Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
.
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapenda kuutaarifu umma kuwa shughuli ya Harambee
ya kuchangia ujenzi wa Msikiti wa Patandi uliopo wilaya ya Arumeru jijini
Arusha ambao umepangwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 15, 2015 na ambayo awali
ilitangazwa kuwa mgeni Rasmi katika Harambee hiyo angekuwa Mheshimiwa Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa
itasimamiwa na Mheshimiwa Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa
jimbo la Monduli.
Mabadiliko haya yanatokana
na Mheshimiwa Makamu wa Rais kukabiliwa na majukumu mengine ya Kitaifa na hivyo
kutoa ombi maalum kwa Mheshimiwa Edward Lowassa kumuwakilisha katika shughuli
hiyo jambo ambalo amekubali.
Kufuatia taarifa hii,
tunauomba umma na wananchi wote wenye nia njema kushirikiana nasi pamoja na
mgeni Rasmi atakayemuwakilisha Makamu wa Rais katika harambee hiyo inayolenga
kukusanya fedha ili kukamilisha msikiti huo ambao ulianza kujengwa mwishoni mwa
miaka ya 1990.
Msikiti wa Patandi upo
katika eneo wanalokaa wananchi wenye imani mbalimbali na waumini wanaoutumia msikiti
huu, wamekuwa wakijitoa kwa namna nyingi katika kusaidia kujenga mshikamano
baina ya jamii zinazowazunguka bila kuwa na vikwazo na pia wamekuwa wakishiriki
katika kuwasaidia watoto yatima na wengine wenye uhitaji katika kukabiliana na
maisha yao.
Kufuatia dhima hii na
mchango huo wa wanajamii wanaoswali katika Msikiti huu, Mheshimiwa Makamu wa
Rais ameona na imempendeza kuwa, shughuli hii ya uchangiaji ujenzi isisogezwe
mbele kumsubiri bali iendelee kwa kuwa anaamini Mheshimiwa Lowassa ni mzoefu katika
kufanikisha shughuli za aina hii na kwamba mchango wake katika jamii hasa
shughuli za harambee ni wa kutiliwa mfano. Tunawakaribisha sana kushirikiana
naye katika kufanikisha Harambee hii. Kumbukeni kutoa ni moyo na wala si
utajiri!
Imetolewa
na: Boniphace Makene
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais
Dar
es Salaam: 12 Mei 2015
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia