Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi.
Zulmira Rodgrigues, akiwasilisha mada katika warsha ya siku tatu
iliyofanyika katika kijiji cha Nyakahungwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza
kuhusu ushirikishaji jamii katika kuandaa na kutekeleza mikakati
itakayochangia kuzuia na kutokomeza unyanyasaji na dhulma zinazofanywa
dhidi ya watu wenye albinism iliyoshirikisha waganga wa asili, wauguzi na
wakunga, viongozi wa dini, walimu pamoja na watu maarufu iliyoandaliwa na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Mauaji
ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) yanayoendelea nchini yanatokana
na mitazamo hasi kitamaduni miongoni mwa wanajamii.
Hayo
yameelezwa na washiriki wa warsha ya siku tatu inayoendelea katika kijiji
cha Nyakahungwa kata ya Nyakahungwa wilayani Sengerema yenye lengo la
kubadili mitazamo iliyojengeka katika jamii na kusababisha madhara makubwa
kwa watu wenye albinism iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Warsha
hiyo ni miongoni mwa mlolongo wa warsha nne zitakazofanyika katika wilaya
za Sengerema, Mwanza, Kahama na Bariadi kwa kuzishirikisha jamii kuibua
masuala mbalimbali yanayobagua, kunyanyapaa na kuwatenga watu wenye
albinism katika maeneo husika.
Warsha
hizo zinafanyika katika kipindi ambacho kumetokea mauaji ya mtoto wa kike,
msichana na kijana wenye albinism wilayani Sengerema wakati tarehe 14 Mei
2015 mwanamke mmoja alikatwa mkono wilayani Bariadi.
Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Sengerema, Bw.
Bushaija Vicent (kulia), akitoa takwimu za idadi ya za wanafunzi wenye
albinism katika wilaya yake kwa Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO Bi.
Zulmira Rodgrigues.
Kwa
mujibu wa Afisa Maendeleo Jamii wilayani Sengerema Bwana Bushaija Vicent
kati ya shule za msingi 191 wilayani humo ni Shule zenye watoto wenye
albinism ni 14, Idadi yao ni 16 katika shule ya awali watoto 4 wana
albinisim, vyuo mbalimbali Sengerema vijana 4 wana albinism na katika Shule
za sekondari 48, watoto wenye albinism 4.
Akitoa
mada kuhusu uhamasishaji jamii katika masuala ya albinism, Mkuu wa Ofisi na
Mwakilishi wa UNESCO Bi Zulmira Rodgrigues amesema miongoni mwa masuala
ambayo warsha italenga ni kutafakari kwa kina kwa nini watu wenye albinism
wanauawa, kubaguliwa, kutengwa na mambo yanayosababisha Tanzania kuongoza
katika mauaji hayo ikilinganishwa na nchi nyingine ambazo pia zina watu
wenye albinism.
"Watu
wenye albinism hawauwawi katika sehemu nyingine duniani, kwa nini Tanzania?
Ikiwa mauaji hayo yako kwa wingi nchini Tanzania basi kuna tatizo kubwa
ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi, na si serikali, UNESCO wala taasisi
yoyote ambayo inaweza kuleta mabadiliko hayo isipokuwa jamii yenyewe,"
alisema Rodrigues.
Tatizo
kubwa lililotajwa kuhusiana na mauaji ya watu wenye albinism ni utamaduni
uliojengeka katika fikra za watu na kuwa na imani kwamba watu wenye
albinism si watu wa kawaida, hawana hadhi na hawastahili
kuishi.
Watu
wenye albinism ni watu wa kawaida wanaostahili heshima na kulindwa kama
binadamu wengine kulingana na kanuni na sheria za nchi na za kimataifa
zinazopinga ubaguzi wa rangi, jinsia, tabaka na kukatisha maisha ya mtu.
Tofauti ni kwamba rangi yao inatokana na ukosefu wa vinasaba asili
vijulikanavyo kama melanin, vyenye uwezo wa kuzalisha rangi ya
nywele, macho na ngozi.
Utamaduni uliojengeka katika jamii wa kuwabagua,
kuwatenga na kuwapuuza watu wenye ulemavu wa ngozi kumehalalisha mauaji
ambayo kwa hivi sasa imekuwa biashara ya kuuza viungo vya watu wenye
albinism kwa waganga wa asili kwa lengo la kupata utajiri, cheo na
madaraka.
"Mara
nyingi waganga wa asili wamekuwa wakitajwa kuwa ndio chanzo cha mauaji hayo
kwa ajili ya imani potofu ya kujipatia utajiri, vyeo na madaraka. Biashara
hiyo inaonekana kushamiri kwa kuwa hakuna mifumo mahsusi kudhibiti maafa
hayo," alisema mmoja wa washiriki anayeshughulikia masuala ya
usalama.
Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO Bi.
Rose Haji Mwalimu, akichangia mada kuhusu ushirikishaji jamii katika
kuandaa na kutekeleza mikakati itakayochangia kuzuia na kutokomeza
unyanyasaji na dhulma zinazofanywa dhidi ya watu wenye albinism
iliyoshirikisha waganga wa asili, wauguzi na wakunga, viongozi wa dini,
walimu pamoja na watu maarufu iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Katikati ni Mratibu ambaye pia ni
Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman
Mathias na Kulia ni Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi.
Zulmira Rodgrigues.
Akichangia mada wakati wa majadiliano yanayokusudiwa
kuzalisha mikakati ya kukomesha maovu hayo, Mratibu na Mkufunzi wa Redio
Jamii kutoka UNESCO Bi Rose Haji Mwalimu alisema kwamba wakati umefika wa
kutambua kitu gani kizuri katika tamaduni zilizopo zitakazoweza kusaidia
kuleta mafanikio na kuachana na zile ambazo hazina tija na zinasababisha
maafa katika maendeleo na ustawi wa jamii.
"Ni
kweli kuna changamoto nyingi katika jamii zinazosababishwa na kuhalalisha
tamaduni zinazolenga kupotosha badala ya kujenga. Tukiendelea kuzikumbatia
tutajikuta tunajenga taifa lisiloona mbali kimaendeleo kuhadaiwa na watu
wenye ubinafsi kutoka nje na ndio maana Tanzania imekuwa soko kubwa au
shamba lenye rutuba ya kupandikiza mbegu ambazo mavuno yake hupatikana kwa
urahisi", alisema Bi Mwalimu.
Katika
warsha hiyo washiriki walibaini maeneo makuu matatu ya kuyawekea mpango
kazi. Maeneo hayo ni Kuzuia mauaji, ubaguzi, unyanyapaa na kuwatenga, eneo
la pili ni kuwalinda watu wenye albinism katika maeneo ya makazi,
mashuleni, katika jamii na familia zao na la tatu ni hatua za kisheria wale
wote watakaoonekana kuhusika moja kwa moja au kwa namna nyingine katika
kuwatendea maovu watu wenye ulemavu wa ngozi kuanzia ngazi za kimataifa,
kitaifa, kifamilia na shuleni.
Mganga wa jadi kutoka kijiji Nyanzenda, wilayani
Sengerema, Maimuna Musa akizungumzia jinsi anavyotoa huduma za kutibu
watoto magonjwa mbalimbali ya watoto ikiwemo na huduma ya kuzuia mwanamke
asizae mtoto mwenye ulemavu wa ngozi.
Mganga wa jadi kutoka kijiji cha Nyakasungwa, Omary
Mongongwa akitoa msimamo kuhusu uwezo wa tiba kwa waganga wa jadi
unavyotofautiana na kuwasihi waganga wenzake wa jadi wanapojadili
wazungumzie kazi za mtu binafsi na utendaji wake na si kuusemea moyo wa
mganga mwingine.
Mzee maarufu kutoka kijiji cha Bukokwa, Felician
Buhumbi, akifafanua hatua zilizokuwa zikichukuliwa wakati wa Ukoloni dhidi
ya waganga asili wenye kupiga ramli chonganishi wakati wa warsha ya siku
tatu iliyofanyika katika kijiji cha Nyakahungwa wilayani Sengerema mkoani
Mwanza.
Sehemu ya washiriki wa warsha hiyo ya siku tatu
iliyowashirikisha, Waganga wa Jadi, Viongozi wa dini, walimu shule za
msingi na sekondari, wazee maarufu, Wakunga, Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora, Shirika la Under the Same Sun, Baraza la taifa la dawa
asilia, Afisa wa polisi wa dawati la jinsia pamoja na Maafisa wa mkoa wa
Mwanza na wa wilaya ya Sengerema.
Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi.
Zulmira Rodgrigues aliyeambatana na mbunge wa viti maalum CCM anayetetea
maslahi ya watu wenye albinism, Mh. Al-Shaymaa Kwegyir wakiwa kwenye picha
ya pamoja na washiriki.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia