Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza jijini Dar es Salaam juzi kuhusu makubaliano yaliyofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)baada ya kikao cha wenyeviti na makatibu wa vyama hivyo. Kulia ni mwenyekiti wa Chadema |
Dakika chache baada ya CCM kumpitisha Dk John Magufuli kuwa
mgombea wake wa urais, viongozi wa vyama vya upinzani wamesema
hawatishwi na Dk Magufuli na wanamuona kama kada wa kawaida miongoni mwa
wengi waliopo CCM na kwamba hawezi kuleta mabadiliko yoyote.
Wamesema vita yao ni kuondoa mfumo wa uongozi uliopo na si ya mtu mmojammoja.
Wakizungumza jana viongozi hao, hasa wanaounda
Ukawa, walisema wanajipanga kumtambulisha mgombea wao kesho na kila
Mtanzania atapata fursa ya kumfahamu.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema CCM inakabiliwa na tatizo la mfumo mbovu, hivyo vita iliyopo
inaelekezwa katika kukiondoa madarakani ili kuruhusu kitu kipya kuchukua
nafasi na kuwapa Watanzania uzoefu mwingine.
Alisema Ukawa haimhofii mgombea huyo kwa kuwa hata
sifa zilizotumika kumpata ni za chama chake na kwamba suala
linalozingatiwa ni hoja zenye mashiko mbele ya wananchi ambao
wamechoshwa na taratibu za siku zote kushughulikia kero zao.
“Ajenda na hoja tulizonazo ndizo zitakazotubeba
mbele ya wananchi… tutawapelekea ili waamue wakiwa na taarifa sahihi.
Kama ni kutowajibika au ufisadi ndani ya CCM, suala hilo linaanzia ngazi
ya juu mpaka kwa mwanachama wa kawaida,” alisema na kuongeza:
“Hatutegemei kashfa kama kigezo kikuu cha kumshinda mgombea wa CCM kwa kuwa hilo ni tatizo la mfumo wa chama kizima,” alisema.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi
alisema endapo wananchi wataachana na dhana ya kufuata itikadi na
wakaelekeza fikra na akili zao katika hoja za kampeni, watakuwa kwenye
nafasi nzuri ya kumchagua kiongozi bora.
“Hatustushwi na (Dk John) Magufuli kwa lolote na
mashambulizi yetu yatakuwa makubwa. Lengo letu la kuiondoa CCM
madarakani liko palepale,” alisema Dk Makaidi ambaye pia ni Mwenyekiti
wa NLD.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika
alisema mabadiliko ya mfumo mbovu wa utawala hayawezi kufanywa na mteule
yeyote wa CCM kwa kuwa chama hicho kimeahidi kufanya mambo yaleyale.
Alisema baada ya chama hicho kumaliza harakati
zake za kumpata mgombea urais, kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kumteua
Samia Suluhu Hassan aliyeshiriki uongozi wa kuichakachua Katiba Mpya.
“Hii inadhihirisha kuwa nchi itaongozwa na watu
walio nyuma ya pazia kuendeleza uchakachuaji badala ya kuheshimu matakwa
ya wananchi. Ufisadi utaendelea iwapo CCM itaendelea kutawala,” alisema
Mnyika.