BREAKING NEWS

Thursday, May 14, 2015

WAKUU WA EAC WALAANI VIKALI KITENDO CHA MAPINDUZI YA RAIS NKURUNZINZA WA BURUNDI JAPO AYAJAFANIKIWA

Nchini Burundi, aliyekua mkuu wa majeshi Jenerali Godefroid Niyombare ametangaza Jumatano Mei 13 kuwa rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza amepinduliwa madarakani.
Meja Generali Niyombareh alisema wamechukua hatua hiyo baada ya watu wa Burundi kukataa kwa kinywa kipana awamu ya tatu ya urais wa Nkurunziza.
Jenerali huyo aliyetimuliwa na Nkurunziza mwezi februari alisema kuwa Nkurunziza alishindwa kuheshimu mwafaka wa amani mbali na sheria za kimataifa.
Wakati  Mapinduzi  hayo  yakitangazwa, Rais Nkurunziza alikuwa  nchini Tanzania kujumuika na viongozi wa kanda  ya Afrika Mashariki kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi tangu Nkurunzinza atangaze nia yake ya kuwania awamu ya tatu.
Baada  ya  tangazo  la  kupindulikwa  kwake, Rais  huyo  alipanda  ndege  kurejea  nchini  kwake  licha  ya  tangazo  la  kufungwa  kwa  mipaka  yote  na  viwanja  vya  ndege.
Kwa  mujibu  wa  taarifa  ya  BBC  asubuhi  hii  ya  mei  14, Ndege  ya  Rais  huyo  haikuweza  kutua  nchini  Burundi  na  badala  yake  ilirudi  tena  Tanzania  ambapo  mpaka  sasa  Rais  Nkurunzinza  yupo  jijini  Dar  es  Salaam- Tanzania
Rais kikwete alipohutubia waandishi wa habari Dar es Salaam akiandamana na Rais Nkurunzinza
Maafisa wa jeshi la Burundi wakisheherekea Barabarani Bujumbura
Raia wakisheherekea ''Mapinduzi''
Manuari za kijeshi zingali barabarani mjini Bujumbura
**************************
WAKATI HUO HUO…
Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki WALAANI Jaribio la Mapinduzi Burundi......Aliyetangaza Mapinduzi Asema Kiburi Chake Kimemponza
WAKUU wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamelaani jaribio la mapinduzi ya kumng’oa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi na kutaka Katiba ya nchi hiyo ifuatwe ili kudumisha amani na utulivu nchini humo.
Aidha, wameagiza mamlaka husika nchini Burundi kutangaza kusimamisha kwa muda uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike Juni 26 mwaka huu ili kurejesha hali ya amani katika nchi hiyo.
Akizungumza jana katika kikao cha ndani kilichofanyika kwa takribani saa nne kutokana na mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, Mwenyeikiti wa Mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete alisema hatua ya kufanya jaribio la mapinduzi halitasaidia kuleta amani katika nchi hiyo.
“Tumekuwa na vikao kwa muda wote tangu asubuhi mpaka muda huu tukijadili suala la Burundi. Tukiwa tunaendelea na vikao kukawa na mambo yanaendelea Bujumbura. Kama Jumuiya tunalaani mapinduzi ya Burundi na jumuiya inaona kuwa hatua hiyo hataisaidia kumaliza hali ya sasa, hivyo tunataka kuheshimiwa kwa Katiba."
Aliongeza: “Kwa hali iliyopo sasa nchini Burundi, Jumuiya inaona sio mwafaka kufanyika uchaguzi, hivyo tunaziagiza mamlaka husika nchini Burundi kutangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo na ufanyike ndani ya kipindi cha utawala wa uongozi wa sasa kwa muda usiozidi muda wa utawala wa sasa.
Aidha, Kikwete alisema jumuiya itaendelea kuzungumza na wadau wote katika kuhakikisha hali ya amani inarejea ili uchaguzi uweze kufanyika kwa uhuru na haki kwa kuzingatia katiba ya Burundi, sheria ya uchaguzi na kuzingatia maazimio ya Arusha.
“Pia tunalaani vurugu zinazoendelea, hivyo tunavitaka vyama vyote kuhakikisha wanazuia na kuacha vurugu. Jumuiya haitakubali kuona vurugu zinaendelea,” alisema.
Kikwete alisema wakuu wa nchi ya jumuiya hiyo, watakutana baada ya wiki mbili kufuatilia suala hilo na kuchukua hatua stahiki. Hata hivyo, pamoja na Rais Nkurunziza kuwapo nchini jana, hakuweza kufika katika ukumbi wa mkutano Ikulu.
Baadaye jioni ilielezwa Rais Nkurunziza anayeiongoza Burundi tangu Agosti 26, 2005 aliondoka kurejea nchini mwake, lakini habari ambazo zimetufikia asubuhi hii zinasema rais huyo alishindwa kutua jijini Bujumbura, Burundi na hivyo kurejea tena jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, mawaziri wa mambo ya nje na Katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Richard Sezibera walikuwa wa kwanza kuingia katika mkutano huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete aliingia ukumbini hapo majira ya saa 7.00 mchana ambako alifanya kikao cha ndani na mawaziri wa mambo ya nje wa EAC kwa saa moja kabla ya kuanza kuingia wakuu wa nchi za jumuiya hiyo.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliwasili ukumbuni hapo saa 8:12 mchana na kufuatiwa na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, na baadaye Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambao walifanya mkutano wa ndani kupitia na kujadili ripoti ya timu ya mawaziri wa mambo ya nje.
Wengine waliokuwamo kwenye kikao hicho, mbali ya Ramaphosa aliyemwakilisha Rais Jacob Zuma, mpatanishi wa mgogoro wa Burundi aliyeachiwa jukumu hilo na aliyekuwa Rais wa Kwanza, Nelson Mandela ambaye naye aliachwa jukumu hilo na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, pia alikuwepo Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola ambao ni mwenyekiti Maziwa Makuu.
Hata hivyo, hali ya hewa ilibadilika ukumbini hapo kwa waandishi wa habari na wajumbe mbalimbali wakiwamo wawakilishi wa mataifa mbalimbali baada ya kutokea taarifa za kufanyika mapinduzi nchini Burundi huku mkutano ukiwa unaendelea.
Hata Rais Kikwete ambaye alitoka nje ya mkutano kwa dakika kadhaa hakuwa katika hali ya kawaida na kukataa kuzungumza chochote baada ya waandishi wa habari kumtaka kuzungumzia kinachoendelea.
Machafuko Burundi
Wakati mawaziri na marais hao wa EAC wakiendelea na kikao jijini Dar es Salaam, vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti juu ya tukio la kupinduliwa kwa Nkurunziza ikielezwa kwa sasa jeshi limeitwaa nchi hiyo.
Mkuu wa Majeshi nchini Burundi Meja Jenerali Godefroid Niyombareh alikaririwa akisema maofisa waandamizi nchini humo wamemkana Nkurunziza kutokana na machafuko yaliyoibuka hivi karibuni baada ya kiongozi huyo kutangaza kuwania urais katika kipindi cha tatu mwezi ujao.
Alitangaza kuwa hadi sasa Kamati ya Ukombozi ya Taifa imeundwa kwa ajili ya kuiongoza kwa muda nchi hiyo.
Jenerali Noyombareh, alisema hatambui uongozi wa Nkurunziza kwa kuwa kitendo chake cha kuwania kipindi cha tatu cha urais ni kinyume na Katiba ya nchi hiyo.
Tangu jana mchana vikosi mbalimbali vya jeshi nchini humo vilitawanywa sehemu mbalimbali za Burundi, ikiwemo ofisi za mashirika ya Utangazaji ya Taifa hilo.
Katika ukurasa wa Twitter wa Rais Nkurunziza, umeandikwa kuwa jaribio la kupindua nchi hiyo la majenerali wa juu wa nchi limeshindikana.
Machafuko yalianza nchini humo tangu Aprili 26, mwaka huu na kusababisha zaidi ya vifo 20. Aidha pamoja na taarifa hiyo ya Niyombare, vyombo vingi vya habari vya kimataifa vimebainisha kuwa bado havijathibitisha mapinduzi hayo.
Maelfu ya wananchi wa Burundi wanaokadiriwa kufikia 50,000 wamekimbia nchi hiyo kwenda nchi jirani kuepuka machafuko hayo.
Tanzania pekee inakadiriwa kupokea zaidi ya wakimbizi 20,000 walioingia kupitia mipaka ya Kagunga wilayani Kigoma Vijijini, mkoani Kigoma na wengine Ngara, mkoani Kagera.
Niyombare, ambaye awali alifukuzwa kazi na kuvuliwa cheo cha Ukuu wa Usalama, alitangaza kuondolewa madarakani kwa Nkurunziza katika kambi ya jeshi huku akiwa amezungukwa na baadhi ya maofisa waandamizi wa jeshi na Polisi.
“Kutokana na kiburi na kutotii kwake matakwa ya jamii yake na yale ya kimataifa yanayomtaka aheshimu Katiba na Makubaliano ya Amani ya Arusha, Kamati ya Mapatano ya kitaifa, imeamua kumuondoa madarakani Rais Nkurunziza na Serikali yake,” alisema.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates