ilivyo kwa
nchi nyingine, Tanzania nayo inakabiliwa na ongezeko la idadi ya wazee.
Kwa
mfano, amesema asilimia 4.5 ya idadi ya watu, ni watu walio na umri wa
miaka 65 wastani wa juu zaidi kuliko ule wa asilimia 3.6 Afrika
Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“
Asilimia 80 ya watu hawa wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea
kilimo. Serikali inajitahidi kadri iwezavyo kutoa huduma za msingi kwa
kundi hilo ingawa pia, na kama ilivyo kwa nchi nyingine, tunakabiliwa na
changamoto nyingi kukidhi mahitaji yote ya wazee”. Akabainisha.
Akatumia
pia fursa hiyo kuyashukuru mashirika ya kimataifa kama vile Help Age
International ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake nchi nchi tangu
mwaka 1993.
Akatoa
mfano kwa kusema Shirika hilo, mwezi Juni mwaka huu kwa kushirikia na
Pfizer limezindua mpango wa miaka miwili wa kupunguza athari
zitokanazo na magonjwa yasiyoambukiza (NCD) ambayo yamekuwa yakiwaathiri
wazee.
Akasema utoaji wa huduma hiyo unakwenda sambamba na juhudi za serikali katika kukabiliana na magonjwa hayo.
Akatoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano huo na kwamba serikali itakuwa tayari kushirikiano nayo,Takwimu
kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu ( UNFPA)
zinaonyesha kwamba, katika kila sekunde watu wawili duniani
wanaadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa kwao, na kwa mwaka karibu watu
milioni 58 wanaadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa.
Aidha
katika kila watu nane, mmoja ana miaka 60 au zaidi na makadirio
yanaonyesha kwamba ifikapo mwaka 2050 katika kila watu watano mmoja
atakuwa na miaka 60 au zaidi.
Ongezeko
la idadi ya wazee duniani linachangiwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja
na ongezeko la umri wa kuishi ambapo katika nchi 33 raia wao wanaishi
zaidi ya miaka 80 wakati miaka mitano iliyopita nchi ambazo umri wa
kuishi ulifika miaka 80 zilikuwa 19 tu.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia