Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa habari kutoka mitandao ya kijamii, kwenye vijiwe na
mijadala sehemu mbalimbali, majina hayo matano yanaaminika kwamba
yatatoka miongoni mwa watiania 10 ambao wametajwa zaidi katika mijadala
hiyo.
Sababu kuu mbili ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye mijadala hiyo na
hata na baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa Tanzania ni mbili. Mosi,
uzoefu wao ndani ya ungozi wa serikali na pili, nafasi yao ndani ya
chama, ama kama wajumbe wa NEC au Kamati Kuu.
Majina ambayo yanatazamiwa kwamba yanaweza kupenya Kamati Kuu ni
pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu wa
zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa; Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose
Migiro; Waziri Mkuu Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi
Maalum), Profesa Mark Mwandosya; Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani;
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Ujenzi, John
Magufuli;.
Kwa ujumla kundi la makada hao (hapo juu) kila mmoja ana nafasi ya
kupenya kwenye mchujo wa Kamati Kuu, lakini pia anakabiliwa na
changamoto kadhaa.
BILAL
Dk. Bilal ni Makamu wa Rais, katika hali ya kawaida ni vigumu
msaidizi namba moja wa rais aliyeko madarakani kukosa nafasi ya kupenya
ngazi hiyo hata kama ni kwa sababu tu za kiprotokali .
Mbali na wadhifa wake, Bilal anayetoka Zanzibar amepata kuwa Waziri
Kiongozi na ana uzoefu wa kuendesha serikali, kwa maana hiyo
anawakilisha kundi la upande mmoja wa Muungano na hivyo siyo rahisi jina
lake kutokuzingatiwa. Hata hivyo, Bilal ana changamoto ya umri kwani
kwa umri wa miaka 70 alio nao sasa inakuwa ni kazi kubwa kukimbizana na
changamoto za sasa katika nafasi hiyo.
LOWASSA
Lowassa ni mbunge wa Monduli, lakini pia alipata kuwa Waziri Mkuu
hadi alipojiuzulu Februari 2008 kutokana na kadhia ya Richmond juu ya
mkataba wa kufua umeme. Hata hivyo, kadri muda ulivyosonga hadi sasa
kadhia hiyo ilikuja kujidhihirisha kusukumwa zaidi na misuguano ya ndani
ya CCM hasa juu ya chuki za nafasi ya uwaziri mkuu.
Kama walivyo watia nia wengi, ni mjumbe wa NEC, amekuwa waziri
katika serikali ya Mzee Ali Hassan Mwinyi na ya Rais Benjamin Mkapa,
anaijua serikali vizuri.
Lowassa amekuwa gumzo kubwa miongoni mwa watia nia wote kiasi cha
kuandamwa hata na wapinzani wake ndani ya chama kwa kuwa tu kila wakati
kura za maoni zimeonyesha kuwa ni chaguo la kwanza la wananchi katika
kundi la wawania urais wote, ndani ya CCM na hata ndani ya upinzani.
Mwanasiasa huyo ambaye wengi waliamini kwamba kadhia ya Richmond
ilikuwa imemmaliza, aliigeuza hali hiyo kiasi cha kuonekana kuwa mtu
anayestahili kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mvuto
wake kwa wananchi wengi, umefanya wapinzani wake wajipange kumwandamana
kwa tuhuma mbalimbali, ambazo amezipuuza.
Wakati wa mchakato wa kutafuta wadhamini ndani ya CCM, Lowassa
alionyesha kwa vitendo halisi jinsi anavyoungwa mkono na wanaCCM
wenzake, kwani mikutano yake iligeuka kuwa ‘mafuriko’ kila mkoa
alikokwenda. Alidhaminiwa na wanachama zaidi ya laki nane.
Lowassa anaungwa mkono na wananchi wengi kwa sababu ni miongoni mwa
viongozi wa serikali wachache ambao wanatenda kwa vitendo halisi kuliko
kupiga kelele kwenye majukwaa ya kisiasa.
Anakumbukwa kwa ufuatiliaji wa karibu kwenye kila wizara aliyokuwa,
anakumbukwa kwa kusaidia Tanzania kunufaika na maji ya ziwa Victoria na
wakati akiwa Waziri Mkuu alianza kubadili mfumo wa utendaji serikalini
kutoka ‘business as usual’ na kuibua ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi
miongoni mwa watumishi wa umma.
WASIRA
Wasira ni miongoni mwa makada wa siku nyingi wa CCM, amehudumu kama
waziri katika serikali za awamu tatu, ya Mwalimu Nyerere; ya Mzee
Mwinyi na ya awamu ya nne, inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe, akiwa amejizolea umaarufu ndani
ya CCM na hata kwenye upinzani kwani mwaka 1995 alihamia NCCR-Mageuzi
na kugombea ubunge jimbo la Bunda na kumshinda, Jaji Joseph Warioba.
Hata hivyo, baadaye mahakama kuu ilitengua ubunge wake na kumtia hatiani
kwa kuhusika na vitendo vya rushwa katika uchaguzi.
Ingawa kiutendaji Wasira anaonekana kama mmoja wa watu wanaojituma,
kitendo chake cha kuhama CCM na kurejea tena kinaweza kuwa moja ya
sababu za kutumika dhidi yake.
MEMBE
Amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje tangu mwaka 2007 alipoondoka Dk.
Migiro kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN). Membe
aliingia bungeni mara ya kwanza mwaka 2000 wakati wa utawala wa Mkapa,
lakini ni chini ya Kikwete alipata nafasi ya kuwa Naibu Waziri, akianzia
Mambo ya Ndani na baadaye Nishati na Madini kabla ya kuibukia Mambo ya
Nje kama waziri kamili.
Ni mjumbe wa NEC kama walivyo makada wenzake. Kwa miaka mingi ya
utumishi wake Membe ambaye pia ni ofisa wa usalama wa taifa, alifanya
kazi nje ya nchi.
Duru za kisiasa nchini zinasema kuwa ingawa hana mizizi mirefu
ndani ya chama, kukaa kwake wizara ya Mambo ya Nje kwa muda huo kumempa
uzoefu wa uendeshaji wa serikali. Hata hivyo kumekuwa na maoni kuwa
Membe anabebwa na wakuu serikalini.
MIGIRO
Huyu ni mwanamke pekee anayepewa nafasi ya kufika mbali miongoni
mwa watia nia wote kwa sababu ya nafasi yake, kwanza ndani ya nchi na
nje alipokuwa UN. Anaelezwa kuwa na uzoefu wa ndani na wa kimataifa.
Katika kipindi hiki ambacho Rais Kikwete amekuwa anatoa fursa
nyingi zaidi kwa wanawake katika vyombo vya maamuzi, Dk. Migiro anaweza
kupenya kwenye kundi la tano bora hivyo kusaka kura za NEC kama anataka
kufika kwenye tatu bora kwenye mkutano mkuu.
PINDA
Huyu ni waziri mkuu tanu Februari 2008 alipojiuzulu Lowassa. Pinda
amekuwa mbunge tangu awamu ya pili ya Rais Mkapa na kuwa waziri wa
Tamisemi.
Muda wake mwingi wa utumishi alikuwa ndani ya Ikulu kama ofisa wa
serikali. Ni mwanasiasa ambaye kimsingi hajawa na kishindo sana licha ya
nafasi yake kubwa ya uwaziri mkuu.
Pinda amekuwa miongoni mwa mawaziri wakuu wapole ambao hawajaacha
kishindo kama alivyokuwa Waziri Mkuu pekee wa Rais Mkapa, Sumaye ambaye
alikaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka 10, lakini hakuacha kishindo
chochote pia.
Hata hivyo, kwa sababu za itifaki kama ilivyokwa Dk. Bilal, itakuwa
ni vigumu kumpiga panga jina lake katika ngazi ya Kamati Kuu, ingawa
wote umri nao umesogea, Bilal miaka 70 na Pinda miaka 67.
MWANDOSYA
Mwandosya ni mwanasiasa aliyeweka rekodi mwaka 2005 kwa kuingia
tatu bora katika kinyang’anyiro cha urais, akiachwa nyuma na Kikwete na
Dk. Salim Ahmed Salim.
Amekuwa moja ya nguzo ya siasa ya CCM kwa miaka mingi na ndiye
alianzisha mkakati wa harambee ya kuchangia chama kabla ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2005.
Amehudumu katika awamu mbili kama waziri, awamu ya tatu na ya nne.
Kwa kitambo alikuwa ndiye nguzo ya wanaCCM mkoani Mbeya, lakini kuibuka
kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe,
kama mmoja wa watia nia, kumeibua maswali mengi kama Profesa Mwandosya
bado anashikilia nafasi hiyo Mbeya na kanda yote ya nyanda za juu
kusini. Hata hivyo, umri wa miaka 66 wa Mwandosya siyo haba katika dunia
ya leo inayohitaji mchakamchaka.
SUMAYE
Sumaye aliweka rekodi ya waziri mkuu aliyekalia kiti hicho
mfululizo kwa muda mrefu zaidi ya mawaziri wakuu tisa kuwahi kuteuliwa
tangu uhuru.
Hakuna ubishi kwamba Sumaye ana uzoefu wa kuendesha serikali,
amekuwa naibu waziri, waziri na waziri mkuu kwa miaka 10. Alishikilia
ubunge wa jimbo la Hanang hadi alipoamua kustaafu mwaka 2005 baada ya
kuliwakilisha kwa miaka 20.
Ingawa Sumaye hana kikwazo chochote cha kisiasa kupenya hatua ya
Kamati Kuu, nguvu zake za kisiasa jimboni kwake zimepungua ndiyo maana
mwaka 2012 alibwagwa katika nafasi ya UNEC na Mary Nagu, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais (Mahisiano na Uratibu).
MAGUFULI
Dk. Magufuli amekuwa ni miongoni mwa mawaziri wachache wachapakazi
tangu awamu ya Rais Mkapa na hata sasa. Amekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi
na kisha Waziri wa Ujenzi wakati wa Mkapa na chini ya Kikwete amekuwa
Waziri wa Uvuvi na Mifugo, kisha wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi. Kila alikopelekwa amejitahidi kuchapa kazi.
Ni kati ya mawaziri wanaozijua wizara na majukumu yao sawasawa, ni
mfuatiliaji. Kwa utendaji huo, Magufuli amejijengea sifa ya kuwajibika
kama kiongozi.
Hata hivyo, kuna jambo kubwa ambalo limekuwa likiibuka kila wakati
juu ya kuhusika kwake na uuzaji wa nyumba za serikali. Ingawa inadaiwa
kuwa ulikuwa uamuzi wa baraza la mawaziri, bado wananchi wengi wamekuwa
wakihoji uamuzi wa kuuza nyumba hizo.
Mbali ya kuwa mbunge wa Chato tangu mwaka 1995, Magufuli hajawahi
kugombea nafasi nyingine ya kuchaguliwa ndani ya CCM. Siyo mjumbe wa NEC
na hakuna kumbukumbu zozote kwamba alipata kuomba nafasi hiyo.
POLISI WAMWAGWA DODOMA
Wakati Kamati Kuu ikikutana leo, kufyeka majina 33 ya wagombea na
kubakisha watano bora, Jeshi la Polisi linadaiwa kumwaga askari 200 wa
kikosi maalum katika mji wa Dodoma kulinda usalama.
Askari hao wanaodaiwa kutoka mikoa ya Manyara, Singida, Iringa na
Morogoro ni wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao walianza kuingia
mjini hapa jana mchana, ukiwa ni mkakati wa jeshi hilo kuongeza nguvu za
kukabiliana na jambo lolote la vurugu au uhalifu wakati wa vikao vya
CCM ya uteuzi wa mgombea urais.
Wakati vikosi hivyo vikielezwa kuingia katika mji wa Dodoma kwa
ajili ya kuongeza ulinzi, NIPASHE ilishuhudia Kikosi Maalum cha Askari
wa Farasi kikirandaranda katika viunga vya mji huo.
Ulinzi katika mji wa Dodoma umeimarika zaidi baada ya Rais Jakaya
Kikwete kuwasili makao makuu ya chama kuanza kibarua kigumu cha
kuiongoza Kamati ya Usalama na Maadili kuchambua kwa makini ubora wa
wanachama walioomba uongozi ama wanaoteuliwa katika ngazi mbalimbali za
chama kabla vikao vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe
kugombea uongozi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alipotafutwa na
NIPASHE kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala la ulinzi kuimarishwa, hakuwa
tayari kulizungumzia akisema kuwa ni masuala yanayohusu mambo ya ndani
ya Jeshi la Polisi.
Kesho Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) itayapigia kura majina matano
yatakayotoka Kamati Kuu na kupatikana majina matatu ambayo yatapelekwa
kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa chama hicho kwa ajili ya
kupigiwa kura ili apatikane mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya
CCM kugombea urais dhidi ya vyama vingine vya upinzani.
WAANDISHI WA HABARI WAPATA WAKATI MGUMU
Waandishi wa habari wanaoripoti habari kuhusu mfululizo wa vikao
vya mchakato wa uteuzi wa mgombea wa CCM jana walijikuta katika wakati
mgumu walipotakiwa na maofisa wa usalama kuondoka katika viwanja vya
Makao Makuu ya CCM.
Maofisa hao waliwataka waandishi hao kuondoka eneo hilo na kuwaacha
wapiga picha pekee kuendelea kuwapo eneo hilo kwa madai kwamba
hapakuwapo na hotuba wala mkutano wa aina yeyote ambao ungehutubiwa na
Rais Kikwete wala viongozi wa CCM Taifa.
Hata hivyo, maafisa hao wa usalama walishindwa kutambua kazi ya
uandishi wa habari siyo kuripoti tu hutoba za viongozi bali pia mambo
mengine ambayo wananchi wana haki kuyafahamu.
“Mtoke hapa, hamtakiwi waandishi wa habari. Watu waliopewa ruhusa
ya kubaki eneo hili kwa muda ni wapigapicha peke yao na hata wao
tutawaondoa. Halafu kuanzia sasa mkae sehemu moja na mnapotaka
kuzungumza na mtu aliye nje ya uzio mtumie lango kuu kutoka nje na siyo
kuzungumza nao mkiwa ndani ya ukuta na wao wakiwa ng’ambo ya barabara,”
alisema ofisa mmoja wa usalama.
WATA
TAKUKURU: HAKUNA ALIYEKAMATWA
Wakati mijadala mbalimbali ikiwa imetawala katika mitandao ya
kijamii tangu juzi kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) ilikuwa imewanasa baadhi ya wapambe wa mgombea wa kiti cha
urais, Makongoro Nyerere, wakiwa wanagawana fedha hotelini ili
kuwashawishi baadhi ya wajumbe wa Nec na baadhi ya wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa Taifa kumchagua, Takukuru imekanusha taarifa hiyo kuwa si ya
kweli.
Ujumbe huo kuhusu tuhuma za kukamatwa na rushwa kwa baadhi ya
wapambe wa mgombea huyo, zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe wa Nec na
baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu pia waliokutwa hotelini humo (jina
linahifadhiwa) wakiwa ndani ya chumba namba mbili wakipokea rushwa ya
kati ya Sh. 100,000 na 500,000.
Mkuu wa taasisi hiyo mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga, aliiambia NIPASHE kuwa:
“Natumia nafasi hii kukanusha habari hizo zilizotolewa kwamba si za
kweli. Taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na
habari za kukamatwa kwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kwa tiketi
ya Chama cha Mapinduzi Julai 7, mwaka huu ni uzushi.”
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi iwapo madai hayo
yana ukweli, Makongoro Nyerere alisema: “Walioeneza uzushi huo
wamenidonoa tu, hawajanigusa kwa namna yoyote. Hujuma zinafanywa na watu
ambao sifa yao imeshatiwa doa kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.”
“Watu sasa wamekwama, wanataka ionekane kila mtu ndani ya chama
anahusika na rushwa, wakati kila mtu anafahamu kuwa wanaoendekeza
vitendo vya rushwa ni watu wachache sana.”
KINGUNGE AMVAA NAPE
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge-Ngombale Mwiru, amesema kauli
zilizotolewa juzi na msemaji wa CCM, Nape Nnauye ni za kibabe na
zinalenga kuwanyima watu haki zao kikatiba na kikanuni.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Kingunge
alisema maneno yaliyotolewa juu ya kuteua bila kujali shinikizo la watu
au kikundi na kwa sababu ya muda hautoshi, hakuna mgombea
atakayeruhusiwa kukata rufaa yana utata na yamevuruga hali ya hewa.
Alisema kama CCM haijali shinikizo la watu ambao ni wanachama, inajali nini kwa sababu shughuli ya siasa ni kwa ajili ya watu.
“Wanasema sisi warithi wa Nyerere, lakini wazingatie Mwalimu
alisema nini juu ya chama. Mwalimu Nyerere alisema chama chetu katika
kutafuta wagombea, naongezea hasa wa urais, chama kisikilize watu
wanasema nini, ” alisema Kingunge.
Aidha, alisema kama ingekuwa wakati wa Mwalimu Nyerere mtu wa aina hiyo angefukuzwa na kuvuliwa uanachama wake.
Alieleza katika chama hakuna mtu zaidi kuliko wengine, hivyo wajitahidi kulinda na kuhakikisha umoja na nguvu unaendelea kuwepo.
“Baadhi yetu tunatumia nguvu kubwa sana kupambana na wanachama
wenzetu ukilinganisha na nguvu ya kupambana na wapinzani wetu. Ni hatari
sana. Sisi sote tujirekebishe tusipoteze nguvu zetu,” alisema Kingunge.
Alibainisha kuwa CCM haiwezi kusimama inapopambana yenyewe kwa yenyewe na kwamba inaweza kutokomea baharini.
Alisema wakiwapuuza watu wanasema nini wakaishia kujifungia kwenye kamati na kuona wanatosha watambue kuwa hawatashinda.
Akifafanua kuhusu madai ya msemaji wa CCM kuhusu muda wa ukataji wa
rufaa kuwa hautoshi, Kingunge alisema kauli hiyo ni ya ajabu
ukizingatia ratiba ya uchaguzi mkuu inajulikana siku zote wakati chama
hakijazaliwa jana.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia