Chama cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha Dk John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Kwanza kabisa napenda kumpongeza sana Magufuli kwa
hatua aliyofikia na kumtakia kila la heri. Naomba kukiri kwa uwazi
kwamba katika uchaguzi unaohusisha vyama vya siasa ni lazima mshindi
atapatikana na kwa Tanzania ni lazima mshindi huyo atoke kwenye chama
cha siasa.
Tanzania ina vyama 22 vilivyosajiliwa na
vinavyofanya kazi sasa, tutake tusitake ni lazima rais wa nchi atatoka
katika chama kimojawapo, na kwa sababu CCM imeshapitisha mgombea wake na
yeye ana fursa ya kushinda uchaguzi kama ambavyo fursa hiyo ilivyo
kwenye vyama vingine. Natumia nafasi hii kufanya uchambuzi wa dhati juu
ya taswira ya serikali ya Magufuli ikiwa atafanikiwa kushinda uchaguzi
wa mwaka huu. Taswira ya namna hii pia nitaifanya kwa wagombea wengine
wa vyama ambavyo vitaamua kuweka wagombea urais.
Katika kulifanya jukumu hili nitachambua masuala
10 ambayo nafikiri kwamba yanaweza kujenga utawala wa Magufuli, ikiwa
atachaguliwa na Watanzania kuwa rais wa awamu ijayo.
Mambo matano kati ya hayo nayatazama kama taswira
bora na mengine matano yanaweza kuwa taswira hasi. Katika uchambuzi wa
leo nitaanza na mambo matano ambayo ni taswira bora.
Usimamizi bora
Taswira ya kwanza ambayo Magufuli anaweza
kuirejesha bila wasiwasi ni usimamizi thabiti wa serikali na nidhamu ya
utendaji ndani ya serikali. Naamini kuwa serikali ya Magufuli itakuwa ya
kiusimamizi na yeye mwenyewe anaweza kulifanya jambo hilo bila kusita.
Katika nyadhifa nyingi alizopitia hadi sasa ameijenga taswira hii kila
alikopita na bado inambeba hata ikitokea anachaguliwa kuwa rais wa awamu
ya tano.
Tukumbuke kuwa moja ya mambo ambayo yameanguka
kabisa nchini hivi ni utendaji ndani ya serikali. Tunafahamu kuwa
wafanyakazi ndani ya serikali ukiachilia mbali matatizo waliyonayo kwa
maana ya vipato, hata mambo madogo ambayo wangeweza kuyasimamia ndani ya
dakika au saa chache huchukua wiki kadhaa na hata miezi kadhaa.
Utaratibu wa utoaji huduma umekwama sana na nadhani kama akiwa na uwezo
huo atafanikiwa kutatua changamoto kubwa na ya siku nyingi. Ikiwa
utendaji wa serikali unaimarika na huduma zinatolewa kwa wakati,
tutaweza kujenga taifa linalokwenda mbele bila kujali chama gani kiko
madarakani.
Msimamo imara
Taswira bora ya pili ya serikali ya Magufuli
inaweza kuwa ni misimamo katika masuala ya msingi na kutoyumba sana.
Magufuli muda wote ambao amekuwa kiongozi ameonyesha jambo hilo. Kila
mara amekuwa na misimamo hata kama siyo sahihi. Kwa tafsiri nyingine hii
huwa ni njia bora ya uongozi wa nchi japokuwa misimamo ya serikali au
kiongozi mkuu wa serikali huwa haipaswi kuwa juu ya haki na matakwa ya
wananchi.
Moja ya mambo ambayo serikali iliyopita ilikosa,
ni pamoja na kukosa misimamo na kuwa na “double standard”. Mfano mdogo
tu ni kwenye mchakato wa katiba mpya ambapo Rais anayeondoka alisimamia
uanzishwaji bora wa mchakato huo, akaunga mkono katika hatua zote na
rasimu zote, lakini akaja kuwageuka wajumbe wa tume hiyo na rasimu yao
ya pili alipolihutubia Bunge Maalumu la Katiba. Naamini Magufuli si mtu
wa kugeuka na kuna masuala mengi anaweza kuyasimamia kwa dhati na kila
mmoja wetu akakubali kuwa, naam! Hapa kuna kiongozi anasimamia masuala
haya.
CHANZO:mwananchi gazeti
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia