Wafugaji wa Vijiji vya Enduimet na Tinga tinga vilivyopo wilaya ya
Longido mkoani Arusha wametakiwa kufuga kisasa ili waweze kuvuna mazao
bora ya maziwa na nyama ambayo watayauza na kukuza uchumi wao badala
ya kujivunia kuwa na mifugo mingi ambayo haina tija kiuchumi.
Akizungumza na Wafugaji wao kutoka vyama vya ushirika vya Wafugaji vya
Leo Pastoralist Cooperation pamoja na Tinga Tinga pastoralist
cooperation ,Mkurugenzi wa Shirika lisilokua la kiserikali la uhifadhi
wa Mazingira na viumbe hai la African Wild life Foundation (AWF)
upande wa Hifadhi ya milima Kilimanjaro ,Noah Sitati amesema kuwa
licha ya kupata manufaa ya kiuchumi wanayoyapata wafugaji hao pia
wanapaswa kuwasomesha watoto wao ili kuchochea maendeleo kwa jamii ya
Wafugaji.
Sitati amesema kuwa wako kwenye mpango wa kuwasaidia wafugaji hao
kupata madume ya kisasa yatakayowawezesha kupata mbegu bora za ng`ombe
wa maziwa na nyama hivyo kukuza uchumi wao.
"Ufugaji wa kisasa unaleta manufaa makubwa hata ukiwa na mifugo
michache ambayo utaitunza vizuri tofauti na kuwa na idadi kubwa ya
mifugo ambayo hawasaidii kuinuka kiuchumi" Alisema Sitati
Kwa upande wao Wafugaji kutoka vyama hivyo vinavyofadhiliwa na AWF
wameeleza kuwa vyama hivyo Hamisi Hassani na Isack Ole Ndereko
wamesema kuwa vyama hivyo vya usharika vinawasaidia kuwa na sauti
moja na kupiga hatua kiuchumi kupitia misaada ya kitaalamu pamoja na
fedha ambazo wanaziweka akiba na kukopeshana ili kukuza uchumi wa
wafugaji.
Afisa Programu wa Shirika la kimataifa la uhifadhi wa maliasili
International Union for Consevation of nature (IUCN) lenye makao
yake nchini Kenya,Akshay Vishwanath amesema kuwa umoja wa wafugaji
utawasaidia kukuza shughuli zao na ustawi katika kujiletea maendeleo .
Licha ya Tanzania kuwa moja kati ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na
idadi ya mifugo bado sekta ya ufugaji nchini haijachangia kukua kwa
uchumi kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na wingi wa mifugo,changamoto
ambayo ikitatuliwa huenda sekta ya ufugaji ikakuza uchumi na kuondoa
umasikini